Tuesday, November 15, 2011

Serikali kupanga ada shule zote

KUANZIA Januari shule zote nchini zitalazimika kutoza ada mpya itakayopangwa na Serikali.

Hatua hiyo inatokana na Serikali kuahidi kabla ya mwisho wa mwezi ujao, kutoa waraka wa ada mpya za shule binafsi na za Serikali.

Kwa sasa waraka unaotumika ni namba 19 wa mwaka 2002 ambao ulipanga ada kwa shule binafsi za bweni za sekondari kuwa Sh 380,000 kwa mwaka na za kutwa Sh 150,000.

Hata hivyo, kutokana na muda mrefu kupita na mazingira kubadilika, shule hizo zimekuwa zikijipangia ada bila kufuata waraka huo.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alitoa maelezo hayo jana wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Kassim Ahmed (CUF).

Rukia alihoji sababu za Serikali kutoingilia suala hilo na kuweka viwango elekezi vya ada ili kusiwe na mkanganyiko wa kielimu.

Akijibu swali hilo, Mulugo alisema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imeandaa rasimu ya maoni kutoka kwa wadau ili wapitie na kuamua kwa pamoja juu ya viwango vya ada kwa shule zote za Serikali na za binafsi nchini.

“Wizara yangu itahakikisha viwango vya ada vitakavyowekwa vinazingitia gharama halisi ya kila mwanafunzi na kuweka uwiano katika ulipaji na utoaji ada,” alisema Mulugo.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Jakaya Kikwete, akiwa kwenye mahafali ya 11 ya shule za sekondari za FEZA, Dar es Salaam, alisema elimu ni huduma na si bidhaa ya kuuzwa kwa bei ghali, kama zinavyofanya baadhi ya shule binafsi nchini.

“Natoa mwito wa kuangalia upya mifumo yenu ya ada, ili kuwawezesha wazazi wengi zaidi kuwaleta watoto wao katika shule zetu.

Elimu ni huduma si bidhaa kama zilivyo bidhaa nyingine, ambako faida ndicho kichocheo kikubwa cha kuwekeza,” alisema Rais Kikwete katika mahafali hayo.

Kabla ya tamko hilo, Rais Kikwete wakati akikabidhi hati idhini kwa vyuo vikuu tisa nchini mwaka huu, alielezea nia yake ya kuundwa chombo maalumu cha kusimamia viwango vya ada kwa shule binafsi hadi vyuo vikuu, kwa kuwa kiasi kinacholipwa kwa sasa ni kikubwa na hakiendani na maisha halisi ya Watanzania.

Aliwataka wawekezaji katika elimu kuondoa mawazo kuwa shule ni kitega uchumi cha kuwapatia faida kwa kuwa wakifikia hatua hiyo ni hatari kwa ustawi wa nchi.

Alitoa mfano kuwa hivi sasa kuna shule za chekechea zinazotoza ada kubwa hata kuliko inayotozwa na vyuo vya elimu ya juu nchini.

“Kuna haja ya kuunda chombo kama Ewura (Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji) ambacho kazi yake itakuwa inaangalia viwango vya ada kuanzia shule za chekechekea za binafsi hadi vyuo vikuu.

“Lengo ni kuwawezesha Watanzania wengi wenye kipato cha kawaida kumudu kulipa badala ya hali ilivyo sasa ambapo watu wachache ndiyo wanaofaidi elimu hiyo,” alisema.

Hata hivyo shule nyingi za binafsi hususan zinazomilikiwa na taasisi za kidini, zimekuwa zikikubaliana na utaratibu wa ada elekezi ya Serikali, lakini mara zote zimekuwa zikilalamikia gharama za uendeshaji kuwa kubwa.

Baadhi yao zimekuwa zikiomba Serikali isaidie kuzilipia mishahara ya walimu ili zibakie na majukumu mengine ya uendeshaji ili kuwezesha kutoza ada nafuu.

No comments: