Thursday, June 25, 2009

Mgongano huu wa maudhui kati ya Ikulu na wizara!

KWA mara nyingine, Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2009/2010 imekuwa na kasoro kadhaa. Kasoro ambazo ni dhahiri si za bahati mbaya.

Kasoro hizo ni pamoja na kufutwa kwa misamaha ya ushuru wa mafuta ya petroli kwa kampuni mpya za uchimbaji dhahabu nchini, huku zile za zamani zikipewa fursa ya kipekee ya kujadiliana kwanza na serikali.

Mara kwa mara tumekuwa tukisikia serikali, kupitia kwa viongozi wake wakiwamo mawaziri na wakati mwingine Rais, wakisisitiza kuwa kazi kubwa ya serikali ni kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji. Huu ni wimbo wa muda mrefu, ulioanza kuchukua nafasi kubwa zaidi katika Serikali ya Awamu ya Tatu na kuendelezwa na serikali ya sasa.

Kwa kuzingatia wimbo huo, milango na hata madirisha ya uwekezaji nchini yalifunguliwa. Wawekezaji wa sekta ya madini wakaanzisha shughuli zao bila bughudha yoyote na zaidi, wakapatiwa misamaha mbalimbali ya kodi.

Wakafutwa machozi hata pale walipoigiza tu kulia. Wakati mwingine ilipojitokeza wakazi wa jirani na migodi wameingia katika mgogoro na wawekezaji hao, basi serikali ilisimama upande wao dhidi ya wananchi. Mifano iko mingi na sehemu ya ushahidi ni kesi zilizowahi kufunguliwa kuhusu migogoro hiyo.

Wapo wananchi waliohamishwa bila fidia inayostahili ilimradi tu wapishe ardhi waliyokuwa wakitumia ili mwekezaji achimbe dhahabu. Hapa, wakazi wa Nyamongo, wilayani Tarime wanafahamu suala hili kwa undani zaidi.

Lakini pia nani amesahau kiwewe cha uhusiano wa shaka, kati ya wawekezaji wa sekta ya madini na baadhi ya viongozi wa serikali kiliwahi kumtia matatani aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, baada ya kutia saini mkataba wa uchimbaji madini hotelini mjini London, ilimradi tu asikwamishe ‘mipango.’

Kashfa Buzwagi ndiyo ile iliyochangia kumtia katika msukosuko Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, ambaye mwishowe alisimamishwa kuhudhuria vikao vya mkutano wa Bunge.

Kimsingi, uzoefu unaonyesha kuwapo kwa upendeleo wa muda mrefu kwa kampuni za uchimbaji dhahabu ambao wakati mwingine hata hutishia usalama wa nyadhifa za viongozi wa serikali. Upendeleo huo ulianzia katika misamaha ya kodi ya mapato hadi katika ushuru wa mafuta ya petroli.

Soma zaidi

No comments: