Tuesday, June 9, 2009
Utata uhamishaji mabilioni BoT
- Ni Sh bilioni 137 za Tanesco na IPTL
- Gavana Ndullu asema hajajulishwa
TAKRIBAN Sh. bilioni 137.8 zilizohifadhiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika akaunti ya pamoja ya Serikali na kampuni ya kufua umeme ya IPTL, zimeandaliwa mpango wa kuhamishwa kwa utaratibu unaoibua maswali mengi zaidi, Raia Mwema imedokezwa.
Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kwamba kuna mpango wa kuhamisha fedha hizo kutoka BoT kwenda kwenye akaunti tofauti bila maelezo ya kuridhisha.
Haikuweza kufahamika mara moja fedha hizo zitahamishiwa kwenye akaunti ipi kutokana na nyaraka husika kutobainisha taarifa muhimu kuhusiana na uhamishaji huo.
Mpango huo umekuwapo kutokana na kile kinachoonekana kuwa ni fedha hizo ‘kuzubaa’ BoT baada ya mali za IPTL kuwekwa chini ya mfilisi, ambaye ni Wakala wa Usajili, Vizazi na Vifo (RITA) bila kujumuisha fedha hizo.
Ikiwa mpango wa kuhamisha fedha hizo utafanikishwa kabla ya mwaka 2010, itakuwa ni mtikisiko mwingine mkubwa kutokea ndani ya BoT baada ya ule wa fedha zilizoibwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. Fedha zilizothibitishwa kuibwa EPA mwaka 2005 ni Sh bilioni 133.
Fedha hizo ambazo ziliwekwa kwenye akaunti maalumu (Escrow account) ndani ya BoT hadi kufikia Sh 137, 769, 763, 052.84, zilitokana na malipo yaliyokuwa yalipwe kwa kampuni ya IPTL kutokana na kuliuzia umeme Shirika la Umeme nchini (Tanesco), kabla ya kubainika kuwapo udanganyifu uliofanywa na kampuni hiyo tata kuhusiana na gharama halisi za uwekezaji.
Raia Mwema imefanikiwa kupata mawasiliano ya awali ambayo yanaonyesha kuwapo kwa barua kutoka RITA kwenda kwa Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndullu, kwa lengo la kuomba mfilisi huyo, kwa niaba ya IPTL, apatiwe udhibiti wa fedha hizo.
Barua hiyo, ambayo Raia Mwema imepata nakala yake, ni yenye kumbukumbu namba ADG/OR/IPTL/GEN/009, ya Mei 6, mwaka huu.
Nakala za barua hiyo pia zimepelekwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mtendaji Mkuu wa Tanesco.
“…Mfilisi wa IPTL ameamua kutumia mamlaka yake kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa kifungu cha 188 ya sheria za makampuni ili kudhibiti kikamilifu akaunti ya pamoja (Escrow account) ya IPTL Tegeta ambayo ipo BoT,” inasema barua hiyo ambayo pia inaweka bayana kuwa wenye mamlaka ya kutoa fedha hizo katika akaunti hiyo ni watu wawili tu.
Watu hao wawili waliotajwa katika barua hiyo ambayo sahihi zao ndizo zinazoweza kutoa mabilioni hayo ni Theophil Rugonzibwa na Dk. Magesvaran Subramaniam anayetajwa kuwa raia wa kigeni.
Imeelezwa na barua hiyo kwamba watu hao ndio wenye mamlaka ya kutoa maelekezo kwa BoT na kutoa fedha hizo kutoka katika akaunti hiyo ya pamoja, wakimtaka Gavana Ndullu kutekeleza matakwa ya mkataba huo.
Gavana wa Benki Kuu, Profesa Ndullu, ameliambia Raia Mwema kwamba hadi jana Jumanne alikuwa hajapokea maelekezo yoyote kuhusiana na kutolewa kwa fedha hizo akikwepa kufahamu lolote kuhusiana na barua ya RITA.
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Idrissa Rashidi, hawakuweza kupatikana jana ikielezwa kuwa walikuwa na mikutano muhimu, lakini habari za ndani ya ofisi zao zimethibitisha kufahamu kuwapo kwa mawasiliano ya kutaka kuchukuliwa fedha hizo.
Habari zaidi zinasema kwamba wakati kukiwa na mkakati wa kuhamisha fedha hizo kumekuwapo Azimio la Bunge linalotaka suala hilo kumalizwa haraka nje ya mahakama ili fedha hizo kutumika katika kumaliza madeni ya Tanesco na kuichukua mitambo ya IPTL ili ibadilishwe na kutumia gesi na hivyo kupunguza makali ya bei na uhaba wa umeme nchini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe, ambaye kamati yake ndiyo iliyowasilisha mapendekezo yaliyotoa azimio hilo, alisema “uamuzi wowote utakaofikiwa kuhusiana na IPTL unapaswa kuzingatia azimio la Bunge.”
Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za Bunge (hansard) azimio ambalo linahusu IPTL lilitolewa Aprili 29, 2000 likiwa na maelezo ya kuitaka Serikali na wadau wengine wa suala hilo kuzingatia zaidi maslahi ya Taifa katika maamuzi yao.
“Suala la IPTL limalizwe kwa haraka nje ya Mahakama ili kuharakisha ubadilishaji wa mtambo huo ili utumie gesi na hivyo kuongeza uzalishaji wa umeme wa megawati 100 ambao unatakiwa hivi sasa ambapo kuna nakisi kubwa ya umeme na hivyo kupelekea mgawo unaoumiza uchumi wa nchi,” inaeleza sehemu ya azimio hilo la Bunge na kuendelea;
Soma Zaidi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment