SERIKALI imesitisha mpango wake wa kuyafutia misamaha ya kodi mashirika ya dini na asasi zisizo za kiserikali (NGOs) kama ilivyopanga.
Hatua hiyo ya serikali inatokana na hatua ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia ushauri alioupata kutoka kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye juzi alikutana na viongozi wa dini na kujadiliana nao kwa kina kuhusu mpango huo wa awali wa serikali.
Waziri Mkuu aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana, kuwa Rais Kikwete aliridhia mashirika hayo ya dini na NGOs kuendelea kupewa misamaha ya kodi jana.
Alisema serikali imefikia uamuzi huo baada ya kuona kuwa mpango huo umepokelewa kwa upinzani mkali na Wabunge, viongozi wa mashirika ya dini, wananchi na wahisani wa nje ambao wanasaidia miradi ya maendeleo kupitia mashirika ya dini.
Alisema serikali imeona mpango huo haujaeleweka vizuri kwani azma ya serikali ilikuwa si kufuta misamaha ya kodi hata kama huduma muhimu za jamii kama afya, maji na elimu kama ilivyoeleweka.
Alisema lengo kubwa lilikuwa ni kujaribu kubana mianya ya matumizi mabaya ya misamaha hiyo kwa baadhi ya viongozi wa mashirika ya dini ambao wamekuwa wakitumia misamaha ya kodi kujinufaisha.
“Baada ya kuona kuwa suala hili limekuwa na mjadala mkubwa hasa kwa Wabunge wa CCM, ambao wametushauri tulitazame kwa upana wake kutokana na mchango mkubwa wa mashirika haya kwa wananchi, serikali tumeona ni vizuri tukawasikiliza.
“Kutokana na usikivu wa serikali, jana (juzi) nilikutana na viongozi wa dini na tukalijadili suala hili kwa kina ili kuona nini cha kufanya.
Alikuwepo Baba Askofu Malasusa, Baba Askofu Mokiwa, Baba Askofu Mwamasika, Shiekh wa Mkoa wa Dodoma aliyekuja na Masheikh wengine na viongozi wengine wa dini ambao walitueleza atahiri za kuendelea na mpango huu,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema rai ya viongozi hao wote kwa serikali ilikuwa ni kuisihi serikali kusitisha azma hiyo kwa vile ingeweza pia kuleta sura mbaya kwa wahisani wa nje ambao wanatumia fedha za walipakodi wao kuwasaidia wananchi wa Tanzania.
“Niliwaelewa ingawa pia niliwaeleza nia nzuri iliyokuwa nayo serikali katika mpango huu ya kubana maeneo ya misamaha kwani fedha hizo zikikusanywa zinaweza kuleta mchango mkubwa kwa maebdeleo ya wananchi wetu,” alisema.
Alisema kwa pamoja viongozi hao wa mashirika ya dini wameahidi kuisaidia serikali katika kuwasaka na kuwadhibiti viongozi wa dini wanaotumia mianya ya misamaha hiyo ya kodi kwa manufaa yao.
Alisema pia pande hizo mbili zimekubaliana kukutana ili kujadiliana mfumo mzuri utakaowezesha mashirika ya dini kuendelea na mfumo wa kutolipa kodi lakini wakati huohuo kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi.
Alisema ili kuziba nakisi ya makusanyo ya kodi itakayotokana na uamuzi huo wa serikali, Waziri Mkuu alisema tayari serikali imeainisha vyanzo vingine vya fedha vitakavyoweza kuziba pengo la mapato hayo ambayo yangepatikana kwa mashirika ya dini kulipa kodi.
Alisema Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo atakapomaliza shughuli za kuwasilisha bajeti yake bungeni, atakutana na wataalamu wa Wizara yake na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Harry Kitilya ili kuunda kamati itakayosimamia marekebisho ya mfumo ili kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi kwa mashirika ya dini na NGOs
No comments:
Post a Comment