Tuesday, November 1, 2011

Wajasiriamali wanawake wawasaidie vijana-Waziri Simba

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Tanzania, Sophia Simba akitembelea Maonesho ya Wajasiriamali Wanawake yanayofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja leo jijini Dar es Salaam

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Tanzania, Sophia Simba amesema ushiriki wa wanawake katika shughuli za ujasiriamali nchini zimeku zikichangia kiasi kikubwa maendeleo ya nchi. Pamoja na hayo amewataka kuhakikisha wanaweka jitihada za kuwafundisha shughuli za kijasiriamali vijana ili kukabiliana na tatizo la kukosekana kwa ajira rasmi.

Waziri Simba ameyasema hay oleo ndani ya Viwanja vya Mnazi mmoja alipokuwa akifungua Maonesho ya Wajasiriamali Wanawake yanayoshirikisha wanawake wajasiriamali kutoka nchi za Kenya, Malawi na wenyeji Tanzania.

Amesema shughuli za ujasiriamali zinaweza kuwa mkombozi dhidi ya tatizo la ajira nchini, hivyo kuwataka vijana waingia na kufanya ujasiriamali kwa moyo ili kuweza kuendesha maisha yao.

“Sisi tunafanya vizuri na kunahaja ya kuwashirikisha vijana wetu nao waingie kwenye shughuli hizi (ujasiriamali)…nasema hivyo kwasababu ajira kwa sasa ni ngumu si kwa Tanzania tu bali hata kwenye mataifa makubwa ambayo yanauwezo mkubwa,” alisema Waziri Simba.

Amewataka wanawake kuendelea kuzitumia vizuri fursa zilizopo na kuacha kasumba ya kulalama kwa kila jambo; “tusiendelee kujituma peke yetu tufanye hivyo kwa vijana wetu pia ili kuweza kuwainua nao,” aliongeza waziri huyo.

Aidha ameongeza kuwa takwimu kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) zinaonekana ushiriki wa wanawake katika maonesho ya biashara ya nje ya nchi ni mkubwa ukilinganisha na wanaume, jambo ambalo linabainisha wamekuwa na mwamko na uwezo tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Alisema miaka ya nyuma walikuwa wanategemea zaidi kuongozwa na wanaume lakini kwa sasa kuna mabadiliko makubwa na wengi wanaendesha shughuli za kijasiriamali zaidi ya wanaume.

Maonesho ya Wajasiriamali Wanawake Tanzania, wameandaliwa na Tamasha la Wanawake Wajasiriamali Tanzania (MOWE) na kufadhiliwa na mashirika mbalimbali ya kimataifa na WAMA. Yanafanyika kuanzia Oktoba 30 hadi Novemba 4.

No comments: