Tuesday, June 2, 2009

Liyumba akwama kupata dhamana


Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba jana alikwama kupewa dhamana na mahakama katika mashitaka yake yanayomkabili ya kutumia vibaya madaraka aliyokuwa nayo na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 200.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana ilikataa kutoa dhamana hiyo kwa kutumia vivuli vya hati ya mali, baada ya kukataa ombi la utetezi la kutaka kupokewa kwa kivuli cha hati ya nyumba ya mshitakiwa yenye thamani ya Sh milioni 880 ili itumike kukidhi moja ya masharti ya dhamana. Hakimu Mkazi Nyigulila Mwaseba alikataa kutoa dhamana hiyo kutokana na ombi hilo la utetezi la kutaka kutumiwa kwa kivuli hicho kwa madai ya hati halisi iko mahakamani hapo.

"Sitoweza kutoa dhamana kwa kutumia kivuli cha hati, tena ambacho hati yake halisi ilitumika katika kesi ambayo imeshafutwa, mahakama inatakiwa kujiridhisha kabla ya kutoa dhamana,” alisema Mwaseba katika suala ambalo kama dhamana kwa mshitakiwa ilikuwa ni kutoa fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya Sh milioni 300 pamoja na kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya dhamana yenye thamani ya Sh milioni 50.

Alisema jalada la kesi hiyo limepelekwa Mahakama Kuu ambalo limehitajiwa na mamlaka za huko. Akiwasilisha maombi hayo, Wakili Majura Magafu aliitaka mahakama kupokea kivuli cha hati hiyo, kwa madai kuwa hati halisi ya kivuli hicho ilitumika katika kesi ya jinai namba 27/09, iliyokuwa ikimkabili mshitakiwa huyo ambayo imefutwa, na kwamba mpaka sasa inashikiliwa na mahakama hiyo.

Pia Magafu alisema mahakama imeendelea kushikilia hati ya kusafiria ya mshitakiwa ambayo nayo ilikabidhiwa mahakamani hapo katika kesi hiyo ya awali. Magafu alidai kuna hati iliyokabidhiwa kwa upande wa mashitaka ili kufanyiwa tathmini na mpaka walipofika mahakamani, walikuwa hawajapata taarifa yoyote kutoka kwa upande huo inayoelezea tathmini ya hati hiyo.

Soma zaidi

No comments: