-Hoja yawasilishwa utungiwe sheria maalumu
MPANGO wa Serikali wa kuhami na kunusuru uchumi dhidi ya mtikisiko wa uchumi duniani, uliotangazwa na Rais Jakaya Kikwete, umetiliwa shaka na kambi ya upinzani ambayo imesema unaweza kuleta "EPA namba mbili".
Makombora dhidi ya mpango huo yalitoka Kambi ya Upinzani Bungeni kupitia kwa kiongozi wake, Hamad Rashid Mohamed. Kambi ya Upinzani imependekeza mpango huo kutungiwa sheria maalumu ya udhibiti kwa kurejea uzoefu wa baadhi ya nchi za Asia.
Mapendekezo hayo yanatajwa kulenga kuinusuru nchi na kile kilichoelezwa kuwa ni “EPA namba mbili”, hasa ikizingatiwa kuwa katika wizi wa fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), takriban Sh bilioni 133 zililipwa kwa kampuni nyingine hewa. Ikihofiwa kuwa huenda katika kufanikisha mpango huo na hasa suala la kufidia hasara za baadhi ya kampuni, zipo kampuni hewa.
Katika hotuba yake bungeni wiki hii, mjini Dodoma , Hamad Rashid Mohamed, kwa niaba ya wabunge wenzake kutoka vyama vya CUF, CHADEMA na UDP, alihoji masuala mbalimbali kuhusu matumizi ya fedha hizo za stimulus package, zipatazo Sh. trilioni 1.7, zilizotangazwa na Rais Kikwete.
“Tunataka sheria ya Appropriation Act iwe na Schedule maalumu ya Stimulus Package na iseme waziwazi nani atapata nini, kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge iwe inapata taarifa kila miezi 3 ya utekelezaji wa hiyo stimulus package.
“Ni ukweli uliowazi kuwa stimulus package inazinufaisha benki tu, kwa kuzipa mwanya wa kufanya biashara nzuri na Serikali kwa kutumia fedha za Serikali yenyewe, na ndio maana katika nchi nyingine serikali imelazimika kuwa na hisa ili kuhakikisha kuwa fedha iliyotolewa ambayo inatokana na kodi za wananchi inadhibitiwa na kurudi kwa walipa kodi na wapiga kura.”
Hamadi alisema katika bajeti ya mwaka 2007/08 na ile ya 2008/09 serikali ilijizuia kukopa kwenye mabenki, kwa kigezo kikubwa kuwa mabenki yaweze kufanya biashara ya kukopesha sekta binafsi na kuwa zuio hilo liliongeza ufanisi kwa mabenki kukopesha sekta binafsi kwani mikopo kwa sekta binafsi ilipanda hadi kufikia asilimia 40.
Stimulus Package itapunguza mikopo ya benki kwenda kwenye sekta binafsi, na yale mafanikio yaliyokwishafikiwa yatayeyuka, vinginevyo mabenki yawekewe viwango vya kufikia katika kutoa mikopo nje ya stimulus package.
“Kwa mujibu wa taarifa ya Sera ya Fedha ya BoT serikali itazikopesha benki Sh bilioni 270 kwa ajili ya kuzikopesha sekta binafsi. Itatoa Sh bilioni 205 ili kukopa kwenye benki hizo.
Je, benki hizo zikishindwa kutumia fedha zile ambazo serikali imeziweka ili kukopesha sekta binafsi kutumia fedha hizo kufanya biashara na serikali kwa fedha za serikali? Hili litadhibitiwa vipi? Waziri atueleze,”, alihoji Hamad na kuongeza kuwa;
“Mwaka huu wa bajeti ni ya kuongeza matumizi na madhara yake ni mpango huo wa kuhami uchumi kuongeza mfumuko wa bei.
“Serikali imeamua kufidia vyama vya ushirika na kampuni zinazonunua mazao ya wakulima na kuyauza kwa hasara. Katika soko huria kuna kupata faida na kupata hasara. Wafanyabiashara makini wa mazao hupanga bei zao za kununulia mazao kwa kuzingatia bei walioipata katika soko la baadaye.
“Hata hivyo wengine hawapendi kuchukua tahadhari kwa kutegemea kwamba bei itapanda na kwa hiyo watapata faida kubwa. Bei imeshuka kwa hiyo wamepata hasara.Ó Alihoji akisema; Je, hakuna wafanyabiashara wa mazao waliolipa mikopo waliokopa kwa kujibana. Serikali ina uhakika gani kuwa mikopo hii ilitumiwa vizuri?”
Pia alipendekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua kampuni zitakazopewa fedha kutoka katika mpango wa kuhami uchuni.
Alitaka CAG kwanza kuthibitisha kuwa hasara waliopata haikutokana na matumizi mabaya ya mikopo na kwamba, gharama ya ukaguzi huu ilipwe na benki zilizokopesha. Alionya kuwa, la sivyo serikali inaweza kuliingiza taifa katika EPA namba mbili.
Kwa upande mwingine, Hamad katika hotuba yake hiyo alihoji kama serikali iko tayari kusaidia wafanyabiashara, kampuni na benki zilizopata hasara lakini bia kuwapo kwa hatua zozote za kuwasaidia wakulima wanaopata bei mbaya ya mazao isiyorudisha gharama.
“Hivi sasa wakulima wa pamba hawavuni pamba yao kwa kuwa bei ya pamba ni ya chini sana na hakuna soko la uhakika. Si hotuba ya Rais wala ya Waziri wa Fedha iliyotoa matumaini kuwa walalahoi pia wanakumbukwa na watafidiwa hasara na athari walizozipata kutokana na mtikisiko wa uchumi duniani.
“Serikali imeamua kutoa udhamini wa madeni ambayo wakopaji kwa sababu ya msukosuko wa uchumi wa dunia wanapata matatizo kulipa kwa wakati. Madeni hayo yanafikia Shs.270 bilioni.
“Kuna hatari ya serikali kujiingiza katika kudhamini madeni ambayo hatimaye yatabidi yalipwe na serikali. Serikali inajiongezea mzigo wa madeni yanayoweza kutokea (Contigent Liabilities).
Serikali imeamua madeni haya yadhaminiwe kwa miaka miwili na siyo mwaka mmoja ili shughuli za Uchaguzi Mkuu wa 2010 ziwe zimemalizika. Hii itatoa mwanya kwa wanaodhaminiwa madeni wachangie kwenye kampeni na baada ya uchaguzi mzigo wa madeni ubebwe na serikali.
“Kuna hatari ya EPA nyingine kuzinduliwa. Ukaguzi wa kina wa mahesabu ya makampuni husika ufanywe na CAG kwa gharama za mabenki yaliyokopesha kabla ya serikali kuyadhamini makampuni haya,” alionya Hamad.
Kutokana na maelezo yake hayo, katika mazungumzo yake na Raia mwema nje ya ukumbi wa Bunge, Hamad alisema endapo Waziri wa Fedha na Uchumi hatatekeleza mapendekezo hayo na hasa suala la kutungia sheria stimulus package, basi wataamini kuwa huo ni mpango wa kuchota fedha ili zitumike katika uchaguzi kama ilivyo mabilioni ya fedha za EPA.
“Endapo serikali haitakubali haya na hasa suala la kuwapo kwa sheria ya usimamizi wa fedha hizo Sh trilioni 1.7 na pia kama haitakubali kampuni zitakazopewa fedha za kufidia hasara kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, ni wazi kuwa tutakuwa tumethitisha mpango huo ni “EPA namba mbili” alisema Hamad.
Waziri Mkulo anatarajiwa kutoa majibu ya hoja hizo pamoja na hoja nyingine za wabunge kesho wakati atakapokuwa akijumuisha mapendekezo ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2009/2010. Ijumaa wiki hii, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, anatarajiwa kuwasilisha bajeti kwa ajili ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2009/2010.
No comments:
Post a Comment