MUSWADA wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011 unatarajiwa kusomwa bungeni kwa mara ya pili wiki ijayo na kujadiliwa kwa siku tatu mfululizo.
Pamoja na hilo, hoja binafsi za wabunge wawili wa Chadema ikiwemo ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ya kutaka kufunguliwa upya mjadala wa kuijadili kampuni ya kufua umeme ya Richmond, zipo hatihati kuwasilishwa na kujadiliwa katika vikao vya Mkutano wa Tano wa Bunge unaoendelea.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana na Ofisi ya Bunge baada ya Kamati ya Uongozi kukaa na kupanga shughuli za kuwasilishwa bungeni, Muswada huo wa Mabadiliko ya Katiba utawasilishwa Jumatatu ya wiki ijayo na kabla ya kuwasilishwa, wabunge watapewa semina juu ya muswada huo Jumamosi ya wiki hii.
Muswada huo tayari umepingwa na baadhi ya vyama vya siasa na wanaharakati wakisema una vipengele vingi vyenye utata kama Rais kupewa mamlaka makubwa na wananchi kutoshirikishwa ipasavyo kutoa maoni yao.
Endapo muswada huo utapitishwa kuwa sheria, Rais ataweza kuunda Tume ya kukusanya maoni kuhusu Katiba na kuunda Bunge la Katiba kwa madhumuni ya kutunga Katiba mpya.
Tayari Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameshasema Katiba mpya itazinduliwa wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano, Aprili 26, 2014.
Ratiba hiyo ya shughuli za Bunge inaonesha kuwa hakutakuwa na uwasilishwaji wa hoja binafsi za Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Amour Arfi (Chadema) ambaye hoja yake inahusu madhara ya uwekezaji kwenye sekta ya ardhi na madhara yake kwa wananchi huku Mnyika akitaka mjadala wa Richmond ufunguliwe upya.
Alipoulizwa Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge, John Joel kwa hoja hizo katika shughuli za Bunge hili linaloendelea, alisema; “wale wamewasilisha kusudio la kuwasilisha hoja, lakini hawakuleta hoja zao na wakileta tutayafikiria na kama itawezekana tutazipanga katika Bunge hili”.
Alipoulizwa Mnyika, alisema aliwasilisha kusudio la kuwasilisha maelezo na hoja na kufafanua: “Katibu wa Bunge anapaswa kunijibu kimaandishi kunipa nafasi ya kuwasilisha maelezo na hoja hivyo wakishanijibu nitawasilisha kwa mujibu wa barua…mimi hadi sasa sijajibiwa hivyo ipo fursa ya hoja yangu kupokelewa.”
Kwa upande wa Arfi, alisema juzi alikamilisha hoja yake na jana aliiwasilisha kwa wanasheria kurekebishwa na kufafanua; “nina uhakika kesho (leo) hoja yangu itafika ofisini kwa Katibu.”
Ijumaa ya wiki ijayo, Kamati teule ya kuchunguza sakata la kusimamishwa na kurejeshwa kazini kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo inayoongozwa na Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani itawasilisha taarifa yake na kujadiliwa na wabunge.
No comments:
Post a Comment