Thursday, February 26, 2009

Mrejesho wa Semina za GDSS- Maandalizi ya Kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani.

Siku ya Kimataifa ya Wanawake (International Woman's Day -IWD) inaadhimishwa tarehe 8 Machi ya kila mwaka Ulimenguni pote. Ni sikukuu ya kidunia ya kusherekea mafanikio na harakati za wanawake katika nyanja za Uchumi, Siasa, na Kijamii. Siku hii ilianza kama tukio la kisiasa, na chimbuko lake ni kutoka katika tamaduni za nchi zilizokuwa jamuhuri ya Kisovieti ya Russia. Taratibu siku hii ilipoteza asili yake ya kisiasa na badala yake kuwa siku ambayo wanaume wanaonyesha/kueleza upendo wao kwa wanawake. Hata hivyo, dhana za kisiasa na haki za binadamu kama zilivyobuniwa na shirika la Umoja wa Mataifa-UN na kupenyezwa katika siku hii, zinaendelea kuwa imara, na kusadia harakati za kisiasa na kijamii za wanawake kuangaliwa katika hali inayotia matumaini zaidi.
Nchini Tanzania, wanaharakati wa haki za binadamu na Wanawake -TGNP na FemAct- wameendelea kuungana na wanaharakati wengine duniani kote katika maandalizi ya kuiadhimisha tena siku hii. Mara nyingi siku hii huadhimishwa kwa kuandaliwa mijadala ya wazi, semina, vipindi vya television na redio, na shughuli zingine ambazo zitaonyesha/kueleza harakati za kumkomboa mwanamke kimapinduzi zinazoendelea katika nchi yetu. Katika semina za kila jumatano za GDSS, wiki hii-tarehe 25/02/2009- wanaharakati waliweza kukutana na kujadiliana juu kuadhimisha siku hii muhimu. Wanaharakati waliweza kukubaliana juu ya kauli mbiu ya mwaka huu na waliona ni vyema ilenge/kuisisitiza serikali irudishe rasilimali kwa wananchi zaidi. Hivyo walikubaliana kauli mbiu ya mwaka huu iwe;
Kuwahudumia Wagonjwa wa UKIMWI Majumbani ni jukumu letu wote, Wanawake, Wanaume, na Serikali”
Wanaharakati walikubaliana na kauli mbiu hii na kuioanisha na mgogoro wa kiuchumi unaoendela duniani ambao unaongeza machungu na mateso kwa wanawake zaidi; kwa sababu mgogoro huu utasababisha upunguzwaji wa wafanyakazi katika sekta mbalimbali kwa mfano walimu, wafanyakazi wa afya na viwandani, na uchangiaji wa huduma za afya utazidisha machungu zaidi kwa wanawake. Utunzaji wa wagonjwa wa walioathrirka na VVU majumbani unaamanisha kuongezeka kwa mzigo wa kazi kwa akina mama majumbani, na shida zaidi ni kwa watu wanyonge-wasio na uwezo wa kifedha. Hivyo wanaharakati wanapendekeza haja ya kuilazimisha serikali iongeze rasilimali zaidi kwa watu wa aina hii ambao wana haki ya kudai rasilimali zaidi kutoka serikalini kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa hawa.

Pamoja na mambo mengine wanaharakati wanadai kuwepo na mfumo mbadala ambao utatoa fursa kwa wanawake, wazee, na watoto kupata huduma za afya kwa gharama za serikali tofauti na sasa ambapo sera zinasema hivyo lakini utekelezaji wake umekuwa wakusuasua sana. Wagonjwa wengi hawana hata fedha ya nauli ya kwenda klinic kuchukua dawa, achilia mbali fedha ya kununua vyakula vyenye virubisho! Wanaharakati wanadai siku hii ya wanawake duniani mwaka huu iadhimishwe ili kutoa fursa kwa jamii yetu kuwa na upendo na akina mama kitu ambacho kitasaidia kuwalinda na kuwaenzi akina mama kama wazazi na watu muhimu katika maisha ya kila siku.

Wanaharakati wametoa wito kwa wanajamii kuiadhimisha siku hii kwa kuwatetea wanawake ili wapunguziwe mzigo wa kazi uliotokana na mfumo wa jamii yetu.

Ukiwa kama mwananchi wa kawaida unashiriki vipi katika kuiadhimisha siku hii muhimu? Na kuhakiksha juhudi zako zinaleta mabadiliko katika maisha ya wanawake wengi hasa wale wanyonge?

Jiandae katika ushiriki wa Siku hii Muhimu tarehe 8 Machi, 2009!

Tuesday, February 24, 2009

Mtoto wa miaka 10 apewa ujauzito Kenya


Mtoto huyu mwenye umri wa miaka 10 amepewa ujauzito hivyo ameharibiwa maisha yake kwani hataweza kuendelea na masomo kwa kipindi kirefu akimlea mtoto wake. Hii ni sawa jamani?

Kampuni 25 zilizochota CIS kufilisiwa

Kampuni ya Msolopa Investment Limited iliyopewa jukumu la kukusanya madeni ya Sh bilioni 199 zilizochotwa serikalini kupitia mpango wa Uagizaji wa Bidhaa Nje (CIS) imeomba ulinzi wa polisi kwa ajili ya kukamata na kutaifisha mali za kampuni 25 zinazodaiwa deni hilo.

Wakala huyo alitoa wiki mbili kwa baadhi ya wabunge na mawaziri wakiwamo wastaafu 40 ambao kampuni zao zimetaifishwa pia kuchota pesa hizo wawe wamelipa vinginevyo, atawaanika katika vyombo vya habari sambamba na kutaifisha mali zao.

Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Ibrahim Msolopa alisema kati ya kampuni 30 (tofauti na hizo za wabunge na mawaziri) zilizopewa wiki mbili kulipa madeni hayo, kampuni tano pekee ndiyo zilijitokeza kuanza kulipa madeni.

Alizitaja kampuni tano zilizoanza kurejesha fedha kuwa ni Shela Beach Investiment, Chichi Enterprises, Paninye Investments, Simba Resources na Avicena Pharmaceutical.

Kampuni 25 ambazo wamiliki wake wameendelea kukaa kimya ambazo alisema zitakamatwa wakati wowote baada ya kupata ulinzi wa Polisi, ni Kiex Trading inayomilikiwa na Rajabu Maranda ambaye anatuhumiwa kuchukua fedha za Akaunti za Madeni ya Nje (EPA) na mfanyabiashara Andrew Traders.

Nyingine ni K. Agencies International, Chawe Transport, Sikute Enterprises, Danico Ltd, Apemac, Dar es Salaam International School Trust Fund, Oriental Transport, Auxi Pharmaceutical, Family Care Clinic Pharmacy, Aliya Investiments, Agriculture Sales, Kashif Traders na Rein.

Alizitaja kampuni nyingine kuwa ni Twins Investments, Road Conqueres, Getca International, Dodoma Oil Mills, Shivji & Sons, Tyre Centre, Rela Investments, Amazon Trading, Transport Import & Export na Pharmavet. Kwa mujibu wa Msolopa, wameshamwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kuomba ulinzi kwa ajili ya kuendesha operesheni hiyo ya kukamata kampuni hizo.

Alisema baada ya kumaliza kukamata na kutaifisha mali ili kufidia madeni, ifikapo Machi 15 mwaka huu, wataanza kukamata mali za mawaziri na wabunge walioko madarakani na waliostaafu, ambao wako ndani ya kundi la kampuni 40 waliokaidi kulipa madeni.

Alisema mawaziri na wabunge wanaendelea kulipa fedha zilizochotwa na wengine walianza kulipa baada ya wafanyakazi wa kampuni hiyo kuwafuata bungeni katika Mkutano wa Bunge uliopita lakini wapo ambao hawalipi kabisa licha ya kuwa na taarifa za kudaiwa.

Akizungumzia kiasi cha fedha kilichokusanywa mpaka sasa, Mkurugenzi huyo alisema wameishawaandikia makamishna wa sehemu nne zinazotumika kulipia madeni, ili kutambua kiasi cha fedha kilichokusanywa ambacho watakitangaza kwa umma ili kukifahamu baada ya kampuni hiyo kuanza kazi ya kukusanya madeni hayo.

Alisema wadaiwa wa fedha hizo hulipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), benki za NMB, CRDB na ya Rasilimali Tanzania (TIB). Alisema serikali ilizikopesha kampuni 916 Sh bilioni 199 kwa lengo zuri lakini zilitumika kwa madhumuni yasiyokusudiwa, kampuni zingine 80 zilikuwa zimeishalipa fedha zilizokopa na nyingine ziliendelea kulipa isipokuwa hizo 30.

Daily News; Monday,February 23, 2009

Utumwa wa "hiari" waja

Sasa tujiandae kushuhudia watoto wetu wakikimbilia utumwani kwa maelfu. Wazazi na ndugu wa karibu wa vijana wa Afrika wanatakiwa wajiweke tayari kisaokolojia kukabiliana na upotevu wa vijana wao watakaoondoka hivi punde kujipeleka katika utumwa wa hiari.

Wanakwenda wapi? Si kwingine bali ni kule kule Marekani ambako walipelekwa mamilioni ya Waafrika waliouzwa huko kama punda wabeba mizigo, Waafrika ambao ndio waliojenga ukwasi mkubwa wa Marekani.

Sasa Marekani wanaye rais mweusi, ambaye ushindi wake umeshangiliwa sana na Afrika na dunia nzima kwa ujumla. Sasa, huyu rais mweusi anataka watu wengi wa kujitolea, hasa weusi, kwenda kumsaidia kupigana katika vita ambazo vijana wa Marekani wenyewe wanazikacha, kama hii ya Afghanistan.

Marekani wanasema sasa kwamba kijana ye yote asiyekuwa raia wa Marekani anayetaka kuwa raia atapewa uraia ndani ya miezi sita, MIEZI SITA TU, alimradi awe tayari kujiunga na majeshi ya Marekani kwenda kupigana Afghanistan na kwingineko kulikoungua shoka ukabaki mpini.

Utaratibu huu ulikuwa haujafanyika tangu mwisho wa vita ya Vietnam, ambayo, kwa ukali wake, ilihitaji vijana kutoka mataifa mengi duniani, hasa kutoka dunia ya tatu, na waliojitolea wakahongwa biskuti ya uraia.

Habari hizi bila shaka zitakuwa na ladha ya Bongo Flava kwa vijana wetu wanaopita wakisema, “Bora mbwa Ulaya kuliko Mswazi Bongo”. Watahamia Marekani, tena kwa wingi, siyo tu kwa sababu wameitwa kwenda huko bali pia kwa sababu nchi hii haielekei kujua ni nini inataka kufanya na vijana wake. Wameachwa wanamea kama magugu katika mahame. Hawajajengewa matumaini katika maisha yao ya baadaye na ni kweli kwamba wanaweza kuamini kwamba ni bora kuwa mtumwa Ulaya kuliko kuwa “huru” Afrika.

Ndivyo stori kutoka barani kote Afrika zinavyoonyesha, kama kule Senegal, ambako vijana wanasema, kama kufa na wafe, lakini hakuna kubaki Afrika, na mama zao wanakubaliana nao!

Friday, February 20, 2009

Trekta kwanza vitambulisho visubiri

BAADA ya miaka mingi ya danadana kuhusu uanzishwaji wa Vitambulisho vya Taifa, hatimaye Wizara ya Mambo ya Ndani imetangaza kwamba kampuni sita zimepita kwenye mchujo wa awali wa wazabuni wanaopendekezwa kutengeneza vitambulisho hivyo. Mradi huo unatarajiwa kugharimu takribani Sh. bilioni 222.

Tunafahamu hii ni habari njema, kwa wakati huu, kwa kuzingatia kuwa mradi huo umekuwa kwenye kauli zaidi kuliko vitendo, ukitawaliwa na utata, kificho na danadana nyingi, tena kwa muda mrefu mno. Tunasema ni habari njema kwa wakati huu, kwa sababu mchakato wa kuzichuja kampuni hizo sita zilizoingia kwenye kinyang’anyiro cha mradi huo, bado unaweza kuchukua muda mrefu na kuingiwa na danadana nyingine zaidi.

Lakini pia, kwa mtazamo wetu, kwa kuzingatia matakwa ya nchi hivi sasa, tunaona suala la Vitambulisho si kipaumbele cha maendeleo kwa sasa. Tulipaswa kuangalia matakwa ya sasa ya wananchi, na mazingira tuliyomo, ya mtikisiko wa uchumi duniani na upungufu wa chakula kutokana na baadhi ya vyakula kutumika kama nishati.

Kwa maana hiyo, kwa maoni yetu kwa kuangalia mahitaji ya sasa ya nchi, mradi wa Vitambulisho vya Taifa unaweza kuwekwa pembeni, na wala tusidhurike, ili hizo Sh. bilioni zaidi ya 200 zitumike, kwa mfano, kununulia matrekta yatakayoongeza kasi ya kilimo nchini yakituzalishia chakula na fedha ili tukiwa na shibe na tuna ‘vijisenti’ katika mifuko yetu hapo tuulizane nani ni nani.

Kwa nini tunasema haya leo? Kwa miaka mingi, tangu wazo la kwanza la kuwa mradi huu lilipoota, hakuna kitu kilichofanyika, badala yake watu wamekuwa wakikodoa macho kutaka kuona nani atafaidi nini kutokana na mradi huu, na Mungu bariki, kwa miaka yote hakuna Mtanzania aliyeteseka kwa kuwa hana kitambulisho; na hiyo ni pamoja na ukweli kwamba huo ndio wakati ambao nchi hii ilijaa watu: wakimbizi kwa malaki, ambao sasa wamerudi makwao.

Bila Vitambulisho vya Taifa, nchi imeendelea na mambo yake kama kawaida ikizama katika matatizo yetu makubwa lakini ya kawaida: njaa, afya, elimu, miundombinu, na mengineyo.

Sisi tulidhani sasa wakati umefika wa kuachana na mradi huu, pamoja na umuhimu wake wote, walau kwa muda, ili tuelekeze nguvu zetu katika mambo kipaumbele.

Sasa tunakabiliwa na njaa, tena katika mikoa ambayo huko nyuma ilikuwa ni aibu kuitaja kuwa ina njaa, badala ya Vitambulisho fedha hizi zitumike kwenye zana na pembejeo za kilimo, ziboresha elimu yetu ambayo imepanuliwa bila vifaa na miundombinu ya kutosha, ziboreshe huduma za afya, ujenzi wa barabara na usambazaji wa nishati.

Hatuwezi tukajitokeza hadharani leo hii, mbele ya ulimwengu, tukiwa vifua mbele, tukadai kuwa Vitambulisho vya Taifa ni bora zaidi kuliko matrekta na pembejeo kwa wakulima, au hata maabara, vitabu na walimu kwenye shule zetu. Kwa hakika, tukiwa na mawazo hayo tutashangaza watu.

Wakati mwingine dhana nzima ya Vitambulisho hakika inaghilibu akili. Hebu fikiria vitambulisho hivyo vitatumia teknolojia ya kisasa, hii maana yake ni kwamba vitahitaji umeme au mitambo inayoendeshwa kwa umeme.

Lakini sehemu kubwa ya jamii yetu ipo vijijini, ambako umeme bado ni kitendawili kikubwa, ni huko pia kwenye zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wote, wanaotegemea kilimo, hata kama bado ni kilimo duni. Kitambulisho kinachotumia teknolojia hiyo kitatumikaje na kitamsaidia nini mkulima huyu ambaye haoti kupata umeme leo wala kesho?

Inatosha kuwa wazi kwamba sasa tuangalie mambo ya kipaumbele kwa maendeleo na faida ya jamii pana. Inawezekana Vitambulisho vya Taifa vilikuwa kipaumbele nyakati fulani siku zilizopita. Kwa leo, ukichanganya na anguko la uchumi duniani kote, hakika kununua vitambulisho ni kati ya matumizi yasiyokuwa ya lazima. Si kipaumbele cha maendeleo. Tunasubiri kuona huyo Mtanzania atakayenunua kitambulisho sampuli hii, ilihali kwake hakuacha mchango wa meza.

Raia Mwema, 18 Februari, 2009.

Thursday, February 19, 2009

Mrejesho wa GDSS

Katika semina za GDSS jumatano ya tarehe 18/02/2009 mada ilikuwa ni juu ya “Mawazo Mbadala Kuhusu Mgogoro wa Kiuchumi wa Dunia na Mkutano Mkuu IMF na Afrika wa Machi 10-11” Wawasilishaji mada walikuwa ni Bashiru Ally (UDSM) na Morjorie Mbilinyi (TGNP) na washiriki kuweza kuibua hoja mbalimbali.

Bashiru(pichani) aliuhusisha mfumo wa sasa wa soko huria na chanzo chake ambacho ni enzi za biashara za utumwa, ukoloni, ukoloni mamboleo, mpaka utawandazi wa sasa. Tangu mwanzo mfumo huu wa kinyonyaji haukuwa na mafanikio mazuri, na umekuwa na migogoro mara kwa mara na kuyafanya mataifa ya kibepari-ubeberu kuendelea kubuni mbinu mpya ya kuendeleza unyonyaji wao. Waafrika na mataifa mengine duniani kote ambayo yalikuwa yakinyonywa na mabepari hao waliendeleza mapambano ya kudai haki zao zilizokuwa zikichukuliwa kwa nguvu. Mbinu mbali zilitumiwa na waafrika na mataifa haya ya duniani ya tatu, baada ya uhuru ule wa bendera wa miaka ya 1960, kwa mfano hapa Tanzania tulifuata mfumo wa usawa na kujitegemea.

Mgogoro wa uchumi unaoendelea dunia, unamaanisha kwamba mfumo wa kibepari-ubeberu unaendelea kushindwa kama ulivyoshindwa huko awali. Kwa maoni yake(Bashiru), mgogoro huu una sura mbili kwa Watanzania na Afrika. Sura ya kwanza; Watanzania wanaweza wakashindwa kabisa kujinasua katika mgororo huo, na mfumo wetu wa kiuchumi kuumizwa vibaya. Sura ya pili; mgogoro huu unaweza kutoa fursa kadhaa, ambazo ni pamoja na; kuweza kutambua kwamba kuathiriwa kwetu vibaya katika kipindi hiki kumetokana na kufuata mfumo wa utegemezi kuendesha serikali na nchi yetu, njia tuliyoshauriwa na IMF/WB na hivyo kupata fursa ya kujipanga na kutafuta njia mbadala. Fursa ya pili ni kwamba tunaweza kupunguza utegemezi na kuweza kupanga mipango ya maendeleo kulingana na mazingira, mifumo, taratibu na changamoto zetu zinazotukabili. Fursa ya tatu ni kuepuka kupanga mipango ya uchumi na maendeleo kwa kutegemea wawekezaji na wafadhili katika utekelezaji, kitu ambacho Bashiru alikiita ni kupanga mipango ya kiuchumi ya “kikamali”. Furasa nyingine ni kuweza kujiamini na kupata uwezo wa kufanya maamuzi magumu zaidi hivyo kujiletea maendeleo halisi.

Morjorie naye aligusia juu ya hatua/mbinu zinachukuliwa na mataifa tajiri katika kupambana na mgogoro huu wa kiuchumi ambazo alizitaja kuwa ni pamoja na; kupunguza riba; kutoa mikopo; serikali kuendelea kuungilia uchumi na biashara ya nchi husika; ambaye yeye (Morjorie) aliona hatua hizi ni sawa na kuanzisha mfumo wa Ujamaa kwa matajiri.

Alitaja madhara ya mgogoro huo wa kiuchumi kwa Afrika ni pamoja na; kukosekana kwa masoko kwa bidhaa za Afrika na kushuka maradafu kwa bei za bidhaa hizo, kukosekana kwa mikopo kwa wafanyabiashara, fedha za kigeni kupungua zaidi, bei ya chakula na nishati-hasa mafuta kuendelea kuongezeka, vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja kuongezeka maradufu, biashara haramu za ngono na ya kusafirisha watu kushamiri, na maliasili zetu kuendela kuporwa na wageni.

Pia Morjorie alielezea kuhusu migogoro inayeondelea hapa nchini na harakati za wananchi kugombea mgawanyo bora na sahihi wa maliasili zilizopo, na kuoanisha migogoro hiyo na mgogoro wa kiuchumi duniani. Kwa mfano; Migomo katika sekta ya elimu, wananchi kuzuia misafara ya viongozi, DC aliyewachapa viboko walimu, na mapigano ya wakulima na wafugaji. Na kuongeza, “hali hii isipodhibitiwa mapema itakuwa na madhara makubwa katika kipindi hiki cha mgogoro mkubwa wa kiuchumi duniani”

Tufanye nini?
Katika tufanye nini wanasemina walikubaliana mambo makuu ambayo ni muhimu yakafanyika katika siku hizi mbili za mkutano huu wa IMF na Afrika Machi 10-11.
1. Wanasemina walipendekeza maandamano ama mkutano kwa siku mbili nje ya jengo la mkutano huo na kuishinikiza IMF iondoe sera zake za ukandamizaji dhidi ya Afrika na Tanzania.
2. Liandaliwe tamko kwa vyombo vya habari ambalo litakuwa na msimamo na Ujumbe wa wanaharakati kwa IMF na washirika wao duniani kote.
3. Wanaharakati watumie vyombo vya habari kwa ajiri ya kutandaa na kuweza kufanya harakati za pamoja za kupingana mfumo huu kinyonyaji na kusaidia watu wengi kupata taarifa zaidi za mfumo huu wa unyonyaji na mkutano huu mkuu, hivyo kuwawezesha kushiriki katika harakati hizi za ukombozi huu wa pili wa bara la Afrika!

Harakati Daima!

Habari zaidi bofya:
http://www.imf.org
http://www.changes-challenges.org/

Wednesday, February 18, 2009

Mchungaji akutwa na viungo vya Albino

Mchungaji wa Kanisa la Pentecoste lililopo Idiwili Kata ya Iyula, wilayani Mbozi anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kukutwa na mabaki ya mwili wa binadamu yaliyokuwa yakiuzwa Sh milioni 30.

Cosmas Mwasenga (39) alikamatwa Februari 13 mwaka huu akiwa na Luseshelo Mwashilindi ambaye inadaiwa alikuwa ameyahifadhi nyumbani kwake mabaki hayo. Mabaki hayo ambayo Polisi inahisi kuwa ni ya albino, ni vipande vinne vinavyosadikiwa kuwa sehemu ya mikono.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Zelothe Stephen alisema leo kuwa watuhumiwa hao walikamatwa katika eneo la Mlowo, Mbozi. Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Zelothe alisema Februari 12 mwaka huu, polisi walipata taarifa kuwa kuna kikundi cha watu Mlowo, wana vipande vya mabaki ya mwili wa mwanadamu vinavyosadikiwa kuwa ni mabaki ya mwili wa albino.

Alisema taarifa hizo zilidai kuwa kikundi hicho kilikuwa kinatafuta wateja ili kuwauzia vipande hivyo na kwamba watu waliokuwa wanatafuta wateja waligawanyika katika Wilaya ya Mbozi na baadhi ya mitaa ya Jiji la Mbeya.

“Tuliweka mtego na kukutana na watu hao ambao walisema wanauza viungo vya ‘kunguru mweupe’ wakimaanisha albino, ambapo walikubaliana na kukutana na Mwashilindi ambaye alikuwa anahifadhi viungo na kufikia makubaliano ya kuvinunua kwa Sh milioni 30,” alisema.

Alisema Februari 13, taratibu za kupata kiasi hicho cha fedha zilikamilika na walipofika kwa Mwashilindi alitoka akiwa na vipande vinne vya mabaki ya binadamu vikiwa vimefungwa katika karatasi, na Polisi wakamkamata. “Baada ya kupekua katika nyumba ya Mwashilindi tulifanikiwa kupata dawa za binadamu, maji ya kuchanganya na dawa na koti jeusi mali ya Mchungaji Mwasenga,” alisema.

Aliongeza kuwa watuhumiwa wote wawili wanashikiliwa na watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika. Kamanda Zelothe alisisitiza umuhimu wa wananchi kutoa taarifa Polisi na kusema kwa kufanya hivyo, ndipo vitendo vya mauaji ya albino vitapungua. “Tunapenda kuwaomba wananchi waendelee kutoa taarifa za siri kwa viongozi wa juu, ili ziweze kufanyiwa kazi haraka,” alisema.

Daily News; Tuesday,February 17, 2009

Tuesday, February 17, 2009

18/2/2009 GDSS : ALTERNATIVE VIEWS ON GLOBAL ECONOMIC CRISIS AND IMF's AFRICA SUMMIT IN MARCH

Gender and Development Seminar Series

You are invited to the weekly Gender and Development Seminar Series session in which Bashiru Ally (UDSM) and Marjorie Mbilinyi (TGNP) will make a presentantion on the;

Alternative Views on Global Economic Crisis and IMF's African Summit in March!

Date: 18th February, 2009

Time: 3:00 pm - 5:00 pm

Venue: TGNP Grounds / Adj.NIT

Please confirm your participation through
info@tgnp.org

Come One Come All !!!!!!

Monday, February 16, 2009

Ukimpenda Hutampiga, Utamjali na Utamheshimu!


Ukimpenda Mwanamke hautampiga na utamheshimu, Sema hapana kwa Ukatili wa kijinsia!

Friday, February 13, 2009

Wabunge kujadili nyaraka za Mkapa


SERIKALI imebanwa na Bunge, kiasi cha kulazimika kuanza kufikiria uamuzi wa kisheria na hata kutafakari fursa ya kumwondolea kinga Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, au kutafuta uwezekano wa kumhoji kuhusu mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira mkoani Mbeya, anaodaiwa kuwa mmoja wa wamiliki, kupitia kampuni ya ANBEN.

Mbinyo huo wa Bunge dhidi ya Serikali unatokana na kile kinachoelezwa kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kunasa nyaraka zinazobainisha kuwa Rais Mstaafu Mkapa ni mmoja wa wamiliki wa mgodi wa Kiwira, nyaraka ambazo baadaye zilifanyiwa mabadiliko ili kumwondoa Mkapa katika wingu hilo.

Nyaraka hizo ambazo Raia Mwema imefanikiwa kuziona zinabainisha kuwa Mkapa pamoja na mkewe Anna ni wamiliki wa hisa katika mgodi wa Kiwira kupitia kampuni yao ya ANBEN. Hata hivyo, kutokana na mwenendo wa mambo na hasa baada ya suala hilo kuonekana kumweka pabaya kisiasa na kisheria Mkapa, umiliki wa mgodi huo ulifanyiwa mabadiliko.

Katika mabadiliko hayo, nyaraka za sasa zinabainisha kuwa mgodi huo unamilikiwa na kampuni ya Tanpower Resources Ltd, ambayo ni muungano wa kampuni nne tofauti.

Kampuni hizo ni Fosnick Ltd, ambayo wanahisa wake ni Nick Mkapa, Foster Mkapa na mwingine aliyetambuliwa kama B. Mahembe, kampuni nyingine ndani ya mwavuli wa Tanpower Resources ni Choice Industries ambayo wanahisa wake ni Joe Mbuna na Goodyear Francis, nyingine ni Devconsult Ltd yenye wanahisa D. Yona na Dan Yona jr, wakati kampuni ya nne ni Universal Technologies Ltd ambayo wanahisa wake ni Wilfred Malekia na Evans Mapundi.

Raia Mwema imedokezwa kuwa tayari nyaraka za awali (original) zenye kuonyesha kuwa mgodi wa Kiwira unamilikiwa na kampuni ya ANBEN ambayo ni ya Mkapa, zimefikishwa katika uongozi wa juu wa Bunge.

Kwa mujibu wa habari za uhakika zilizotufikia inaelezwa kuwa nyaraka hizo zimejitosheleza kiushahidi kwamba Mkapa ni mmiliki wa ANBEN kampuni ambayo inahusika katika umiliki wa mgodi wa Kiwira.

Kutokana na hali hiyo na hasa kile kinachobainika kuwa Bunge kupitia Kamati yake ya Nishati na Madini kuridhishwa na ushahidi katika nyaraka hizo, muhimili huo wa Taifa umedhamiria kuibinya Serikali katika mambo makuu mawili.

Jambo la kwanza ni kushinikiza mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira kurejeshwa serikalini kutokana na sababu kadhaa lakini kubwa zaidi ni wawekezaji wanaopaswa kuendesha mgodi huo kubainika kuwa ni wababaishaji walioshindwa kutekeleza ahadi zao kwa Serikali.

Source:Raia Mwema, Februari 11, 2009

Thursday, February 12, 2009

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MADAI YA WANAHARAKATI KUPINGA TAMKO LA WAZIRI WA SHERIA NA MAMBO YA KATIBA KUHUSU SHERIA YA MAKOSA YA KUJAMIIANA (SOSPA) YA MWAKA 1998.

UTANGULIZI

Mtandao wa wanaharakati wanaoshiriki semina za kila Jumatano za jinsia na maendeleo, ukombozi wa wanawake na haki za binadamu (GDSS) tunalaani vikali tamko la Mh. Mathias Chikawe Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba alilolitoa kwenye gazeti la Rai tarehe 8-14/1/2009 kutaka adhabu ya makosa ya kujamiiana ipunguzwe.

Mh. Waziri ameonyesha udhaifu wa kutafsiri sheria hiyo, kwa kutoa tamko bila kufanya utafiti wa kina kwa wahanga walioathiriwa na vitendo vya ubakaji mfano wanawake, watoto, vikongwe, watu wenye ulemavu nk.

Ikiwa ni miaka kumi (10) sasa tangu kupitishwa kwa sheria hii, Waziri anaposema sheria hii ni mbaya anaonyesha wazi kutotambua mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chote hicho kwa jamii kuvunja ukimya na kuripoti matukio mengi ya ubakaji na watuhumiwa kuchukuliwa hatua, hata kiasi yeye mwenyewe kukiri kuwa wafungwa wa ubakaji ni wengi magerezani.

MADAI YA WANAHARAKATI
Kutokana na hayo tuliyoyaeleza hapo juu sisi wanaharakati tunadai yafuatayo:-

1. Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba iitishe mjadala wa Kitaifa kwa wadau wote ili kufanya upya mapitio ya sheria hii ili kuangalia mapungufu na mafanikio ya sheria hii, kabla ya kupelekwa Bungeni kama Waziri alivyoahidi.

2. Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto atoe tamko rasmi akielezea mafanikio ya sheria ya makosa ya kujamiiana tangu kuanzishwa hadi sasa.

3. Tumesikitishwa na matamshi ya Mhe. Waziri kwamba Bunge lilishinikizwa na wanaharakati kupitisha sheria hii ya makosa ya kujamiiana. Hivi waziri anammanisha nini hapa? Je? linafanya kazi kwa shinikizo la watu bila kufuata sheria na taratibu? Kwa hili tunamtaka Waziri aliombe radhi Bunge letu tukufu.

4. Sheri ya ndoa ya mwaka 1971 na sheria ya makosa ya jinai (Penal code) zifanyiwe marekebisho haraka ili zisikinzane na sheria ya makosa ya kujamiina ya mwaka 1998 na sheria ya elimu 1978.

5. Sheria ya makosa ya kujamiiana (SOSPA) itambue ubakaji ndani ya ndoa.

6. Kutokana na msongamano mkubwa wa kesi za makosa ya jinai katika mahakama zetu, tunaitaka serikali ianzishe mahakama maalum itakayoshughulikia kesi zote zinazohusiana na ukatili wa jinsia.

Sisi kama wanaharakati tunaamini kuwa kutiliwa mkazo kwa sheria ya SOSPA kutasaidia sana kupunguza matatizo mengi ya unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo kuwaepusha mabinti wanaotiwa mimba wakiwa shuleni jambo ambalo ni kilio kikubwa kwa Taifa letu.

Mwisho tunashauri viongozi wetu wawe makini pale wanapotoa matamko mbalimbali.

Imetolewa na Mtandao wa wanaharakati wanaoshiriki semina za kila Jumatano za jinsia na maendeleo, ukombozi wa wanawake na haki za binadamu (GDSS) na kusainiwa na

1.Kigogo Youth and Women Development Programme (KYWDP)
2.African Life Foundation
3.Youth Action Volunteers (YAV)
4.Mabibo Youth Center
5.Twitange Development
6.SHDEPHA + Mbagala
7.Afya kuu (KURASINI)

Wednesday, February 11, 2009

Msamaha wa madeni wanunulia ‘mashangingi’

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema imetumia fedha za msamaha wa madeni na kuamua kununua magari ya kifahari 80 kwa ajili ya viongozi. Akitoa ufafanuzi leo kuhusu ununuzi wa magari hayo ya kifahari ambao umelalamikiwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, alisema fedha hizo hazitokani na kodi ya wananchi.

"Tumenunua magari ya 'mashangingi' aina ya Toyota Prado, jumla yake 80 kutokana na msamaha wa madeni kutoka taasisi za fedha za kimataifa ... hapo tuliamua ni bora kuagiza magari kwa ajili ya matumizi ya viongozi," alisema Hamza. Alisema magari hayo mara baada ya kuwasili nchini yaligawiwa kwa viongozi wa ngazi za juu wakiwamo mawaziri, naibu mawaziri na wakuu wa mikoa Unguja na Pemba.

Hamza alisema si busara kwa mawaziri na watendaji wakuu wa serikali kusumbuka kutokana na tatizo la usafiri ambalo lilikuwa kubwa. Aidha, alisema mbali ya kununua magari hayo, SMZ ilitumia fedha hizo kununua matrekta 12 kwa ajili ya kazi za kilimo Unguja na Pemba.

"Hatukununua mashangingi tu, pia tulinunua matrekta 12 kwa ajili ya kuimarisha sekta ya kilimo kwa wakulima wetu katika kuondokana na ukosefu wa chakula," alisema. Hamza alilazimika kutoa ufafanuzi huo kutokana na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanasiasa na wananchi kuhusu serikali kununua magari ya kifahari yenye kugharimu fedha nyingi, huku wananchi wakikabiliwa na matatizo mengi.

Daily News; Tuesday,February 10, 2009 @20:28

Monday, February 9, 2009

KASHFA YA RADA: Chenge na Dr. Rashid wanasubiri nini?Wanaharakati,

Siku chache zilizopita makachero wa Uingereza wa kuchunguza makosa mazito SFO walitoa ripoti yao kwa mwanasheria mkuu wa serikali ya Tanzania kuelezea matokeo ya uchunguzi wao waliofanya ambao wamebaini kuwa aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali wakati huo Mheshimiwa Andrew Chenge(MB) na Dr. Idris Rashid (Gavana wa zamani wa Benki kuu ya Tanzania) ambaye sasa ni Mkurugenzi mkuu wa shirika la umeme nchini TANESCO walihusika moja kwa moja na sakata zima la ununuzi wa RADA na wanatuhumiwa kwa ulaji mkubwa wa rushwa.

Vigogo hawa wanasubiri nini?

Friday, February 6, 2009

Waziri Masha atajiuzulu?


WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Lawrance Masha, anaweza kulazimika kuchukua uamuzi wa kujiuzulu au kulazimishwa kujiuzulu, kama Bunge litaridhika kuwa ameingilia mchakato wa zabuni ya kumpata mchapishaji wa Vitambulisho vya Taifa.

Taarifa za hivi karibuni zaidi kuhusu suala hilo la Vitambulisho vya Taifa, zinasema ya kuwa Waziri Masha yupo katika mtanziko wa ama kujiuzulu kabla ya kushambuliwa kwa hoja kali za wabunge au kusubiri mashambulizi hayo ndani ya ukumbi wa Bunge.

Taarifa zinasema kwamba juzi Jumatano, Waziri Masha aliitwa mbele ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ya Bunge, inayoongozwa na Mbunge wa Muleba Kusini, Wilson Masilingi, iliyokusudia kumhoji kwa kina kuhusu tuhuma za uingiliaji anaodaiwa kuufanya na kama Kamati hiyo itaridhika kuwa ameingilia mchakato huo, basi Kamati italazimika kuwasilisha suala hilo katika Kamati ya Uongozi ya Bunge, ambayo itapanga muda wa kulijadili.

Mfumo huo wa mahojiano unaomnyemelea Masha ni mithili ya ule uliotumika wakati wa uchunguzi wa kibunge wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond.

Kwa upande wake, Masha alipohojiwa na Gazeti la Raia Mwema alithibitisha kuitwa na kamati hiyo ya Masilingi akisema amepewa taarifa ya kuitwa na atakwenda na kwamba asingeweza kuingia katika undani wa jambo hilo linalohusisha uvujaji wa nyaraka za siri.

Wiki iliyopita, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akizungumza bungeni kujibu maswali kuhusiana na Vitambulisho aliweka bayana kuwa kuna tatizo katika Wizara ya Mambo ya Ndani kwamba kuna nyaraka zimenyofolewa katika moja ya mafaili wizarani hapo.

Hata hivyo, alisema kunyofolewa kwa nyaraka hiyo si suala la msingi bali kwamba tatizo la msingi ni kuingiliwa kwa mchakato huo.

Pinda alimweleza Dk. Wilbroad Slaa, aliyekuwa amehoji mchakato wa Vitambulisho katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kuwa alikuwa amewahi mno kuuliza suala hilo kwa kuwa mchakato wa zabuni bado haujafika mwisho.

Akashauri kuwa ni vema mchakato ukafika mwisho na hapo ndipo Waziri Masha anaweza kubanwa vizuri kwamba ameingilia mchakato huo au la.

Hata hivyo, kuna uwezakano mkubwa kwa suala hilo kujadiliwa ndani ya Bunge kutokana na madai ya kuwapo kwa vielelezo thabiti vinavyomuhusisha Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, ambaye anadaiwa kulalamikiwa na Waziri Masha kwamba amefanya uamuzi bila kumtaarifu yeye kama waziri wa wizara husika.

Waziri Masha anadaiwa kuandika barua kwa Waziri Mkuu Pinda akimlalamikia Luhanjo kuwa amefanya uamuzi kwa kumpa maagizo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, bila ya yeye kutaarifiwa.

Baadhi ya wazoefu wa masuala ya Bunge wanaeleza kuwa huenda suala hili likafikia hatua ya kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge ambayo ina madaraka ya kuhoji watu katika mfumo wa kimahakama.

Katika utaratibu wa kawaida, anayeitwa kuhojiwa na Kamati Teule ya Bunge hulazimika kula kiapo na akibainika kudanganya anaweza kushitakiwa.

Sakata La Rada: Chenge Ametajwa, Hatushituki!


ZIMETUFIKIA habari za Makachero wa Uingereza kitengo cha Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) kubaini maovu zaidi ya kifisadi anayotuhumiwa kuyafanya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Miundo Mbinu Andrew Chenge.
Kwamba Chenge ameongopa chini ya kiapo juu ya fedha, dola za Kimarekani miloni moja na nusu alizoweka kwenye akaunti yake kisiwani New Jersey. Soma zaidi;

http://www.raiamwema.co.tz

Thursday, February 5, 2009

Ulevi wa Pombe Unavyodumaza Maendeleo; Hasa Maisha ya Wanawake.

Mada iliwakilishwa jumatano ya tarehe 4/2/08 na kaka Gunnar Lundstrom na Mathias Kimiro kutoka shirika la IOGT la Sweden, na kuwezeshwa na dada Fedelis Chale. Lengo la Mada hii ilikuwa ni; kujadili unywaji wa pombe katika ngazi ya mtu binafsi, familia na jamii unavyoweza kuleta madhara kwa jamii hasa wanawake na kutafuta ufumbuzi wa kupunguza tatizo hilo.

Washiriki walieleza madhara ya utumiaji wa pombe kupita kiasi katika ngazi ya mtu binafsi, familia, na jamii. Katika ngazi ya mtu binafsi ni pamoja na: magonjwa ya ini, macho, kifua kikuu, upungufu wa nguvu za kiume/kike, umasikini, na kushindwa kufikiri sawasawa.
Katika ngazi ya familia madhara ni pamoja na; mlevi kushindwa kutunza familia na kumuachia mama mzigo wote, watoto kukosa malezi ya baba na kusababisha mmonyoko wa maadili, Umasikini, na ubakaji ndani ya ndoa. Katika ngazi ya kijamii walevi wamshindwa kuchangia ujuzi wao katika kuleta maendeleo kwa sababu muda mwingi wanakuwa wamelewa ama wagonjwa kutokana na ulevi kupindukia. Pia ulevi ni chanzo cha ubakaji wa wanawake. Taifa pia limekuwa likipata hasara kwa; kuwatibia wananchi wanaodhurika na pombe, na njaa za mara kwa mara zinazotokana na utumiaji mbaya wa nafaka kwa ajili ya utengenezaji wa pombe.

Washiriki walipendekeza hatua zifuatazo katika kupunguza ulevi katika jamii; Elimu ya madhara ya pombe iwekwe katika mitaala ya shule za msingi, Elimu ya Kujitambua itolewe kwa jamii kupitia vipindi vya runinga na redio, serikali ishinikizwe kusimamia vizuri sheria za uuzaji wa pombe, wanaharakati watoe taarifa kwa vyombo husika wanapoona kuna ukiukwaji wa sheria za uuzaji wa pombe katika maeneo yao, na wananchi kuwaelimisha watoto wao juu ya madhara ya utumiaji wa pombe.


Je, wanaharakati wamefanya nini kuhakikisha utumiaji wa pombe kupita kiasi hauendelei kuleta madhara kwa wanawake?

Wednesday, February 4, 2009

Familia Jasiri


Ishukuriwe serikali imeanza kuchukua hatua madhubuti kudhibiti ukatili dhidi ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi, vinginevyo familia kama hii isingekuwa na ujasiri wa kushiriki kwenye shughuli za kijamii kama walivyofanya hawa wakati wa kuandamana kupinga ukatili huo hivi karibuni.

Wanaharakati tuendeleze vita dhidi ya ndugu zetu hawa.

Tuesday, February 3, 2009

Pinda yuko sahihi lakini...WIKI iliyopita Waziri Mkuu Mizengo Pinda alifanya ziara mahususi katika mikoa ya Kagera, Mwanza, Shinyanga na Tabora akiwa na ajenda moja kuu: mapambano dhidi ya mauaji yanayoshamiri nchini ya walemavu wa ngozi (Albino).

Sitaki kurejea yale yote yaliyojiri kwenye ziara hiyo ila jambo moja kubwa ambalo limezua mjadala katika jamii. Hili ni kauli yake ya ‘jino kwa jino’ kwa maana kwamba wauaji wa walemavu wa ngozi pindi wanapokamatwa ‘red handed’ basi hakuna haja ya kuwapeleka polisi (ila nao wauwawe).

Hii ni kauli nzito kutolewa na kiongozi mzito wakati huu ambao nchi iko katika hekaheka ya kujaribu kukomesha mauaji ya hawa ndugu zetu ambao kwa miaka mingi tumeishi nao bila matatizo.

Nianze kwa kukiri kabisa kwamba kwa mtu yeyote ambaye ni muumini wa utawala bora kwa maana ya utawala unaoheshimu na kuzingatia sheria, kuua ni ukiukwaji mkubwa wa haki ya msingi ya binadamu ambayo ni kuishi. Hii hahitaji kuwa mwanasheria ili kuwa mtetezi wa haki za binadamu na utawala bora.

Lakini kuna jambo moja la msingi ambalo mpaka sasa linatatiza sana kuhusu hizi haki za binadamu na watu wanaozitetea kwa nguvu zao zote. Kwamba kuua mtu hakuna tatizo ila kuua mtu aliyeua ni kosa kubwa!

Hapo ndipo ninapoungana na Waziri Mkuu Pinda. Kwamba iweje mtu mmoja awe na haki ya kuua lakini abaki na haki yake ya kuishi? Hivi huyu aliyeuawa hakuwa na haki ya kuishi? Na kama anayo kwa nini asitetewe basi? Na kama amenyimwa haki yake ya kuishi kwa nini huyu aliyemnyima naye asipokonywe (auawe) haki yake kama alivyomfanyia mwenzake?

Mnaliangaliaje suala hili wanaharakati wenzangu?