Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ipo kwenye mchakato wa kuandaa utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa maabara katika shule zote za sekondari nchini unaotarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 592.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Gaudentia Kabaka amesema bungeni leo mjini Dodoma kuwa, mradi huo utahusisha pia ununuzi wa vifaa vya maabara hizo.Kwa mujibu wa Kabaka, mradi huo unatarajiwa kutekelezwa katika awamu ya pili wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari(MMES) kwa kuwashirikisha wadau wa maendeleo.
Mradi huo mkubwa utakuwa muendelezo mkakati wa serikali wa kuboresha elimu ya sekondari nchini ikiwa ni pamoja na kutoa ruzuku kwa ajili ya ujenzi wa maabara za sayansi kwenye shule hizo. Kati ya mwaka 2008/2009, Serikali ilipanga kutoa ruzuku za kujenga maabara 230 katika shule za sekondari, 182 zimejengwa, ujenzi wa maabara nyingine unaendelea na kwa mujibu wa Kabaka, utakamilika haraka iwezekanavyo.
Licha ya kujenga maabara hizo, ruzuku hiyo imelenga pia kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Kabaka amewaeleza wabunge kuwa, ili kutekeleza lengo hilo, katika kipindi hicho cha mwaka 2008/2009 Serikali ilitenga sh bilioni 3.9 kujenga maabara hizo na kuzinunulia vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Amesema, fedha hizo hazitoshi kujenga maabara na kununua vifaa katika kila shule hivyo Serikali imezishauri shule zifanye hivyo kwa awamu. Kikao cha sita cha mkutano wa 16 wa Bunge kinaendelea Dodoma, baada ya kipindi cha maswali na majibu, wabunge wataendelea kujadili bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2009/2010.
No comments:
Post a Comment