Monday, June 1, 2009

Dola yaanza kumwandama Mengi


-Aitwa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama
-Yeye ataka mahakama iachiwe ifanye kazi yake
-Sheria ya kudhibiti umiliki vyombo vingi vya habari yaja
KAULI na vitendo vya Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Limited, Reginald Mengi, zinazowagusa watu aliowaita mafisadi papa, vimemuingiza katika matata makubwa, na sasa ameanza kubanwa na vyombo vya dola, Raia Mwema imeambiwa.

Habari za uhakika kutoka serikalini zimethibitisha kwamba mara baada ya Mengi kutoa kauli iliyowataja wafanyabiashara wenzake watano kuwa ndio mafisadi papa, kumekuwa na matukio mazito ya mfululizo yanayolenga kumbana, la karibuni zaidi likiwa ni la mfanyabiashara huyo kuitwa na Kamati Ndogo ya Ulinzi na Usalama wa Taifa.

Ofisa Mwandamizi wa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, aliithibitishia Raia Mwema wiki hii kwamba mara kadhaa wamekuwa wakimtaka Mengi kutoa ushirikiano na wamemfuata hadi nyumbani kwake, wilayani Kinondoni na kumuandikia barua mara mbili lakini yeye amekuwa akisita.

“Ni kweli wakubwa walimtaka atoe ushirikiano bila mafanikio, mara ya kwanza Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) ilimwandikia barua kutaka apeleke ushahidi wa tuhuma alizozitoa, akagoma akieleza kwamba ushahidi huo atautumia mahakamani ambako kuna kesi mbili kuhusiana na tuhuma hizo na mara ya pili sasa Kamati Ndogo ya Ulinzi na Usalama wa Taifa ikamtaka aende kutoa ushirikiano,” alisema Ofisa huyo.

Ofisa huyo wa Polisi ameliambia Raia Mwema kwamba kamati hiyo inayoongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi (DDCI), Peter Kivuyo, ni kamati ya watendaji ambayo kwa sasa inahusisha vyombo vyote vya dola isipokuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ambao walijitoa.

“Unajua haya mambo yana utata sana, maana hiyo kamati ya kina Kivuyo inahusika zaidi na kupambana na ujambazi na dawa za kulevya na ndiyo maana TAKUKURU walijitoa, sasa kama huyo mzee (Mengi) alizungumzia ufisadi, wanapaswa kuwaachia akina Hosea (Dk. Edward, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU) wafanye kazi yao,” alisema.

Habari kutoka TAKUKURU zimethibitisha kwamba tayari chombo hicho kimekuwa kikifanyia kazi kile kilichopewa jina la “malumbano kati ya Mengi na Rostam” na kwamba wamekwishakupata ushirikiano kutoka pande zote zinazohusika.

Mengi mwenyewe alipotafutwa na Raia Mwema wiki hii alieleza kwamba hawezi kuzungumza lolote kwa kuwa yeye tayari amefungua kesi mahakamani na angependa mambo yaende kwa mujibu wa sheria si katika vyombo vya habari.

Soma zaidi

No comments: