KIKAO cha bajeti cha Bunge la Jamhuri ya Muungano kilianza wiki iliyopita mjini Dodoma. Kwamba safari hii kikao hicho kitachukua mwezi mmoja na wiki tatu tu kumalizika badala ya miezi mitatu, ni kitu cha kufurahisha.
Ni kwa msingi huo tunapenda kuipongeza Serikali yetu na Bunge letu, kwa kuchukua hatua hiyo ya kupunguza siku za kikao cha bajeti; hatua ambayo wananchi wamekuwa wakiisubiri kwa muda mrefu.
Tunatambua kwamba hatua hiyo ni moja ya mikakati ya Serikali ya kupunguza matumizi katika kipindi hiki ambacho uchumi wa dunia umeporomoka. Ni matarajio yetu, hata hivyo, kwamba Serikali itaendelea kuchukua hatua nyingine za kubana matumizi katika sekta nyingine.
Ni matarajio yetu vilevile kwamba kupunguzwa kwa siku za kikao hicho cha bajeti, hakutapunguza umakini wa Bunge letu; na kwamba wabunge wetu hawatatumia hatua hiyo kama kisingizio cha kutojadili vyema bajeti za wizara wakianzia na bajeti yenyewe ya Serikali.
Wiki iliyopita Serikali iliwasilisha bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2009/2010. Ni jukumu la wabunge kuhakikisha bajeti hiyo inaendana na hali ya sasa ya anguko la uchumi wa dunia; kwa maana kwamba kila senti inakwenda tu katika matumizi ambayo ni ya lazima.
Ni wajibu wa wabunge wetu kuisoma kwa makini bajeti hiyo ya Serikali na kuichambua ili wajiridhishe kama kweli inaweza kutuvusha katika kipindi hiki kigumu cha anguko la uchumi wa dunia. Na kama hawaridhiki nayo, basi, ni wajibu wao kuionyesha Serikali mapengo yanayostahili kuzibwa katika bajeti hiyo.
Kwa ufupi, wananchi wanatarajia, safari hii, kuuona umakini wa wabunge wao katika kuijadili bajeti ya Serikali yao kuliko ilivyopata kuwa tangu waingie bungeni miaka minne iliyopita.
Tunatarajia kwamba, kwa mara ya kwanza, wabunge wetu wataweka siasa za vyama pembeni na kujadili kwa umakini bajeti hiyo ambayo, kwa kiasi kikubwa, inaamua mustakabali wa Taifa letu katika kipindi hiki kigumu cha anguko la uchumi wa dunia.
Hatutarajii kuwaona baadhi yao wakisinzia bungeni wakati wa kuwasilishwa bajeti hiyo na wakati wa kujadiliwa. Tunatarajia kuona Bunge lililo hai kweli kweli lililosheheni wabunge wenye hoja nzito za kuisaidia Serikali namna ya kuwavusha Watanzania masikini katika kipindi hiki kigumu cha anguko la uchumi wa dunia. Kila la heri.
No comments:
Post a Comment