Monday, June 22, 2009

'Kilimo Kwanza' iwe Kilimo Kwanza kweli kweli

WIKI iliyopita Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, akiwasilisha bungeni taarifa ya hali ya uchumi na malengo kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2009/2010, alitangaza kuanzishwa kwa kaulimbiu mpya ya Kilimo Kwanza.

Katika kile kinachoonekana kuwa Serikali yetu, hatimaye, sasa imekikumbuka kilimo, Waziri Mkulo pia aitangaza nguzo kuu 10 zitakazotuwezesha kufikia mapinduzi ya kilimo nchini.

Alizitaja nguzo hizo kuwa ni Dira ya Kilimo Kwanza, Ugharimiaji wa Kilimo Kwanza, Mabadiliko ya Mkakati wa Kushughulikia Kilimo, Kuhuisha Muundo wa Asasi za Kilimo, Ardhi, Vivutio vya Kilimo, Sayansi na Teknolojia, Mageuzi ya Viwanda vya Kilimo, Raslimali Watu, Miundombinu na Uhamasishaji Watanzania juu ya dhana ya Kilimo Kwanza.

Tunapenda kuipongeza Serikali yetu kwa kukikumbuka kilimo na kwa kuibuka na kaulimbiu hiyo ya Kilimo Kwanza.

Lakini pamoja na pongezi hizo, tunatahadharisha kwamba kaulimbiu ya Kilimo Kwanza itabakia tu ni kaulimbiu; kama haitaandamana na matendo ya dhahiri katika kuzishughulikia hizo nguzo 10 zinazolenga kutuletea mapinduzi hayo ya kilimo nchini.

Tunatoa tahadhari hiyo tukikumbuka kwamba ukosefu wa kaulimbiu halijapata kuwa tatizo katika sekta ya kilimo nchini. Tumewahi kuwanazo nyingi tu; kama vile “Siasa ni Kilimo”, “Kilimo cha Kufa na Kupona”; lakini zote hazikutuwezesha kuyafikia Mapinduzi ya Kilimo tunayoyataka.

Kinachokosekana nchini si kaulimbiu za kilimo bali vitendo; yaani uchapaji kazi wa kweli kweli katika kutekeleza mipango ya kunyanyua kilimo hicho, na pia utoaji wa pesa za kutosha kutekeleza mipango hiyo.

Kwa hiyo tunataraji kwamba “Kilimo Kwanza” si ahadi tu ya makaratasi kama zilivyopata kuishia ahadi nyingine walizopewa wakulima wetu.

Na mfano mzuri ni CCM yenyewe. Katika ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2005, wakulima waliahidiwa kwamba Serikali ya CCM itasambaza kilimo cha matrekta katika wilaya zote nchini. Leo hii, miaka minne baadaye, kilimo cha matrekta hakijasambazwa hata katika wilaya 15 tu nchini!

Kwa hiyo wakati tunaipongeza Serikali yetu kwa kuikumbuka sekta ya kilimo, inayohusisha asilimia 75 ya Watanzania, tunaitahadhirisha kuhusu utendaji. Tunataka Kilimo Kwanza iwe Kilimo Kwanza kweli kweli, na si ahadi nyingine tena kwenye makaratasi tu.

No comments: