Baadhi vya wabunge wamedai kuwa baadhi ya mawaziri hawana uzalendo, ndiyo maana baadhi yao wanatetea na kubeza vita dhidi ya ufisadi na wakati mwingine wanapitisha mikataba isiyo na maslahi kwa Taifa, hali inayoliingiza katika hasara kubwa.
Wakichangia hotuba ya Bajeti jana, wabunge hao walisema licha ya kuwa wataalamu nchini wana udhaifu mkubwa wa kujadiliana na kuingia mkataba na kampuni za wawekezaji, lakini kitendo cha Serikali kutochukua hatua kinaonyesha wazi kuwa kuna harufu ya ufisadi ndani ya Serikali. Mbunge wa Kishapu, Fred Mpendazoe (CCM), aliwafananisha mawaziri hao na mawe yaliyoko chini ya bahari ambayo hayawezi kusikia kilio cha mti wa mtende ulio jangwani.
Mpendazoe alihoji kama kweli Serikali iko makini kupambana na ufisadi, kwa nini wataalamu walioshiriki kuingiza nchi katika hasara kwa kuingia mikataba mibovu bado wanaendelea na kazi tena ndani ya Serikali. Alisema wakati Wizara ya Fedha inakiri kuwa Watanzania wengi wanaishi chini ya Sh 1,720 kwa siku, lakini kuna watu wachache ambao wananufaika na nchi hii na kusababisha umasikini mkubwa kwa wananchi wa kawaida.
Alitaja baadhi ya mifano ambayo wataalamu wa Serikali wameboronga kuwa ni kwenye ubinafsishaji wa mgodi wa Kiwira, Reli ya Kati, ATCL, Richmond, madini, IPTL, lakini wamekuwa wanaendelea na kazi. Mbunge huyo aliitaka Serikali isikilize kilio cha wananchi ambao wanaitaka ichukue hatua dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi. Mbunge wa Maswa, John Shibuda (CCM), alisema ukosefu wa uzalendo miongoni mwa mawaziri umekuwa chanzo cha mikataba mibovu kupitishwa na baadaye kuiweka nchi katika hali ngumu ya kiuchumi.
“Nyie mawaziri mnatupeleka wapi, si hii mikataba mibovu huwa inapitia kwenu, kama ni wazalendo kwa nini msiikatae?” alihoji Shibuda na kusema kukosekana huko kwa uzalendo ndani ya Serikali ndiko kumefanya nchi iendelee kuibiwa fedha nyingi na kampuni za uwekezaji. Mbunge huyo alisema ukosefu huo wa uzalendo ndio umekuwa kikwazo cha kukamilika kwa vitambulisho vya kitaifa, kwani kilichopo ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa sasa ni malumbano na kazi imekwama.
Alipendekeza Wakala wa Vitambulisho vya Taifa aondolewe kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani ili kuharakisha mchakato wa kutengeneza vitambulisho hivyo, viisaidie nchi kupata kodi sahihi kutoka kwa wananchi wake. Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (CCM), alisema nchi hii ni nzuri na ina raslimali nyingi ambazo zinaweza kuisaidia kuondokana na umasikini, lakini baadhi ya viongozi wanashiriki kuibomoa.
Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Mnyaa (CUF), alishangaa kuona hata Waziri wa Fedha na Uchumi na manaibu wake, hawajui jinsi rasilimali za nchi zinavyonufaisha nchi nyingine na badala yake wanatangaza mbele ya umma kuwa Serikali haina takwimu za nchi zinazonufaika. Mnyaa alitoa mifano ya namna misitu ya Tanzania inavyoinufaisha Kenya na sasa wamesitisha kuvuna misitu yao kwa kutegemea misitu ya Tanzania. Pia alitoa mfano wa Kenya inavyonunua ng’ombe Mara badala ya kununua nyama.
No comments:
Post a Comment