Thursday, June 4, 2009

Mfumo wa bajeti ulenge kukomboa wanyonge

Wiki ijayo serikali itawasilisha bungeni bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2009/2010 ikiwa ni ya nne tangu serikali ya awamu ya nne iingie madarakani Desemba 2005.

Bajeti hii inaiacha awamu hii na bajeti moja tu kukamilisha kipindi chake cha utawala cha miaka mitano ambacho kinahitimishwa Oktoba 2010.

Wakati wananchi wakitarajia kusikia bajeti hiyo kwa matumaini tofauti, tayari makundi mbalimbali ya kijamii yameanza kutoa maoni yao jinsi ambavyo wangependa ijielekeze.

Miongoni mwao ni Mtandao wa Kijinsi (TGNP) ambao jana walitoa maoni yao ambayo pamoja na mambo mengine wametaka serikali izibe matundu katika misamaha ya kodi ambayo imekuwa mingi na kuikosesha mapato mengi.

Kadhalika, wametaka juhudi ziongezwe ili bajeti inufaishe makundi yote katika jamii, ikiwa ni pamoja na kuwepo uwazi katika mipango na matumzi ya rasilimali za taifa kwa faida ya wananchi wote.

Maoni ya TGNP ni sehemu tu ya hisia na matamanio ya wananchi walio wengi ya kutaka kuwepo na bajeti inayolenga kunufaisha jamii kwa ujumla na si kusaidia waliopewa dhamana ya kupanga mipango kwa niaba ya wananchi.

Kwa hali hiyo basi, ni matarajio ya kila mwananchi kwamba serikali ya awamu ya nne inatambua kwamba iliahidi mambo mengi kwa wananchi wakati wa kuomba kura, ingawa yapo mazuri yaliyotekelezwa, lakini bado ahadi nyingi hazijaguswa.

Bajeti hii kama tulivyosema hapo juu ni ya nne ya serikali ya awamu ya nne, kwa maana hiyo sasa wananchi wanataka kuona walau ahadi zao zikitekelezwa kwa kiwango zaidi ya asilimia 70 sasa, kwa sababu muda uliobakia ni mfupi mno.

Hata hivyo, sisi tunatambua kwamba uchumi wa dunia umeyumba katika kipindi cha takribani mwaka mmoja uliopita. Mataifa makubwa na yenye nguvu kama Marekani na mengine ya Ulaya kama Uingereza ambao ni wafadhili wa miradi mingi nchini nayo yameyumba.

Pia tunatambua kuna uwezekano mkubwa kwamba misaada kutoka kwa mataifa hisani itapungua kwa kiwango kikubwa mwaka huu kwa sababu zilizo wazi kabisa; kwa maana hiyo tunaamini nguvu ya kutuvusha kama taifa katika bajeti ya mwaka 2009/2010 ni kwa kuongeza juhudi na mikakati ya kujitegemea.

Miaka nenda rudi kumekuwa na kilio juu ya matumizi bora ya rasilimali zetu kama kwenye uvuvi, uvunaji wa mazao ya misitu, uwindaji wa kitalii na mapato yanayotokana na madini yetu.

Maeneo haya yameanishwa mara nyingi kwamba kama mipango mizuri ikiwekwa na umakini ukawepo katika kuisimamia ni dhahiri Tanzania haitahitaji hata senti moja ya msaada kutoka kwa wafadhili.

Kila Mtanzania ni shahidi kwamba hoja juu za utajiri tulionao katika sekta ya uvuvi ilipokuwa inaelezwa, watu wachache sana walikuwa wanafahamu hadi pale Waziri wa Mifugo na Uvuvi, John Magufuli, alipofanikisha operesheni ya kukamata meli ya uvuvi iliyokuwa inavua bila kibali ikiwa na shehena ya samaki wenye thamani ya Sh. bilioni tatu!

Uvuvi wa namna hiyo umefanyika miaka na miaka, hakuna hatua inayochukuliwa; hali ni hiyo hiyo kwenye uwindaji wa kitalii na uvunaji wa wanayama wetu; kadhalika ndiyo hali katika uchimbaji wa madini yote ya nchi hii kuanzia dhahabu hadi kwenye vito vyote hasa Tanzanite.

Tunapoyakumbuka haya na tukitafakari hali ya kuyumba kwa uchumi wa dunia, na hisia kwamba wafadhili safari hii wataota mbawa, tunaona njia ya kujikomboa sasa ni kuwa makini katika matumizi ya rasilimali zetu.

Ni kwa njia hii tu tutaweza kuwa na bajeti ya maana ya mwaka ujao wa fedha kwa hali hiyo kuipa serikali nguvu ya kutekeleza ahadi ambazo wananchi walipewa mwaka 2005 wakati wa kuomba kura lakini bado hazijatekelezwa.

CHANZO: NIPASHE

No comments: