Mbunge wa Kwela, Dk Chrisant Mzindakaya amewashambulia wanaowatuhumu wenzao kuwa ni mafisadi kwa kusema kuwa nao ni mafisadi na wana roho mbaya.
Mbunge huyo pia amewatuhumu wanaomlaumu Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kuwa wana roho za kishetani.
Mzindakaya amesema bungeni leo kuwa, wanaosema wenzao ni mafisadi wana roho za kifisadi na amehoji kwa nini wawaandame wenzao. “Na kwa nini wewe umezaliwa kuandama wenzako tu?” amehoji Mzindakaya wakati anachangia hoja ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2009/2010.
Amesema, watu hao wana roho mbaya, na wanajifanya wazuri kwa kuwa hawana moyo wa kuthubutu. “Binadamu ana kasoro moja, ukifanya mema kumi, ukakosea moja atafuta yote” amesema mbunge huyo katika kikao cha 11 cha mkutano wa 16 wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma.
Amejisifu kwa kuwa na moyo wa kuthubutu uliomuwezesha kuwa mkulima bora mkoani Rukwa, anajivunia hilo na hahitaji kusifiwa. Naye Mbunge wa Same Mashariki, Anne Killango Malecela jana jioni aliwaponda wanaotaka kuwanyamazisha wanaopinga ufisadi akiwamo yeye.
“Kama wewe ni fisadi kwa nini nisikuseme, na ninaomba wananchi watambue kwamba hatutanyamaza hata siku moja” alisema wakati anachangia hoja ya bajeti hiyo.
Ameitaka Serikali ilichukulie hatua kali gazeti lililotangaza kuwa jimbo lake na majimbo mengine manne yapo wazi bungeni na isipofanya hivyo bungeni patakuwa hapatoshi. Mbunge huyo aliwaonyesha wabunge gazeti hilo lilitwalo Nipe Habari, na kusema kuwa ni gazeti uchwara na linaandika mambo ya kihuni.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo, gazeti hilo limeandika kuwa, majimbo matano yapo wazi, na kwamba, waliokuwa wabunge wa maeneo hayo ni mgambo katika vita dhidi ya ufisadi nchini.
“Patakuwa hatatoshi tena hapa, katika hili sitakubali” amesema Mbunge huyo aliyetangazwa kuwa ni mwanamke jasiri zaidi Tanzania. Alimtaka Waziri Mkuu atapokuwa anajibu hoja za wabunge wanaochangia hoja ya bajeti ya ofisi yake amweleze gazeti hilo limechukuliwa hatua gani kali.
“Jambo hili limenikera sana, jambo hili limeniudhi”alisema Killango Malecela bungeni wakati anachangia katika hoja ya bajeti ya ofisi Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2009/2010.
Alitaka vyombo vya habari viache kuandika mambo ya kihuni na akadai kuwa, magazeti kama hayo yanaweza kuiingiza nchi kwenye vurugu.
“Hakuna dhambi kubwa kama hii, Mheshimiwa Spika kesho asubuhi litasema kiti cha Rais kipo wazi” alisema na kutoa kauli iliyoashiria kuwa habari hiyo iliandikwa na wanaounga mkono ufisadi.
Naye Mbunge wa Viti Maalum, Grace Kiwelu amewatuhumu watendaji wa Halmashauri wakiwamo wanasheria kuwa ni wala rushwa, hawanna maadili, na wanawakandamiza wananchi kwa maslahi yao.
“Sijawahi huona hata siku moja tajiri ananyang’anywa ardhi, masikini ndiyo wananyang’anywa ardhi” amesema Mbunge huyo leo wakati anachangia bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu.
Amewatuhumu pia watumishi wa umma kuwa ni watoro, wanatumia muda wa kazi kufanya shughuli zao binafsi, wanaacha makoti na mikoba ofisini kama kiini macho. Wakati anachangia, amesema pia kuwa Tanzania inahitaji wawekezaji kwenye sekta ya viwanda na si wa kujenga migahawa au kuuza maua.
Amesema, kuna raia wengi wa China nchini wanaofanya biashara zinazoweza kufanywa na watanzania hivyo wachunguzwe kwa madai pia kwamba, wanawanyanyasa wananchijiriwa katika biashara hizo na wanalipa mishahara midogo.
No comments:
Post a Comment