Monday, June 29, 2009

KAULI YA (FEMACT NA SAHRINGON) KUHUSU TAMKO LA SERIKALI JUU MJADALA WA UFISADI UNAOHUSU MAKAMPUNI YA MEREMETA , TANGOLD NA DEEP GREEN FINANCE LTD

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Sisi mashirika yanayotetea Usawa wa jinsia, haki za binadamu na maendeleo na ukombozi wa wanawake kimapinduzi (FEMACT)na mtandao wa mashirika yanayotetea haki za binadamu kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (SAHRINGON) tumeshangazwa na kauli iliyotolewa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samwel Sitta na Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda kwamba tuhuma za ufisadi na/au wizi mkubwa wa fedha za umma unaoyahusu makampuni ya Meremeta Ltd., Tangold Ltd. na Deep Green Finance Co. Ltd. haziwezi kuzungumziwa ndani ya Bunge la Jamhuri kwa sababu tuhuma hizo zinahusu mambo ya jeshi na/au usalama wa taifa. Aidha tunapenda kuweka msimamo wetu wazi kwamba hatukubaliani na kauli na/au msimamo huo wa Spika wa Bunge na Serikali kwa sababu zifuatazo:

Kwanza hatuamini kwamba ufisadi mkubwa unaotuhumiwa kufanywa kwa kutumia kivuli cha makampuni haya una uhusiano wowote na mambo ya jeshi na/au usalama wa taifa. Taarifa zilizoko hadharani zinaonyesha kwamba Meremeta Ltd. na Tangold Ltd. ni au yalikuwa makampuni ya kigeni na wala sio ya Kitanzania. Taarifa hizo zinaonyesha kwamba wakati Meremeta Ltd. iliandikishwa nchini Uingereza mnamo tarehe 19 Agosti 1997 na kufilisiwa huko huko Uingereza tarehe 10 Januari 2006, Tangold Ltd. iliandikishwa nchini Mauritius mnamo tarehe 8 Aprili 2005 na kupewa hati ya kutimiza masharti ya Tanzania mnamo tarehe 20 Februari 2006. Zaidi ya hayo makampuni hayo yalianzishwa na kuendeshwa kama makampuni binafsi ijapokuwa inaelezwa kwamba Serikali ya Tanzania kwa kupitia Hazina ilikuwa na hisa katika kampuni ya Meremeta Ltd.

Hakuna hata moja katika makampuni haya mawili ambayo imewahi kuwekwa katika orodha ya makampuni na/au mashirika ya umma na wala hesabu zake kukaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kama ilivyo sheria kuhusu hesabu ya fedha za umma. Aidha Meremeta Ltd. kwa kipindi chote cha uhai wake iliendeshwa na wamiliki wa kampuni ya Triennex (Pty) Ltd. ya Afrika Kusini iliyokuwa na hisa 50 katika Meremeta wakati Serikali ya Tanzania ikiwa na hisa nyingine 50 na makampuni mawili ya Kiingereza yakiwa na hisa moja kila kampuni. Msimamo wa Spika Sitta na Serikali una walakini mkubwa kwa sababu unaweza kutafsiriwa kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Idara ya Usalama wa Taifa ni kichaka cha kufichia ufisadi na wizi wa mali ya umma.

Kuhusiana na kampuni ya Deep Green Finance Co. Ltd., nyaraka zilizoko hadharani zinaonyesha kwamba Deep Green Finance iliandikishwa mnamo tarehe 18 Machi 2004 kwa madhumuni ya, pamoja na mengine, kufanya biashara ya wakopeshaji fedha. Licha ya kutokuwepo kwa ushahidi wowote wa kuonyesha kwamba Deep Green Finance iliwahi kufanya biashara yoyote na Serikali ya Tanzania, katika kipindi cha miezi minne tu kati ya tarehe 1 Agosti na 10 Desemba 2005, Benki Kuu ya Tanzania ililipa jumla ya shilingi 10,484,005.39 katika akaunti ya Deep Green Finance iliyokuwa NBC Corporate Branch, Dar es Salaam. Aidha, kuanzia tarehe 11 Desemba 2005 hakuna fedha yoyote iliyoingizwa katika akaunti hiyo hadi tarehe 27 Februari 2007 kampuni hiyo ilipovunjwa ‘kwa hiari’ ya wanahisa wake. Inasemekana kuwa jumla ya fedha bilioni 155 ziliibiwa kupitia makampuni hayo.

Kwa miaka mingi kumekuwa na taarifa za utatanishi kuhusu umiliki wa makampuni haya. Kwa mfano, Serikali imekuwa ikitoa taarifa kwamba Meremeta Ltd. ilikuwa ni kampuni ya Kitanzania iliyokuwa ikimilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa ajili ya mradi wake wa magari ya deraya ya Nyumbu, Kibaha, Mkoa wa Pwani. Hata hivyo, nakala ya usajili iliyotolewa na Msajili wa Makampuni wa Uingereza na Wales inaonyesha kwamba kampuni hiyo iliandikishwa nchini Uingereza tarehe 19 Agosti 1997 na ilifilisiwa huko huko Uingereza tarehe 10 Januari 2006. Aidha, taarifa ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ya tarehe 31 Mei 2005 inaonyesha kwamba Meremeta Ltd. ni tawi la kampuni ya kigeni iliyosajiliwa Tanzania kama tawi tarehe 3 Oktoba, 1997. Taarifa hiyo inaonyesha kwamba hisa 50 za Meremeta Ltd. zilikuwa zinamilikiwa na Kampuni ya Triennex (Pty) Ltd. ya Afrika Kusini, hisa 50 nyingine zilikuwa zinamilikiwa na Serikali ya Tanzania kwa kupitia kwa Msajili wa Hazina katika Wizara ya Fedha wakati makampuni mawili ya Kiingereza – London Law Services Ltd. na London Law Secretarial Ltd. - yalikuwa yanamiliki hisa moja moja za Meremeta Ltd. Kwa mgawanyo huu wa hisa za Meremeta Ltd., ni wazi kwamba makampuni binafsi ya kigeni yalikuwa yanamiliki sehemu kubwa zaidi ya hisa za kampuni hiyo.

Bunge limepewa wajibu wa kusimamia Serikali na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, 1977. Namna pekee ya Bunge kutekeleza wajibu wake wa kikatiba ni kutumia fursa ya wabunge kuuliza maswali kwa mawaziri na vile vile kwa kuunda Kamati Teule za Uchunguzi au kutumia Kamati za Kawaida za Bunge kuchunguza masuala mbali mbali yanayohusu uendeshaji wa Serikali. Masuala yanayohusu makampuni ya Meremeta Ltd., Tangold Ltd. na Deep Green Finance Co. Ltd. yamejadiliwa sana na Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali tangu mwaka 2007. Kwa muda wote huu, Serikali ya Tanzania haijawahi kuzikanusha rasmi tuhuma za ufisadi zinazoyahusu makampuni haya. Kauli za Spika Sitta na Waziri Mkuu Pinda zinadhihirisha kwamba matumaini hayo ya Serikali hayajafanikiwa. Msimamo wao wa sasa ni dhahiri unalenga kutumia kivuli cha usalama wa taifa au jeshi ili kuzima mjadala huu ndani na nje ya Bunge. Iwapo watafanikiwa kwenye jambo hilo hapana shaka kwamba watatumia kivuli hicho hicho kuzima mijadala mingine ndani na nje ya Bunge na uwezo wa Bunge wa kusimamia Serikali na uhuru wetu wa kushiriki katika mijadala inayohusu masuala mbali mbali muhimu kwa wananchi utafifishwa.

Ni dhahiri kuwa upotevu wa fedha bilioni 155 kupiti makampuni hewa ya Meremeta, Tangoald na Deep Green umeongeza kufukarishwa kwa wananchi walio wengi katika nchi yetu. Fedha hizo zingetosha:

•kujenga visima vya maji safi elfu kumi na tano (15,000) kwa thamani ya shilingi milion kumi (10 milioni) kila kimoja. Nchi yetu ina vijiji visivyozidi elfu kumi na mmoja. Kwa maana hiyo kila kijiji kingepata karibu visima viwili;
•Fedha hizi zinaweza kusomesha zingewezesha watoto zaidi la laki tano (500,000) kusoma bure shule za sekondari kwa gharama ya shilingi laki tatu kila mmoja;
•Kujenga zahanati 1,550 kwa gharama ya shilingi milioni mia moja kila zahanati. Kwa maana hiyo vijiji 1,550 hapa nchini vingepata zahanati;
•Fedha hizo zingeweza kutoa motisha kwa kulipa madaktari na watoa huduma katika sekta ya afya ili waweze kuwahudumia vizuri wagonjwa na hivyo kupunguza vifo visivyo vya lazima. Kwa mfano fedha hizo zingetosha kuajiri madaktari 6,458 kwa mwaka na kuweza kuwalipa shilingi milioni mbili kwa mwezi kila mmoja;
•Kadhalika fedha hizo zingeweza kujenga madarasa 17,222 kila moja kwa gharama ya shilingi milioni tisa. (9,000); au
•Kuajiri wauguzi 12,917 kwa mwaka na kila mmoja akiwa analipwa shilingi milioni mmoja (1,000,000) kwa mwezi

Kwa vile inaelekea Serikali haijawa tayari kuchukua hatua dhidi ya waliohusika na ufisadi uliofanywa kwa kutumia makampuni ya Meremeta Ltd., Tangold Ltd. na Deep Green Finance, tunadai mambo yafuatayo :

i.Bunge la Jamhuri liunde Kamati Teule ya Uchunguzi wa makampuni haya kama lilivyofanya kuhusiana na Kashfa ya Richmond;
ii.Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano atumie uhuru na mamlaka aliyopewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 kufanya uchunguzi maalumu (special audit) ya taarifa za fedha na/au mahesabu ya makampuni ya Meremeta Ltd., Tangold Ltd. na Deep Green Finance kwa nia ya kuhakikisha kwamba fedha zote zilizotolewa na Benki Kuu ya Tanzania kwa makampuni hayo ziliidhinishwa kisheria na kwamba zilitumiwa kwa ajili ya shughuli iliyoidhinishwa kwa mujibu wa sheria;
iii.Watakaogundulika kuhusika na kashfa hii ya fedha za umma wachukuliwe hatua zinazostahili; kisheria na kinidhamu
iv.Waziri Mkuu Mizengo Pinda achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kupotosha bunge juu ya umiliki wa meremeta
v.Tunawahimiza wanachi wote wa Tanzania wadai uwajibikaji wa wabunge wao na serikali yao kwa ujumla kuhusiana na wizi/ufisadi uliyofanywa na makampuni ya Meremeta, Tangoald na Deep green kwa sababu ni wizi mkubwa unaochangia kwa kiasi kikubwa wananchi wengi kuwa na maisha magumu hivi sasa

Imetolewa na FemAct na kusainiwa na
1.Tanzania Gender Networking Programme (TGNP)
2.Legal and Human Rights Centre (LHRC)
3.Concern for Development Initiatives in Africa (ForDIA)
4.Youth Action Volunteers (YAV)
5.The Leadership Forum (TLF)
6.Coast Youth Vision Association (CYVA)
7.Walio Katika Mapambano na AIDS Tanzania (WAMATA)
8.Tanzania Media Women’s Association (TAMWA)
9.Youth Partnership Countrywide (YPC)
10.Tanzania Human Rights Fountain (TAHURIFO).
11.HakiArdhi
12.Women in Law and Development in Africa (WILDAF
13.Women Legal Aid Centre (WLAC)
14.Lawyers’ Environmental Action Team (LEAT)
15.Tanzania Ecumenical Dialogue Group (TEDG)
16.Life Skills Association (LISA)
17.Women Fighting Against Aids in Tanzania Trust Fund (WOFATA)
18.Taaluma Women Group (TWG)
19.Marcus Garvey Foundation (MGF)

28 June 2009

No comments: