Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto itawasaka watu wanaowatumia watoto wa kike kufanya biashara ya ngono na kuwachukulia hatua za kisheria.Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dk Lucy Nkya amesema, Serikali imepata taarifa kuhusu kuwapo kwa biashara hiyo haramu inayofanywa hasa na wanawake wanaojipatia fedha kwa kuwauza watoto wa kike kwa wanaume ili wafanye nao ngono.
Dk Nkya ametoa onyo kwa wanaofanya biashara hiyo waache mara moja, na yupo tayari kushiriki kuwasaka wahusika ili wachukuliwe hatua.Ameyasema hayo katika ofisi za Bunge mjini Dodoma muda mfupi baada ya kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika kesho.
Kiongozi huyo wa Serikali amesema, kuwatumia watoto kufanya biashara ya ngono ni unyama hivyo Wizara hiyo itafanya utafiti kubaini maeneo walipo watoto hao, wahusika wanaofanya biashara hiyo, na maeneo wanapotoka watoto hao.Amewataka wazazi wawe waangalifu ili kuhakikisha watoto wanapata haki wanazostahili ikiwamo ya kulindwa, na ameziagiza pia kamati za shule zifuatilie maendeleo ya watoto shuleni.
Dk Nkya amesema, watoto watakaokamatwa watapelekwa kusoma katika vyuo vya maendeleo ya jamii ili wapate stadi za kazi zitakazowasaidia kujiajiri.Kuna taarifa zinazodai kuwa, kuna watu hasa wanawake wanaochukua watoto wa kike vijijini na kuwapeleka mjini na kuwafanyisha biashara ya ngono.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, watoto hao wamewekwa sehemu moja chini ya uangalizi wa wanawake hao, na kwamba kazi ya wasichana hao ni kufanya ngono na wanaume wanaotoa fedha kwa ajili ya huduma hiyo.Inadaiwa kuwa, ngono hiyo ni biashara, kiasi cha fedha wanazotozwa wanaume hutokana na makubaliano ya mwanaume mwanamke anayemiliki watoto hao, na kwamba, sehemu kubwa ya mapato anachukua mwanamke huyo na si mtoto.
Watoto wanaoishi katika mazingira ya hatari ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.Dk Nkya ametaja changamoto nyingine kuwa ni kuwapo kwa watoto wanaoishi mitaani, kuongezeka kwa idadi ya watoto yatima katika jamii, na kuongezeka kwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji watoto majumbani, shuleni na mitaani.
Amesema, Serikali inaandaa mpango mkakati wa jamii kudhibiti watoto wanaoishi mitaani ili kusaidia upatikanaji wa mahitaji ya watoto hao kama vile chakula, mavazi, malazi, matibabu na elimu.Dk Nkya pia amewaeleza waandishi wa habari kuwa, Serikali inaendelea na mchakato wa kuandaa muswada wa sheria ili itungwe sheria moja kuwahusu watoto ili kuwawezesha watoto wapate haki zao kwa urahisi.
No comments:
Post a Comment