Wednesday, June 3, 2009
Mradi wa maji wa mabilioni ya shilingi kuchochea maendeleo Shinyanga
Rais Jakaya Kikwete alipotembelea Kijiji cha Iselamaganzi, Shinyanga .
Baada ya miaka mingi ya adha kubwa ya maji katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga, hatimaye tatizo hilo limepatiwa ufumbuzi.” Haya ni maneno ya furaha, aliyoyatoa Rais Jakaya Kikwete, alipokuwa akiwahutubia wananchi wa mikoa ya Shinyanga na Mwanza katika Kijiji cha Ihelele Wilaya ya Misungwi Mkoa wa Mwanza.
Alisema hayo wakati wa sherehe ya uzinduzi wa Mradi mkubwa wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Shinyanga hadi Kahama. Siku hiyo, Kijiji cha Ihelele kiliandika historia ya kukumbukwa, hasa mara baada ya viongozi wa kitaifa kumiminika kijijini hapo kwa lengo la kushuhudiwa uzinduzi huo. Huo ni mradi mkubwa wa maji kuwahi kuzinduliwa kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika, ukiacha Afrika ya Kusini ambayo ndiyo iliwahi kuzindua mradi wa aina hiyo.
Ngoma, vifijo, vigelegele na bashasha za hapa na pale zilitumbuiza hadhara ya uzinduzi huo. Akinamama hawakusita kuimba nyimbo za burudani na wengine walisakata muziki wa dansi. Yote hayo, yaliashiria kuwa kilio chao cha muda mrefu cha kutafuta maji, sasa kimetoweka. Miongoni mwa viongozi mashuhuri waliohudhuria uzinduzi huo ni Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Benjamin Mkapa na waliowahi kuwa mawaziri wa maji, akiwamo Edward Lowassa na waliowahi kuwa makatibu wakuu wa wizara hiyo.
Wageni wengine walikuwa ni wabunge. Rais Kikwete aliwashukuru wote kwa uvumilivu mkubwa, waliouonyesha tangu kuanzishwa kwa mradi huo mwaka 2000. Kwa namna ya kipekee, alimshukuru Rais mstaafu Mkapa kwa uwezo wake wa kuthubutu kuuanzisha mradi huo. “Napenda nimpongeze kwa namna ya kipekee Mzee Benjamin Mkapa, ambaye wakati wa uongozi wake, mpango wa kujenga mradi huu ulibuniwa na kuanza kutekelezwa. Nampongeza kwa moyo wake wa kuthubutu.
Kama mjuavyo mradi huu haukupata fedha za wafadhili, wafadhili walikuwa wanaukwepa kutokana na ukubwa wa gharama zake, lakini Mkapa akathubutu. Nakupongeza sana mzee wetu,” alisema Rais Kikwete. Rais anawapongeza pia wote waliohusika, kwa namna moja ama nyingine, kukamilisha mradi huo. Anawapongeza wananchi wa mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Kahama, kwa kuwa wavumilivu kipindi chote, ambacho mradi ulikuwa unajengwa.
“Nawapongeza pia wasanifu wa mradi na wajenzi, kwa kazi nzuri waliyoifanya, tena kwa kuifanya kwa wakati na kiwango kinachostahili,” anaeleza Rais Kikwete. Rais anasema kuwa ujenzi wa mradi huo umechukua takribani miaka mitano, jambo ambalo licha ya kuchelewa ni la kujivunia katika serikali ya Awamu ya Nne ya kuwaletea wananchi wake maisha bora kwa kila Mtanzania.
Soma zaidi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment