Tamko kwa vyombo vya habari
1. Sisi wanaharakati wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na washiriki wa Semina ya Jinsia na Maendeleo (GDSS) ya tarehe 27 Mei 2009 tunaipongeza serikali kwa juhudi za kuboresha maisha ya Watanzania wote na kufikia malengo ya maendeleo na demokrasia kama mwongozo wa bajeti ulivyo. Mjadala wa bajeti ni muhimu katika kutathmini ni yupi anayefaidika na mfumo uliopo wa uchumi, ni nani anayenyonywa? nini kifanyike kuleta mabadiliko? na kwa vipi?
Katika taarifa hii fupi kwa vyombo vya habari kabla ya kikao cha bajeti cha bunge kuanza tarehe Juni 8, tunapenda kudondoa baadhi ya masuala muhimu ambayo tunapendekeza/ serikali kuyapa kipaumbele zaidi katika bajeti ijayo ya 2009/10.
2. Vipaumbele vya msingi kutoka kwa wanaharakati vinazingatia muktadha wa kuyumba kwa uchumi wa dunia, umuhimu wa serikali kujizatiti katika kulinda wananchi wa kawaida ambao tayari hali yao ya maisha ilikuwa mbaya na mapendekezo ya bajeti tunayoitaka. Hivi ni pamoja na:
o MFUMO MKUU WA UCHUMI – Mwaka huu ni mwaka wa mwisho wa sera kuu ya MKUKUTA uliojikita katika sera za urekebishaji wa uchumi, ulegezaji na ubinafsishaji ambazo zimewezesha zaidi sekta za utalii, madini na kilimo cha maua na mboga mboga. Kutokana na ripoti za serikali kila mwaka na Muongozo wa Bajeti wa mwaka huu, haujaweza kupunguza umaskini na imeongeza tofauti kati ya walio nacho na wasio nacho, wanawake na wanaume, watu wa vijijini na mijini. Kwa hiyo tunadai mfumo mbadala wa uchumi ambao utanufaisha wananchi wote na kuwepo sauti na uwezo zaidi wa wananchi katika maamuzi kuhusu maliasili zetu kama vile madini, ardhi , maji, misitu na nyinginezo. Pia tuendeleze viwanda vyetu kwa kutumia malighafi ya hapa nchini, kuzalisha bidhaa nzuri kwa ajili ya soko la ndani kwanza na nje.
o KAZI NA AJIRA - Tunadai kuongeza rasilimali na kuboreshwa kwa sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi zaidi, kuwepo kwa zana/ pembejeo bora na za kisasa, masoko ya kuuza mazao yanayopatikana na pia mazingira mazuri ya kuweza kupata bidhaa bora, kwa kuzingatia hasa mahitaji ya wazalishaji wadogo wadogo hasa wanawake.
o Mfumo mzima wa ajira uboreshwe kuwepo fursa sawa kwa wote bila ubaguzi wa kijinsia wala tabaka na mikopo yenye masharti nafuu pamoja na kuwafikia walengwa kwa wakati, Sera ya ajira itekelezwe kwa kipindi maalum ili maisha bora yaendane na hali halisi ya maisha kwa watanzania wote, kubainisha viwango vya mishahara kwa watumishi ngazi za juu serikalini pamoja na wabunge na sekta binafsi na pia kupandisha kima cha chini cha mishahara, kurasimisha na kutathmini mchango wa pato la kazi anazofanya mama wa nyumbani bila kulipwa ujira wowote.
o MFUMO WA KODI - Tunadai, msamaha wa kodi kwa wawekezaji upitiwe upya na ufutwe kabisa na uthibiti wa ulipaji kodi uimarishwe zaidi ili mabepari na makampuni makubwa yaweze kulipa kodi kwa utaratibu uliowekwa. Kubadili kabisa mifumo ya ukusanyaji kodi kwa kuzingatia uwazi zaidi kwa kodi zinazotozwa makampuni makubwa hasa katika sekta binafsi.
o MIUNDO MBINU - Tunadai huduma za barabara zetu ziboreshwe na zinufaishe makundi yote mijini na vijijini, ufisadi mkubwa unaoendelea katika utoaji wa tenda za ujenzi wa barabara ukomeshwe mara moja. Kuwepo na usawa katika ugawaji wa huduma ya umeme katika maeneo yote nchini bila kuwepo upendeleo wa kitabaka. Kuimarisha mifumo yote ya maji safi na taka ili kupunguza magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu, pia suala zima la uzoaji takataka limekuwa tatizo sugu mitaani hivyo lipatiwe ufumbuzi wa haraka.
o AFYA - Tunadai bajeti ya afya iongezwe hasa kwa afya ya uzazi, itengwe kipekee ili kupunguza vifo vya mama na mtoto, vifaa vya kujifungulia vipatikane bure mahospitalini, ufuatiliaji wa karibu wa upatikanaji na matumizi ya vifaa hivyo uwe wazi, kuimarisha upatikanaji wa huduma za dharura za uzazi na kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya usafiri na kuboresha mfumo wa rufaa kwa wagonjwa na watu wa kaliba zote, masikini na matajiri, mijini na vijijini. Wauguzi waongezwe kwa uwiano wa wagonjwa wanaohitaji huduma hizo, lakini pia masilahi yaongezwe na kuboresha huduma stahili hasa vijijini na mijini.
o MAJI- Tunadai miundo mbinu ya maji iboreshwe mijini na vijijini kwa kuondoa miundo mbinu chakavu na ya kizamani na kuweka mipya, pia itandazwe nchi nzima, tunataka maji yasibinafsishwe. Kwa hiyo muswada wa maji uliopitishwa kwa haraka na bunge hivi karibuni urekebishwe. Maji yasionekane kama bidhaa ni haki kwa wote, kuwepo na bajeti ya kutosha ya kuwapatia wananchi maji safi na salama na ya kutosha, ili kutunisha bajeti ya serikali wafanya biashara wakubwa wenye viwanda, mashamba makubwa na migodi wawajibike kulipia maji
o ELIMU - Tunadai mitaala ya elimu iendane na mazingira yaliyopo na upatikanaji wa elimu ya msingi hadi kidato cha nne uwe bure kwa wote na rasilimali ziongezwe na idadi ya waalimu wenye mafunzo, kuzingatia mishahara, vifaa mashuleni, nyumba za walimu, mabweni ya wanafunzi hasa wasichana na makundi yote maalumu kama vile walemavu na sera ya mifumo miwili ya elimu ya serikali na ya binafsi irekebishwe ili kusiwe na ujenzi wa ‘dunia’ mbili ya walio nacho na wasio nacho.
o UKIMWI - Tunadai rasilimali zaidi katika kutatua tatizo la upatikanaji wa madawa ya kuongeza nguvu (ARVs), kipaumbele kinahitajika zaidi katika kuhakikisha madawa yanapatikana bure kwa magonjwa yote nyemelezi, upimaji bure wa damu na kutoa chakula bure kwa watumiaji wa madawa ya ARVs, na huduma zaidi kwa utunzaji wa wagonjwa wa ukimwi majumbani kazi ambayo mara nyingi inafanywa na wanawake na watoto. Bajeti zaidi ielekezwe katika utoaji wa kinga ili kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi ikiwa pamoja na mikakati bayana kuwezesha wanawake na wasichana kufanya maamuzi kuhusu ngono pamoja na makundi yaliyopo pembezoni k.m. wanaofanya biashara ya ngono; kuboreshwe kwa mfumo wa utoaji na upatikanaji wa taarifa sahihi, elimu kwa wakati muafaka ili kuchangia suala zima la uwajibikaji na uwazi.
o SHERIA NA MAHAKAMA - Tunadai rasilimali zaidi katika kuharakisha kesi hasa mahakama ya mwanzo na mahakama zote . Rushwa, mishahara duni, matumizi ya lugha chafu, viangaliwe kwa kina zaidi. Serikali inatakiwa kutoa rasilimali zaidi na kufuatilia utekelezaji wa mikakati ya kutokomeza ukatili wa kijinsia katika nyanja zote, wakishirikiana na mashirika na taasisi za kiraia na jamii wote wahusishwe katika kufanya mabadiliko kwenye mfumo mzima wa haki na usalama ikiwemo sheria, mahakama, polisi, jeshi la wananchi huku yakichagizwa na utoaji wa mafunzo ya jinsia, uongeza vituo vya kutoa ushauri nasaha, matunzo ya watoto, na kutoa hifadhi mbadala ya makazi kwa waathirika wa unyanyaswaji wakiwemo wanawake na watoto. Jamii yote wachukizwe na vitendo viovu vya unyanyasaji wa kijinsia manyumbani na katika sehemu za umma na wachukue hatua mara moja.
o SIASA NA UONGOZI – Tunadai mikakati madhubuti ya serikali katika kufanikisha uwiano sawa wa kijinsia asilimia 50 -50 kati ya wanawake na wanaume katika mchakato mzima wa uchaguzi unaofanyika katika ngazi za serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani. Wanawake wawe na maamuzi na sauti sawa katika sera, mipango na bajeti katika nyanja zote kuanzia serikali za mitaa, wabunge, serikalini, mawaziri na katika sekta binafsi na jamii huria.
o UWAJIBIKAJI, UWAZI NA USHIRIKI WA WANANCHI. Tunadai kutumika kwa taratibu zilizopitishwa na kukubalika ili kuongeza uwazi, na uwajibikaji kwa kutumia rasilimali zilizopo, na hatua madhubuti zichukuliwe dhidi ya matumizi mabaya ya fedha na ‘ufisadi’. Tunadai nafasi zaidi na kuweka mfumo bayana wa kuwezesha asasi za kiraia na wananchi wote kushiriki katika mchakato wa utengenezaji wa bajeti na ufuatiliaji na tathmini ya matokeo ya bajeti, ili kuwezesha mjadala wa kitaifa kuhusu ukusanyaji na utumiaji wa rasilimali ya umma na taifa katika kuhakikisha maisha bora ya wananchi wote.
……………………….
Usu Mallya,
Mkurugenzi Mtendaji.
01/06/09
1 comment:
vipi waandaaji haya madai na matakwa yamefanyiwa kazi na serikali? ama ni kelele za bure?
Post a Comment