Friday, June 12, 2009

Bajeti 2009/2010


Waziri wa fedha na mipango Mh. Mustafa Mkullo akiingia bungeni jana na mkoba wake tayari kusoma bajeti ya mwaka 2009/2010. Bajeti hiyo itaanza kujadiliwa jumatatu.

Serikali imewasilisha bungeni mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2009/2010. Katika bajeti hiyo ya serikali iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, bungeni mjini hapa jana, maeneo mbalimbali yamefanyiwa marekebisho huku wigo wa kodi ukitanuliwa. Katika mwaka wa fedha wa 2009/2010, matumizi ya serikali yatakuwa Sh trilioni 9.5, matumizi ya kawaida yakiwa Sh trilioni 6.7 na matumizi ya maendeleo ni Sh trilioni 2.8.

Kwa mujibu wa bajeti hiyo, katika matumizi ya maendeleo, kiasi cha Sh trilioni 1.9 zitatokana na fedha za wahisani kupitia miradi pamoja na mifuko ya kisekta na kiasi kilichobaki cha Sh milioni 968,028 zitatokana na mikopo ya ndani na sehemu ya mchango wa wahisani kupitia misaada ya kibajeti.

Kama ilivyotarajiwa bajeti hiyo ya serikali ya mwaka ujao wa fedha, ina mabadiliko makubwa yenye lengo la kutaka kukabiliana na msukosuko wa fedha ulioziathiri nchi nyingi duniani. Bajeti hiyo imezigusa sekta mbalimbali ambapo zipo zilizofutiwa kodi, kupandishiwa au ushuru kurekebishwa.

Katika hatua hiyo, serikali imeamua kupunguza kiwango cha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutoka asilimia 20 ya mauzo hadi asilimia 18 ili kupunguza makali ya athari za mdororo wa uchumi. Bidhaa zilizopandishiwa ushuru Waziri Mkulo alisema serikali imeamua kurekebisha kwa asilimia 7.5 viwango maalumu kwenye bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa isipokuwa zile za mafuta ya petroli.

Alisema marekebisho hayo yamezingatia kiasi cha wastani wa mfumuko wa bei. Viwango vya sasa na vile vinavyopendekezwa ni pamoja na vinywaji baridi ambavyo ushuru unapanda kutoka Sh 54 hadi Sh 58 kwa lita. Ushuru wa bia inayotengenezwa na nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa, umepanda kutoka Sh 194 hadi Sh 209 kwa lita, huku bia nyingine zote ushuru wake ukipanda kutoka Sh 329 hadi Sh 354 kwa lita.

Mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi, kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, ushuru umepanda kutoka Sh 1,053 hadi Sh 1,132 kwa lita na vinywaji vikali umepanda kutoka Sh 1,561 hadi Sh 1,678 kwa lita.

Serikali pia imerekebisha viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye sigara ambapo sigara zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kutokana nba tumbaku inayozalishwa hapa nchini umerekebishwa kwa kiwango cha asilimia 75 kutoka Sh 5,348 hadi Sh 5,749 kwa sigara 1,000. Sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini, umerekebishwa kwa asilimia 75 pia kutoka Sh 12,618 hadi Sh 13,564 kwa sigara 1,000.

Sigara nyingine zenye sifa tofauti na hizo, ushuru wake umerekebishwa kutoka Sh 22,915 hadi kufikia Sh 24,633 kwa sigara 1,000, wakati tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara ushuru umerekebishwa kutoka Sh 11,573 hadi Sh 12,441 kwa kilo na ushuru wa Cigar unabaki kuwa asilimia 30.

Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) Kwa upande wa sheria za Kodi ya Ongezeko la Thamani, Mkulo alisema imependekezwa kufanya marekebisho katika sheria ya kodi ya VAT kwa kusamehe VAT kwenye matangi maalumu ya kuhifadhia maziwa na vipipa vya aluminium vya kukusanyia maziwa ili kuhamasisha matumizi yake.

Pia kusamehe kodi ya VAT kwenye huduma za kilimo za kutayarisha mashamba, kulima, kupanda na kuvuna ili kupunguza gharama za uzalishaji kwenye kilimo na kupanua wigo wa msamaha maalumu wa kodi ya VAT kwenye maduka yasiyotoza kodi ya JWTZ. Serikali pia imepunguza wigo wa msamaha maalum wa kodi ya VAT kwa asasi na Mamlaka za maji safi na maji taka nchini ili msamaha huo uhusishe vifaa na huduma zitakazohusika katika ujenzi wa miundombinu ya maji safi na taka pekee.

Imeondoa msamaha wa VAT kwenye huduma za kukodi ndege, kwani huduma hizo hutolewa kibiashara kama huduma za kukodi vyombo vingine vya usafiri na kuondoa msamaha wa VAT kwenye chai na kahawa iliyozalishwa na kusindikwa nchini ili kuleta usawa na mazao mengine yanayosindikwa nchini.

Alisema pia serikali imeamua kutoza kodi ya VAT kwenye muda wa maongezi kwenye simu kwa kutumia bei halisi inayoonyeshwa kwenye vocha badala ya bei nafuu anayotozwa muuzaji wa jumla. Imepunguza pia wigo wa msamaha maalumu wa Kodi ya VAT kwa kampuni za madini, mafuta ya petroli na gesi ili msamaha huo uhusishe shughuli na utafutaji pekee ambao hufanywa na mwekezaji kabla ya kuanza uzalishaji.

Imeondoa msamaha maalumu wa VAT kwa asasi zisizo za kiserikali (NGOs) na kwa mashirika ya dini na kwamba hatua hiyo itahusisha madhehebu yote ya dini ambayo ni Waislamu, Wakristo, Wahindu, Mabohora na mengine na kuwa vifaa vya kiroho na ibada vitaendelea kupata msamaha wa kodi.

Soma zaidi

2 comments:

Anonymous said...

hakuna jipya, isipokuwa amesogeza tena ulaji mpya usio na udhibiti. haya acha tuwaangalie mwisho wao!

Anonymous said...

hakuna jipya sana, watuambie fedha zilizoibiwa zitarudi lini Hazina?