Monday, June 13, 2011

Wabunge NCCR-Mageuzi nao wazikataa posho

SAKATA la kutaka kufutwa kwa posho za vikao nchi nzima zikiwamo za wabunge limezidi kupamba moto baada ya wabunge wa Chama cha NCCR-Mageuzi kutangaza kuliunga mkono.

Aidha wabunge hao wamesema watamuandikia Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo na Spika wa Bunge Anne Makinda, wakitaka posho zao za vikao kuanzia sasa zipelekwe kwenye fungu la miradi ya maendeleo ya mkoa wa Kigoma.

Pia wamesema katika bajeti ya mwaka huu wa fedha wa 2011/2012 kipaumbele cha miundombinu hakina umuhimu sana kama ilivyo kwa elimu, nishati, afya na kilimo.

Wamesisitiza kuwa pamoja na nishati kuwa moja ya vipaumbele vya kwanza katika bajeti hiyo bado fedha zilizotengwa katika kipaumbele hicho hazitoshelezi kufanikisha utekelezaji wa miradi ya nishati nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR) alisema wabunge wa chama hicho ambao wote wanatokea mkoa wa Kigoma wamekubaliana kutoa posho zao katika miradi ya maendeleo ya Kigoma ambapo kwa mujibu wake kila mwaka mkoa huo hutengewa kiasi kidogo cha fedha za ndani za maendeleo ikilinganishwa na mikoa mingine nchini.

Hivi karibuni akiwasilisha mwelekeo wa bajeti ya Kambi ya Upinzani kwa waandishi wa habari, Waziri Kivuli Zitto Kabwe(Chadema) alisema moja ya mkakati wa kupunguza matumizi makubwa ya fedha za Serikali ni kufuta posho za vikao, jambo ambalo liliungwa mkono na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe (Chadema) pamoja na wabunge wa chama hicho.

Alisema kwa upande wa wabunge wana malipo ya aina tatu ambayo ni mshahara, fedha za kujikimu wakiwa na majukumu ya kujikimu nje ya maeneo yao ya kazi na posho za vikao ambapo aliongeza kuwa katika fedha zote hizo fedha ya posho za vikao haina maana yoyote.

“Kwa sababu mshahara upo, ukiwa Dodoma au Tanga ilimradi ni nje ya eneo lako la kazi unapewa fedha ya kujikimu, sasa tena posho ya vikao ya nini, ndio maana tunasema si halali,” alisema.

Alisema kwa wabunge wanne wa chama hicho kwa siku hulipwa posho ya Sh 70,000 hivyo jumla ya fedha zote za wabunge hao kwa siku ni Sh 280,000 ambapo kwa siku 10 itakuwa ni Sh milioni 2.8 hivyo kwa muda wote watakaokaa bungeni watachangia kiasi kikubwa cha fedha katika miradi ya maendeleo ya Kigoma.

Alisema, mkoa wa Kigoma umekuwa ukipata fungu dogo la miradi ya maendeleo kwani hupata asilimia 27 tu ya fedha za matumizi ya ndani wakati mkoa wa Dar es Salaam pekee hupatiwa asilimia 47.

Kafulila alisema, katika kusisitiza juu ya mfumo mzuri wa matumizi ya fedha za Serikali, chama hicho kitapendekeza bungeni kufutwa kwa nafasi ya mkuu wa wilaya na makatibu tarafa nchini kwa kuwa nafasi hizo ni za kisiasa na zinaingilia wajibu wa wakurugenzi na wabunge.

Akizungumzia bajeti alisema, imeelemewa na madeni makubwa, misaada na mikopo na hivyo kuifanya bajeti hiyo kuwa tegemezi.

“Inasikitisha taifa lenye deni la Sh trilioni 11 bado tunazalisha umeme wa megawati 800 wakati robo ya deni hilo ingetosha kuzalisha megawati 3000 ambazo zimeingizwa kwenye mikakati ya Mpango wa Maendeleo ya miaka mitano.

Alisema suala la kuendelea kulilia misaada kwa wahisani ni aibu kwa Tanzania kwa kuwa nchi hiyo ni miongoni mwa nchi saba zinazopewa misaada kwa wingi duniani, baadhi ya nchi nyingine ni Ethiopia, Sudan, Iraq na Afghanistan ambazo hupatiwa misaada hiyo kwa wingi kutokana na vita na hali mbaya kiusalama. “Ndio maana nasema ni aibu Tanzania yenye amani kusaidiwa sawa na mataifa yenye hali tete ya kiusalama.

Aidha alisema bajeti ya umeme haitoshi ikilinganishwa na bajeti za nyuma za umeme. Alisema mwaka 2006/2007 sekta ya umeme ilitengewa asilimia 24, 2007/2008 ilitengewa asilimia 13.9 na mwaka 2008/2009 asilimia 12 wakati katika mwaka huu wa fedha 2011/2012 miradi ya maendeleo imetengewa Sh bilioni 4.9 na umeme nishati na madini Sh bilioni 530 ambayo ni sawa na asilimia 6.6 ya fedha za miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, mbunge wa Muhambwe Felix Mkosamali (NCCR) alisema baada ya kuwasilisha leo barua kwa Spika pia watawasilisha hoja ya kujadili kifungu cha Sheria kinachozungumzia posho za wabunge na kupendekeza kibadilishwe.

No comments: