Wabunge wameitaka serikali ifanye marekebisho makubwa kwenye bajeti ya mwaka ujao kwa maelezo kuwa inategemea zaidi fedha za nje na kuwapo upendeleo kwenye ujenzi wa barabara. Wabunge wa Kamati ya Uchumi na Fedha ambao walikuwa wanajadili mfumo wa mapato na matumizi ya serikali katika mwaka ujao wa fedha, walisema kama bajeti hiyo itaenda bungeni kama ilivyo, kuna uwezekano mkubwa wa kutopita.
Mbunge wa Mvomero, Suleiman Sadiqq (CCM) alisema kama Wizara ya Fedha na Uchumi haitarekebisha bajeti hiyo kwa kuingiza sehemu ya barabara iliyoko jimboni kwake ili ijengwe kwa kiwango cha lami, ataenda kulalamika kwa Rais Jakaya Kikwete.
Barabara hiyo inatokea Kilosa kwenda Dumila na kupitia Mvomero kwenda Handeni hadi Korogwe. “Rais alishaahidi kuwa barabara hii mwaka ujao itajengwa kwa lami, lakini angalia kule ilikotokea Kilosa ambako ni kwako wewe Waziri umeweka lami.
Mlipofika Mvomero mmeruka hadi mkaenda kuanzisha lami Handeni kwa Dk. Kigoda ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hii hadi Korogwe, hii inamaanisha nini, nasema sitakubali nitaenda kulalamika kwa Rais,” alisema.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), alishangazwa na bajeti hiyo kutotenga fedha kwa barabara za Magharibi badala yake fedha nyingi zimerundikwa kwenye barabara za Mashariki mwa Tanzania.
“Kwa nini Magharibi ambako kuna shughuli nyingi za kiuchumi tunaendelea kuwasahau…angalia Chalinze mnapanua barabara ya lami lakini Kigoma, Rukwa, Tabora hawajui lami inafananaje?” Alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu, Devota Likokola (CCM) alishutumu mpango wa serikali wa kupendelea baadhi ya mikoa katika ujenzi wa barabara wakati wakazi wa Mbamba Bay, Mbinga, Tunduru, Mangaka hadi Masasi tangu wazaliwe hawajawahi kuona lami.
“Wananchi wetu wanayaona haya na wanatuhoji, kuna barabara inaenda Iringa kila mwaka inabadilishwa lami, lakini huko kwetu wananchi hawajui lami kwa nini mnataka kuleta matabaka ya maendeleo katika nchi hii?” Alisema na kuongeza kuwa wakati umefika Wizara ya Fedha na Uchumi itenge keki ya taifa kwa kuangalia uwiano wa maeneo.
Mbunge wa Ilemela, Anthony Diallo (CCM), alisema bajeti hiyo kwa sura iliyonayo kama itaenda bungeni itakuwa ya kwanza kukataliwa na wabunge kutokana na kuwa na upendeleo kwenye ujenzi wa barabara.
Soma zaidi
No comments:
Post a Comment