Wednesday, June 24, 2009

Mollel, Selelii, Mpendazoe wawasha moto


-Wizara za Miundombinu, Nishati zasubiriwa kwa hamu
-Mawaziri watatizwa na namna ya kuitetea bajeti

HALI ya mambo ndani ya Bunge si shwari. Kuna mgawanyiko wa dhahiri kati ya mawaziri na wabunge na mwelekeo wa hoja za baadhi ya wabunge dhidi ya Serikali unaonekana kuwaelemea mawaziri, Raia Mwema imebaini.

Wakati hali ikiwa hivyo, tayari Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ameahidi kulinda uhuru wa kuzungumza bungeni lakini kwa kuzingatia matakwa ya kanuni zinazosimamia mijadala.

Hali ya mambo kuwa magumu kwa upande wa Serikali ilianza kujitokeza mwanzoni mwa wiki hii, wakati Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM), alipoonyesha kukerwa na uamuzi wa mawaziri kwa kushirikiana na watalaamu serikalini.

Salelii alionyesha kukerwa na uamuzi wa kukarabati na kupanua barabara kutoka Same hadi Korogwe ambayo inapita kwa urahisi na yenye kiwango cha lami wakati maeneo mengine muhimu ya nchi yakikosa huduma hiyo.

Katika kuonyesha kukerwa na suala hilo, mbunge huyo alisema anashangazwa na uamuzi huo akiamini kuwa ungeweza kuwa na tija zaidi kama ungelenga kupanua kipande cha barabara kati ya Dar es Salaam hadi Chalinze, hatua ambayo ingepunguza msongamano wa magari hasa ikizingatiwa kuwa barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa nchi kwa kuwa hutumika kupitisha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi katika nchi za Malawi, Zambia na hata Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Lakini pia Salelii alionyesha kukerwa na uamuzi huo ambao pia ungeweza kuelekezwa katika barabara inayounganisha Mkoa wa Tabora na mikoa mingine, pia akiamini kuwa ni hatua ambayo ingechangamsha uchumi katika mikoa ya Magharibi mwa nchi.

Baada ya kuonyesha kukerwa huko mbunge huyo alijikuta akitumia maneno makali bungeni, na akitangaza kutaka mawaziri walaaniwe na kudai kuwa wamekuwa na hila na roho mbaya dhidi ya baadhi ya wabunge kwa kuwa wanapendelea miradi ya maeneo wanakotoka na mingine ambayo iko kwa baadhi ya wabunge vipenzi vyao.

Hatua hiyo ya Selelii kutumia maneno hayo ilimfanya Mbunge wa Pangani, Rished Abdallah, kuingilia kati akiomba mwongozo wa Spika akilenga kumtaka Spika kumwelekeza Selelii afute kauli yake ya kulaani mawaziri kwa kuwa ni ya kukera, ambayo ni kinyume cha kanuni za Bunge zinazosimamia mijadala.

Mbali na kulaani, Selelii aliwataka wabunge kusoma makaburi ambayo alidai yana maandishi yanayosema “Sisi tuliolala hapa tulikuwa kama ninyi” wengine wakitafsiri kauli hiyo kuwa uwaziri waliokuwa nao umetokana na ubunge na hivyo wanaweza kurudi kubaki wabunge na kwamba uwaziri si wa milele.

Lakini Spika Sitta hakuwa tayari kufanya hivyo na badala yake alisema haamini kama kauli hiyo ya Selelii ilifikia kiwango cha kukera kama ambavyo kanuni ya Bunge inavyotamka isipokuwa akasema ilikuwa ni kauli inayoonyesha hisia halisi za mbunge huyo.

Soma zaidi

No comments: