Tuesday, June 23, 2009

Takrima marufuku mwakani

Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 itafanyiwa marekebisho ambapo vipengele vinavyoruhusu takrima katika uchaguzi, vitaondolewa. Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya ofisi yake bungeni jana, Pinda alisema hatua hiyo ni sehemu tu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Pia alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itaandaa vigezo na utaratibu utakaotumika kugawa majimbo ya uchaguzi nchini. “Mapendekezo mengine (ya marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi) ni kuongeza muda wa kufungua kesi za kupinga matokeo na kuweka kikomo cha mgombea kujitoa katika uchaguzi,’’ alisema Pinda.

Vilevile katika marekebisho hayo, NEC itapewa mamlaka ya kuandikisha wapiga kura wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwa na kipindi maalumu cha kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga kura angalau mara mbili kati ya uchaguzi mmoja hadi mwingine.

Alitaja mapendekezo mengine kuwa ni kuipa NEC, mamlaka ya kufanya uchaguzi mdogo wa madiwani angalau mara mbili kwa mwaka, badala ya kila wakati kutokana na kumalizika kwa kesi mahakamani. Mapendekezo mengine kwa mujibu wa Pinda, yanalenga kubadilisha kipindi cha kufanya uteuzi wa wagombea, endapo mgombea urais au mgombea mwenza atafariki dunia. Kutokana na mabadiliko hayo, Pinda aliiomba jamii kuipa ushirikiano NEC wakati wa kutekeleza majukumu yake, ili wapiga kura wasikose haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi.

No comments: