GENGE la watu wasiofahamika, wanatuhumiwa kumbaka na kumsababishia kifo mwanafunzi wa kike wa kidato cha nne mwenye umri wa miaka 21, aliyekuwa akisumbuliwa pia na ugonjwa wa moyo.
Mwanafunzi huyo alikuwa akisoma katika sekondari ya Msakila mjini Sumbawanga na moyo wake baada ya kupimwa kitabibu ulibainika kuwa mkubwa kuliko kawaida.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk. Saduni Kabuma, alisema jana kuwa mwanafunzi huyo alifariki dunia usiku wa kuamkia jana, muda mfupi baada ya kufikishwa katika hospitali ya mkoa mjini hapa kwa matibabu.
Alikizungumza jana kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi, Dk. Kabuma alisema alibainika amejeruhiwa vibaya sehemu za siri na pamoja na majeraha hayo pia kiafya alikuwa dhaifu.
"Alipokewa akiwa mzima ila alikuwa amejeruhiwa sehemu za siri na hali yake ilibadilika ghafla na kufariki dunia muda mfupi hali iliyotufanya tufikie uamuzi wa kuchunguza mwili wake zaidi ndipo tukabaini kuwa alikuwa na moyo mkubwa kupita kiasi … kubakwa kwake kuliharakisha kifo chake," alisema Dk. Kabuma
Alisema rekodi ya afya yake hospitalini hapo imeonesha kuwa alikuwa akisumbuliwa mara kwa mara na ugonjwa wa moyo na pumu.
Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Isuto Mantage, alisema mwanafunzi huyo alifikwa na mauti Jumamosi saa mbili usiku katika kitongoji cha Hali ya Hewa, eneo la Chanji mjini hapa.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Mantage, alisema, usiku huo wa tukio marehemu aliaga nyumbani kuwa alikuwa anakwenda kununua vocha, ili aongeze salio kwenye simu yake ya mkononi.
"Sasa wakati akiwa anarejea nyumbani tena akiwa peke yake, alivamiwa na genge la watu wasiofahamika ambao walimbaka kwa zamu wakamjeruhi sehemu za siri kwa kitu chenye ncha kali na kumsababishia maumivu makali.
Wasamaria wema walipomkuta walimkimbiza hospitali ya mkoa, lakini alifariki dunia wakati anapatiwa matibabu," alisema Kamanda.
Kwa mujibu wa Kamanda wabakaji hao walikimbilia kusikojulikana na Polisi inaendelea kuwatafuta ili iwakamate na sheria iweze kuchukua mkondo wake.
No comments:
Post a Comment