-Vinywaji, vitafunio Ikulu Sh. mil 201
-Pesa za mavazi, mashuka na viatu zabanwa
MCHANGANUO wa mgao wa fedha katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2009/2010 unaonyesha kuwa Ikulu imetengewa Shilingi milioni 115 kwa ajili ya safari za nje ikilinganishwa na Sh. mil 82 ilizotengewa kipindi kilichopita.
Hiyo maana yake ni kwamba, bajeti ya safari za nje za Ikulu imeongezeka kwa takriban Sh. milioni 34.
Bajeti ya Ikulu ya safari za ndani ya nchi nayo imeongezeka kutoka Sh. 608,419,000 kwa bajeti ya mwaka 2008/2009 hadi Sh 723,360,000 kwa mwaka 2009/2010, ikiwa ni ongezeko la Sh. milioni 114.9.
Miongoni mwa mambo ambayo Rais Kikwete amekuwa akishutumiwa nayo na wananchi, ni wingi wa safari zake za nje ambapo inadaiwa kwamba zinachota mapesa mengi ya walipakodi; ilhali manufaa yake hayaonekani wazi.
Rais Kikwete ameingia katika rekodi ya kuwa rais wa kwanza wa Tanzania kusafiri mara nyingi kwenda Marekani katika kipindi kifupi tu cha utawala wake. Mpaka sasa ameshakwenda Marekani mara sita. Aidha ni nadra kumaliza mwezi mmoja bila kufanya safari ya nje; huku wananchi wakilalamika pia kwamba msafara wake mara nyingi unakuwa mkubwa.
Wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya Nje na na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliliambia Bunge kwamba serikali inaangalia uwezekano wa kupunguza idadi ya watu wanaosafiri na viongozi wa juu kwenda nje ya nchi baada ya kupata maelekezo kwa Rais Kikwete mwenyewe, jambo linalodhihirisha ujumbe kumfikia.
Mchanganuo unaonyesha pia kwamba bajeti ya Ikulu kwa ajili ya ununuzi wa mavazi, mashuka na viatu, imepunguzwa kutoka Sh. milioni 127,400,000 kwa mwaka wa fedha 2008/2009 hadi Sh. 116,400,000 mwaka wa fedha wa 2009/2010, ikiwa ni punguzo la Sh. milion 11.
Lakini Ikulu imeongezewa takriban Sh. milioni 201.6 katika bajeti yake ndogo ya vinywaji, vitafunio na huduma nyingine za malazi (hospitality supplies and services), ikilinganishwa na bajeti inayokwisha ya mwaka 2008/2009 kwa upande wa masuala ya utawala.
Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2008/2009, Ikulu ilipangiwa kutumia Sh 242,710,000 kwa ajili ya vinywaji na huduma nyingine za namna hiyo, lakini katika bajeti ya safari hii, yaani 2009/2010, imetengewa Sh 444,350,000 za huduma hizo.
Kwa mujibu wa mchanganuo wa Bajeti Kuu ya Serikali, matumizi katika kipengele hicho yanaonyesha kuongezeka kila mwaka wa bajeti, kuanzia mwaka wa fedha 2007/2008, ambapo matumizi halisi yalikuwa Sh. milioni 190.44, ikiwa ni ongezeko la Sh milioni 51.3.
Hali ni tofauti kidogo kwa Makamu wa Rais ambako gharama kwa ajili ya ununuzi wa mavazi, mashuka na viatu ni Sh 30,296,000, ikiwa kuna ongezeko ikilinganishwa na mwaka jana, ambako Sh. 22,840,000 zilitengwa. Hapa ni ongezeko la Sh. milioni 7.5 hivi.
Kwenye safari za ndani pia fungu la fedha limeongezwa na katika mwaka huu zimepangwa kutumika Sh. 344,200,000, ikilinganishwa na mwaka jana ambapo zilitengwa Sh. 256,970,000, ikiwa ni ongezeko la takriban Sh. milioni 87.2.
Safari za nje ya nchi za Makamu wa Rais zimetengewa Sh. milioni 25, tofauti na mwaka unaokwisha wa bajeti ambao zilitengwa Sh. milioni 2 ikiwa ni ongezeko la Sh. milioni 23.
Kwa upande wa bajeti ya Makamu wa Rais kuhusu vinywaji na vitafunio, zimetengwa kutumika Sh. milioni 214, ikiwa kuna ongezeko kwa kulinganisha na bajeti ya mwaka wa fedha unaokwisha ambayo ni Sh. milioni 137, hapa kukiwa na ongezeko la Sh. milioni 77.
Wakati takwimu hizo zikiwa kwa ajili ya Makamu wa Rais, kwa upande wa ofisi yake (Ofisi ya Makamu wa Rais) fedha zilizotengwa kwa ajili ya vinywaji baridi na moto, chai na vitafunio, ni Sh. milioni 12.5, tofauti na mwaka jana ambako hapakuwa na bajeti ya aina hiyo.
Maofisa katika ofisi hiyo wamepangiwa kutumia Sh 331,270,000 kwa ajili ya safari za nchini, fedha ambazo ni zaidi ya walizopangiwa mwaka uliopita Sh. 273,215,000, kukiwa na nyongeza ya kitita cha Sh. milioni 58.
Lakini wakati hesabu zikiwa hivyo kwa ajili ya safari za ndani, mambo ni tofauti kwa upande wa safari za nje za maofisa wa ofisi hiyo zikiwa zimepangwa kutumika Sh. milioni 331, ikiwa ni tofauti ya Sh. 270,000 na kiasi kilichotengwa kwa ajili ya safari za ndani ya nchini, lakini pia ni kiasi kikubwa zaidi kwa kulinganisha na fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli hiyo kwa mwaka jana ambazo ni takriban Sh. milioni 145.6.
Kwenye mavazi (mfano sare), viatu na mashuka zimetengwa Sh milioni 37.5, ikilinganishwa na Sh milioni tano za mwaka uliokwisha.
Kwa Waziri Mkuu, safari za ndani ya nchi zimepangwa kutumika Sh. milioni 636.6 ikiwa ni pungufu ya kiasi kilichotengwa mwaka jana ambacho ni Sh. milioni 842.34, kukiwa na upungufu wa Sh. milioni 205.7.
Kwa ufupi, Ikulu ni moja ya taasisi za serikali zilizoongezewa fedha za matumizi kama ya vinywaji na vitafunio, mambo ambayo yanapingwa na baadhi ya wabunge.
Wabunge hao wanaopinga ni pamoja na wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa ambaye aliliambia bunge, juzi jioni, kuwa matumizi hayo si kipaumbele cha matatizo mengi yanayoikabili nchi kwa sasa, kauli ambayo ilipata upinzani mkali kutoka kwa wabunge wa CCM.
Spika wa Bunge Samuel Sitta, aliingilia kati kwa kuwataka wabunge wenzake wa CCM kumuacha Dk. Slaa aendelee kutoa maoni yake na kwamba ana haki ya kufanya hivyo na hakuwa amevunja kanuni yoyote hadi hapo Bunge litakapokaa kama kamati kupitisha vifungu vya bajeti hiyo.
Kwa ujumla Ikulu imepangiwa matumizi ya Sh. bilioni 7.23 katika bajeti iliyopitishwa na bunge wiki iliyopita itakayoanza kutumika Julai mosi hadi Juni 30 mwakani.
No comments:
Post a Comment