Tuesday, June 30, 2009

MEREMETA: Wananchi wanataka ukweli

NI jambo la kukatisha tamaa kwamba Serikali yetu, kwa mara nyingine, imeendelea kuwaficha wananchi ukweli kuhusu madai ya ufisadi uliotendeka katika mradi wa Meremeta ambao inaaminika umeteketeza fedha za umma Sh. bilioni 155.

Mwanzoni mwa wiki hii, si tu kwamba Serikali (kupitia waziri wake) ilishindwa, bungeni, kumjibu ipaswavyo mbunge wa CHADEMA, Dk. Willbroad Slaa, kuhusu mradi huo; lakini pia, kwa namna ya kushangaza, ilimtaka aachane na hoja hiyo.

Kauli hiyo ya kumtaka mbunge wa wananchi aachane na hoja hiyo, ni sawa na kuwaambia wananchi (ambao yeye mbunge anawawakilisha), kwamba hawana haki ya kujua ukweli ni upi kuhusu mabilioni ya pesa zao yanayodaiwa kutafunwa kupitia mradi huo wa Meremeta.

Hatukubaliani na hoja kwamba mradi wa Meremeta ni mradi unaohusisha jeshi letu la ulinzi (JWTZ), na hivyo ni jambo nyeti lisilostahili kujadiliwa bungeni! Hakuna jambo nyeti linalohusu madai ya uchotaji wa mabilioni ya pesa za umma ambalo halistahili kujadiliwa bungeni.

Tunaamini hivyo, kwa sababu, kama alivyosema Dk. Slaa, hapa tunazungumzia madai ya wizi, na wala hatuzungumzii siri za ndani za jeshi kama vile tuna kambi ngapi, tuna wanajeshi wangapi, tuna zana gani za kivita nk. Hapa tunazungumzia fedha za umma zilizochotwa, tunazungumzia madai ya wizi, na si siri za jeshi.

Isitoshe, kama serikali yetu ilijua kwamba jeshi ni asasi nyeti katika usalama wa taifa; ni kwa nini ililiruhusu lijitose katika biashara ya kununua dhahabu kupitia Meremeta? Tena katika zama hizi ambapo biashara duniani zinaendeshwa kwa uwazi?

Kwa hiyo, serikali bado ina deni kwa wananchi. Na deni hilo ni kuelezwa ukweli kuhusu madai kwamba mapesa hayo ya umma yaliyochotwa kupitia Meremeta.

Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Saerikali (CAG), alipata kusema kwamba Meremeta haimo katika makampuni ya mashirika ya umma, na hivyo ofisi yake haijawahi kukagua mahesabu yake.

Kama hivyo ndiyo, na hasa ikizingatiwa kuwa benki ya kigeni ilihusishwa katika mradi huo, wananchi wanataka kujua, miongoni mwa mambo mengine, ni nani hasa waliokuwa na hisa katika kampuni hiyo?

Kwa hakika, kiu hii ya wananchi ya kutaka kuujua ukweli kuhusu Meremeta, haitamalizwa kwa serikali kuwakatisha tamaa kina Slaa kwa kuwaambia watafute hoja nyingine. Itamalizwa tu kwa ukweli kuwekwa hadharani.

Kwa hiyo, bado tunaamini kuwa suala hilo linaweza kujadiliwa bungeni kwa namna ambayo siri nyeti zinazohusiana na masuala ya ndani ya jeshi letu hazitaguswa.

Ni hapo tu hilo litakapotendeka, kiu ya wananchi itatulizwa.

Maana; haingii akilini serikali yetu kulishirikisha jeshi katika uanzishaji wa kampuni (Meremeta) ya kufanya biashara ya dhahabu na hata kuwasiliana na mabenki ya nje ( Nedcor Trade Service ya Afika Kusini na Deutshe Bank AG ya Uingereza) kwa ajili ya mkopo, na kisha wananchi kuambiwa suala hilo ni siri baada ya pesa kutafunwa!

Tunafahamu kwamba demokrasia yetu haijakomaa vya kutosha; lakini tuige, basi, kwa wenzetu (kama Afrika Kusini) ambako skandali za manunuzi hata ya silaha za jeshi hujadiliwa bungeni.

Hakika; mzimu wa Meremeta utatulia tu kama wananchi, hatimaye, wataelezwa ukweli wote na sheria kuachiwa ifuate mkondo wake.

Chanzo: www.raiamwema.co.tz

No comments: