“Ajira Bila Ujira! ”
Maendeleo ya nchi yoyote hutegemea wazalishaji mali. Kuna mahesabu anuai yanayofanywa ili kupata pato halisi la nchi husika. Pato la taifa -GDP- hupimwa kwa nguvu kazi inayolipwa. Katika jamii kuna kundi la wafanyakazi ambao pamoja na kufanya kazi nyingi mchango wao ni mdogo katika pato la taifa. Kwa sababu ajira zao hazina ujira rasmi. Kundi hili ambalo mara nyingi hutunza nguvu kazi ya taifa inayotumika katika kuzalisha, limepewa jina la “uchumi wa matunzo na kazi bila malipo” yaani kwa tafsiri (sio rasmi) “Home Based Care Economy”. Wafanyakazi waliopo katika kundi hili ni wanawake na watoto wa kike na mara nyingi kazi wanazozifanya ni pamoja na; kupika, kufua, kusafisha nyumba, kutafuta maji na kuni, kulima shamba la familia kutunza watoto na wagonjwa n.k.
Hali halisi ya pato la taifa limeweka kipaumbele katika uchumi wa uzalishaji viwandani na madini. Sera mbalimbali za nchi zimeendelea kuwekezwa katika maeneo haya mawili muhimu. Mifano ya baadhi ya sera za taifa zinazowekea mkazo katika hili; zimetajwa kwa uchache ni pamoja na Sera ya nishati; Afya; Maji; Miundombinu; Elimu; na pia bajeti ya nchi.
Sera ya nishati haiweki wazi mikakati ya kuwarahisishia wananchi kupata nishati nafuu na mbadala kwa matumizi ya nyumbani, na kwa sababu wanawake ndio watafutaji wakubwa wa nishati hutumia muda mwingi katika kutafuta nishati hiyo hasa kuni katika maeneo ya vijijini. Pia sera ya matunzo ya wagonjwa nyumbani “Home Based Care Policy” ni nzuri kama ilivyoainishwa, lakini serikali imeshindwa kutenga kiasi cha fedha za kutosha kuwahudumia wagonjwa, hivyo mzigo mkubwa wa kuwalea wagonjwa unarudi kwa wanawake na watoto. Eti wanasema kwa kuwa wao –wanawake na watoto- wanaupendo tangu awali. Sijui kama ni kweli?!
Katika sera ya maji serikali imeshindwa kabisa kusaidia wananchi wake kupata maji safi na salama, badala yake maji yamepelekwa katika viwanda vikubwa na migodi. Wanawake na watoto wa kike ndio wanaotafuta maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani; katika maeneo ya vijijini wanawake hutembea zaidi ya kilomita 20 kwa siku kutafuta maji. Katika kilimo hali ni iyo iyo, wanawake ndio wazalishaji wakubwa wa chakula cha nyumbani na kinachobaki kinauzwa kwa ajili ya kujipatia vijisenti kidogo. Katika elimu pia watoto wa kike wanashindwa kwenda shuleni kutokana na kuzidiwa na mzigo wa kazi za nyumbani na uzalishaji mashambani. Ili mradi katika kila sekta wanawake hawana afadhali!
Katika tafiti za karibuni zilizofanywa na mashirika ya wanaharakati zinazoonyesha wanawake wanatumia muda mwingi zaidi katika ajira zisizo na malipo kuliko wanaume (Takwimu zinaonyesha uwiano wa 24% - 6%). Na katika ajira zisizo na malipo wanaume wanatumia muda mwingi zaidi ya wanawake (uwiano upo 39% -24%). Wanaharakati wa utetezi wa usawa katika jamii wameshafanya chambuzi mbalimbali za sera, bajeti ya nchi, na kutoa machapisho na mafunzo mbalimbali ili kuweza kusambaza dhana hii ya “ajira zisizo na ujira” -ingawa ajira hizo ni muhimu- kwa wananchi walio wengi hasa wa vijijini ambao wanaoathiriwa sana na mfumo huu na kuitisha mjadala wa kitaifa katika kuondoa kabisa hali hii na kuleta usawa ama kuzipa ajira hizi hadhi yake katika mchango wa pato la taifa.
Wanaharakati bado wanauliza; Je, ni mikakati gani itumike katika kuboresha hali hii ikiwemo bajeti pamoja na kuimarisha harakati za ukombozi wa wanawake wa Tanzania?
No comments:
Post a Comment