ALIYEWAHI kuwa mshauri wa masuala ya michezo wa Rais wa Zanzibar Dk. Salmin Amour, Mohamed Raza, amezidi kusikitishwa na mwenendo wa baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, na hasa suala la kuporomoka kwa maadili, akihoji “iko wapi CCM ya mwaka 1977 iliyotokana na TANU na ASP?”
Raza ambaye wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, alimzawadia vifaa vya michezo Mbunge wa Same Mashariki kwa ajili ya shughuli za michezo jimboni kwake baada ya mbunge huyo kutunukiwa Tuzo na Marekani, wiki hii alizungumza na Raia mwema na kueleza masikitiko yake hayo.
“Wizi unatisha serikalini tena ukihusisha baadhi ya viongozi…zamani CCM ilikuwa haitaki mchezo wa namna hiyo na yeyote anayehusika hatua zilichukuliwa hata kama kiongozi anatuhumiwa tu, aliwekwa kwanza nje ya uongozi wa chama na serikali ili kupisha uchunguzi,”
“Lakini leo hii hili halifanyiki ndani ya CCM wapo viongozi watuhumiwa lakini wameachwa hawajasimamishwa, sisemi kwamba wana makosa moja kwa moja lakini kama mtu unatuhumiwa na kama unakipenda chama chako na huna shaka yoyote na huna uroho wa madaraka kwa nini usikae pembeni kupisha uchunguzi?
“Iko wapi CCM ya mwaka 1977 iliyozaliwa baada ya kuunganishwa kwa vyama vyenye uadilifu na uzelando wa TANU na ASP?” alihoji Raza.
Katika jitihada za kumwondoa katika lawama hizo Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, Raza aliwatupia lawama wasaidizi wa kiongozi huyo mkuu wa nchi, akiamini kuwa hawezi kufanya mambo yote mazuri kwa nchi peke yake bila mwongozo mzuri na bora kutoka kwa wasaidizi wake.
“Kwanza, Rais ameonyesha utayari mkubwa wa kupiga vita ufisadi na ubadhirifu wa aina yoyote na ndiyo maana leo tunaweza kuzungumza hivi lakini utayari huu wa Rais unaonekana kupingwa kwa chini chini na baadhi ya wasaidizi wake. Kuna hali ya kulindana kuanzia katika chama hadi serikalini na taasisi nyingine.
“Kama chama kingekuwa kinamuunga mkono Rais bila shaka yoyote ni lazima watuhumiwa wengine wenye nyadhifa na ambao bado wako katika chama kama viongozi wangesimamishwa kwanza kupisha uchunguzi na kama watabainika safi warejeshwe huu ndiyo utaratibu bora wa chama bora au serikali bora,” alisema Raza.
“Leo hii utasikia au kuona baadhi ya viongozi wanashindwa kutembea mitaani mchana kwa kuhofia kuzomewa kuwa ni mafisadi…wengine wakitajwa wanajidai kuwa huo ni ubaguzi wa rangi…mimi nasema hakuna ubaguzi wa rangi katika suala la ubadhirifu.”
“Mtu utahukumiwa kwa matendo yako kama ni mwizi utaitwa mwizi na kama ni fisadi utaitwa fisadi hakuna cha ubaguzi wa rangi hapa…tusipotoshe watu. Matendo yenu ndiyo yanayotumiwa na wananchi kuwahukumu,” alisema Raza.
Soma zaidi
2 comments:
ehe ni kweli kama fisadi ni fisadi ata kama ana rangi ya blue!
ehe ni kweli kama fisadi ni fisadi ata kama ana rangi ya blue!
Post a Comment