Wizara ya Fedha na Uchumi imesema, siasa za Tanzania ni nzuri na kuna mipango mizuri ya maendeleo ndiyo maana umasikini wa kipato unapungua. Hata hivyo Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Omar Yussuf Mzee amesema, bungeni mjini Dodoma kuwa, kuna watanzania wengi wanaishi kwa kula mlo mmoja. Kiongozi huyo wa Serikali amesema leo kuwa, umasikini ni mchakato, unapungua siku hadi siku.
Mzee ameyasema hayo wakati anajibu maswali ya Mbunge wa Viti Maalum, Magdalena Sakaya aliyetaka kufahamu ni kwa nini watanzani wengi bado ni masikini wakati nchi imepata uhuru miaka 48 iliyopita.
Mbunge huyo pia alidai bungeni kuwa, watanzania wengi bado ni masikini kabisa kwa kuwa hakuna siasa safi, na pia hakuna mipango mizuri ya kuwawezesha wananchi wapate maendeleo.
Naibu Waziri Mzee amewaeleza wabunge kuwa kuna umasikini wa aina tatu ukiwamo wa elimu, afya na kipato.Amesema, kama Tanzania isingekuwa na siasa safi na mipango mizuri ya maendeleo, takwimu zisingeonyesha kupungua kwa umasikini wa kipato nchini.
Amewaeleza wabunge kuwa, mwaka 1991, asilimia 21.6 ya watanzania wote milioni 24.8 walikuwa masikini kabisa. Kwa mujibu wa kiongozi huyo, mwaka 2001, Tanzania ilikuwa na watu milioni 31.9, asilimia 18.7 kati yao walikuwa masikini kabisa, na mwaka 2007, asilimia 16.5 ya watanzania milioni 38.3 walikuwa masikini kabisa.
Mzee amelieza Bunge kuwa, watanzania wengi bado ni masikini kwa kwa wengi wao ni wakulima wanaotumia jembe la mkono, bei za pembejeo za kilimo zimepanda, na pia mabadiliko ya hali ya hewa yanathiri uzalishaji kwa kuwa sehemu kubwa ya kilimo nchini hutegemea mvua. Ametaja sababu nyingine kuwa ni ukuaji mdogo wa sekta ya viwanda, wakulima kukosa mitaji, na pia ukosefu wa ajira.
No comments:
Post a Comment