Wednesday, June 17, 2009

TRA goigoi

Wabunge wameishambulia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa ndiyo kikwazo cha kuboresha huduma katika bandari ya Dar es Salaam na imesababisha mrundikano wa shehena kutokana na urasimu wa kushughulikia nyaraka za waagiza bidhaa. Wakichangia bajeti ya Serikali jana, baadhi ya wabunge walisema licha ya Kampuni ya Kitengo cha Kuhudumia Kontena (TICTS) kuwa na matatizo yake, lakini urasimu wa wafanyakazi wa TRA wa kutaka kuthibitisha bei ya bidhaa ilikotoka kunachangia mrundikano wa shehena bandarini.

Mbunge wa Solwa, Ahmed Salum (CCM), alisema mifumo iliyowekwa na TRA katika kutoza ushuru bandarini, inakoroga mambo kuliko ilivyokuwa awali kwani ina michakato mirefu ya kushughulika mzigo wa mteja mmoja. Alisema TRA imechangia asilimia 70 ya mrundikano huo na ndio maana baadhi ya wafanyabiashara wameamua kupitishia shehena zao Mombasa, kutokana na kuchoshwa na urasimu huo unaosababisha mizigo kukaa muda mrefu bandarini.

“Kule wafanyabiashara wanafuata uharaka, kwani mzigo unakaa siku mbili licha ya kulipa gharama mara mbili ya ushuru unaotozwa na bandari ya Dar es Salaam,” alisema Salum. Mbunge huyo alisema bandari imewashinda viongozi waliopewa jukumu za kuisimamia na akapendekeza iundwe wizara maalumu ya kushughulikia bandari hiyo, badala ya kuiachia Wizara ya Miundombinu ambayo kila siku inaonyesha kushindwa.

Alisema TRA na wizara wamekuwa wakitupiana mpira kuwa kuna upande hauwajibiki, huku huduma zikiendelea kudorora kila siku bandarini hapo. Mbunge huyo alisema kama bandari ingesimamiwa vizuri, ina uwezo wa kuingizia nchi zaidi ya Sh trilioni 14 kwa mwaka, lakini kilichopo sasa ni porojo tupu. Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (Chadema), alisema msongamano uliopo bandarini unasababishwa na TRA, kwani wafanyakazi wake wanatengeneza fursa ya rushwa kwa kuchelewesha nyaraka za wateja kwa makusudi.

“Tuna matatizo makubwa pale bandarini kwa sasa, enzi za Nyerere, mzigo ulikuwa unamaliza siku mbili, leo unachukua wiki tatu hadi mwezi maendeleo yatatoka wapi?” alihoji Ndesamburo. Alisema mtindo wa ofisa wa forodha kurudisha nyaraka katika nchi ambako mzigo umetoka ili kujiridhisha bei, ndio unachangia mrundikano wa shehena bandarini na kujitengenezea ‘ulaji’.

Alishangaa kuwa wakati Kenya wanapanua bandari yao, mipango ya Tanzania ni kutaka kujenga bandari nyingine Bagamoyo. Pia alishangaa kuwa wakati uwanja wa ndege wa Dar es Salaam haujapanuliwa, kuna mpango wa kujenga uwanja mwingine mpya Bagamoyo. “Hivi kama hatujaimarisha hii miundombinu iliyopo sasa, kwa nini tunataka kwenda Bagamoyo kujenga bandari na uwanja mwingine wa ndege, kwa nini au kwa vile Rais Kikwete (Jakaya) na Waziri wa Miundombinu wanatoka Bagamoyo?” alihoji mbunge huyo.

Mbunge wa Tabora Mjini, Siraji Kaboyonga (CCM), alisema bandari ya Dar es Salaam ni mgodi ambao kama Taifa litaamua kuelekeza nguvu zake huko, nchi itaondokana na umasikini na kuombaomba wakati wa bajeti. Alisema Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia na nyinginezo, zinategemea bandari hii kupitisha shehena zao, hivyo akataka Serikali ifanye kila linalowezekana kuimarisha bandari hiyo.

“Tuondoe ukiritimba kwa TICTS ili uwepo ushindani wa kupakia na kupakua kontena pale bandarini, itasaidia kupunguza mrundikano wa shehena,” alisema Kaboyonga. Mbunge wa Viti Maalumu, Khadija Salum Al Qassmy (CUF), alisema kutojiamini kwa wafanyakazi wa TRA kumechangia kudhoofisha huduma ya bandari ya Dar es Salaam na akatoa mfano kuwa bandari ya Mombasa mzigo unachukua siku tatu, lakini Dar es Salaam ni siku 21. Alisema ‘long room’ ya TRA ambayo kila siku inaundiwa mtandao tofauti tofauti pia haijaleta ufanisi uliotarajiwa.

“Kwa mfano mtu unatuma nyaraka zako kwa mtandao, ukienda pale, unaambiwa hazijafika hii ni ajabu sana.” Alisema nchi kama Hong Kong, uchumi wake unategemea bandari, lakini nchini maneno ni mengi kuliko vitendo, ndiyo maana bandari ya Dar es Salaam imeelemewa na shehena, kutokana na watendaji wazembe kutochukuliwa hatua za kisheria.

Alipendekeza Serikali ipunguze maneno badala yake ifanye kwa vitendo kuboresha bandari ya Dar es Salaam ili nchi jirani zisiendelee kuchukua mipango ya Tanzania na kuiendeleza. “Ni kweli wenzetu wanachukua mipango yetu wanaifanyia kazi, ndiyo maana Mombasa inazidi kupanuka.” Mbunge wa Kwamtipura, Zuberi Ali Maulid (CCM) alisema wakati magari yameshuka ushuru Japan, maofisa wa TRA bado wanang’ang’ania kuwatoza ushuru wananchi kwa bei zao za miaka ya nyuma.

No comments: