Thursday, November 3, 2011

Wanaharakati, viongozi wa dini: Wahofu Rais ajaye kuwa Dikteta

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Francis Kiwanga (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Bi. Ananilea Nkya

WAUNGANA KUMDHIBITI
VIONGOZI wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini na wanaharakati wameonya kuwa kuna kila dalili kwamba mtu atakayemrithi Rais Jakaya Kikwete atakuwa na hulka za kidikteta, hivyo wakataka Watanzania kuandaa mbinu za kumdhibiti mapema.Angalizo hilo lililotolewa na viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Chama cha Wanataaluma Katoliki (PCT), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Jumuiya ya Ahmadiya Tanzania, Makanisa ya Kipentekoste Budha na Wabahai, limekuja kipindi ambacho joto la urais wa 2015 linazidi kuongezeka.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mjadala wa siku mbili wa viongozi wa taasisi za dini nchini wakiongozwa na wanaharakati wa mabadiliko ya katiba nchini uliofanyika Dar es Salaam jana, viongozi hao walisema njia moja kuu ya kumdhibiti kiongozi wa aina hiyo ni kutungwa kwa Katiba Mpya ambayo itambana Rais kwa kupunguza mrundikano wa madaraka aliyonayo kwa sasa.

Kwa upande wa wanaharakati, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Francis Kiwanga alisema: “Rais mwingine akija, (kabla ya Katiba Mpya), hatakubali mabadiliko yafanyike. Hivyo jambo linaweza likavutwa tena kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 ijayo.”

Kiwanga ambaye alikuwa akifafanua mambo mbalimbali baada ya mada yake aliyowasilisha juu ya ukweli kuhusu mabadiliko ya katiba nchini, alisema kuna uwezekano mkubwa Rais ajaye akatumia udikteta unaotokana na katiba ya sasa kumrundikia madaraka kukwamisha mabadiliko hayo.

Alisema wanaharakati wengi wa kisiasa nchini tayari wameweka ajenda ya kuhakikisha katiba ijayo inapunguza madaraka hayo, jambo ambalo wanaamini ni mwiba mchungu kwa Rais ajaye.Katika kufanikisha mkakati huo, aliwataka viongozi hao wa dini kushiriki katika kuhamasisha mpango wa katiba mpya ili ukamilike kabla ya Uchaguzi Mkuu 2015.

Alisema uzoefu unaonyesha kuwa viongozi wengi barani Afrika huzubaisha mabadiliko ya katiba, ili kulinda maslahi yao wawapo madarakani.

Mwanaharakati mwingine, kutoka Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba alisema ni jambo la kumshukuru Mungu kwa sababu Rais Jakaya Kikwete tayari amewaahidi Watanzania kuwa Katiba Mpya, itakuwa tayari mwaka 2014.
Kibamba aliwataka viongozi hao wa dini kuongeza nguvu katika kuchochea shinikizo la mabadiliko hayo, ili yasije kukwamishwa na wanasiasa wenye uchu wa madaraka.

“Ingawa vuguvugu la kudai Katiba Mpya lilianza mara baada ya uhuru, mchakato wa maandalizi yake ulipata msukumo mpya kwa tamko la Rais kuridhia madai ya Katiba Mpya mwishoni mwa mwaka 2010,” alisema Kibamba na kuongeza:

“Kwa sababu hiyo, Watanzania wengi, akiwamo Mheshimiwa Rais (Kikwete) wamependekeza kuwa mchakato huo uchukue miaka minne, yaani kuanzia mwaka 2011 hadi 2014.”

Ingawa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikwishasema kwamba Katiba Mpya itakuwa tayari ifikapo Aprili 26, 2014, Kibamba aliwataka viongozi hao wa taasisi za dini kuongeza nguvu katika harakati hizo za katiba kutokana na ukweli kwamba wanasiasa ni vigeugeu na wanaweza kuzorotesha mchakato.

Kibamba alionyesha picha ya jumba la kifahari ambalo linamilikiwa na aliyekuwa Rais wa Misri, Hosni Mubarak kama kielelezo cha matumizi mabaya ya madaraka na ufujaji wa mali za umma.

Alisema mali za namna hiyo huwafanya viongozi kutaka kung’ang’ania madaraka au kukataa mabadiliko ya katiba, kwa kuwa wanahofia ni kuhojiwa na umma juu ya uhalali wa utajiri huo.

Alieleza mbinu nyingine ambazo zinatumiwa na viongozi kuwanyonya wananchi kuwa ni kuweka kwenye katiba vipengele ambavyo vinawalinda wasihojiwe juu ya mali na utajiri waliojipatia kwa njia zisizo halali walipokuwa madarakani.Alisema Katiba ya sasa inamrundikia Rais madaraka makubwa yakiwamo ya kuteua watu kwenye nyadhifa mbalimbali pasi na kuwapo chombo chochote cha kuhoji hata kama wanaoteuliwa wana historia chafu.

Lakini alisema yeye pamoja na wanaharakati wengine wamekusudia kuhakikisha moja ya mambo yatakayokuwapo kwenye katiba hiyo mpya ni kupunguza madaraka ya Rais.

Katika mchakato wa kuelekea kupata Katiba Mpya, Kibamba alitaja masuala muhimu yanayopigiwa debe na wanaharakati mbali na kupunguza madaraka ya Rais kuwa ni pamoja na kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi na maadili ya taifa.

Mengine ni kuruhusiwa kwa mgombea binafsi, muundo wa tawala kuanzia Serikali Kuu, Mikoa na Wilaya, suala la Muungano na adhabu ya kifo. Kibamba alisema mchakato wa Katiba Mpya ukifanikiwa, itakuwa ni mara ya kwanza kwa Watanzania kushirikishwa.

Alisema licha ya Katiba ya sasa kuwa na viraka zaidi ya 10 tangu uhuru, wananchi hawakushirikishwa na badala yake kazi hiyo ilifanywa na kikundi cha watu wachache walioteuliwa ndani ya mfumo wa chama kimoja.

Kibamba alisema hata Tume ya Jaji Kisanga ilipoishauri Serikali mwaka 1998 kuwashirikisha wananchi kwenye mabadiliko ya Katiba, ilionekana ni ushauri usiofaa.

Bunge lanyooshewa kidole
Mjadala huo pia uliligusa Bunge la 10 likidaiwa kwamba limekuwa halitekelezi kazi zake za kutunga sheria za nchi, kama katiba inavyosema.Mjumbe wa PCT, Dk Paul Shemsanga alisema uchunguzi wao umebaini kwamba Bunge limekuwa halitungi sheria, bali ni kupitisha sheria zinazotungwa na Serikali.

“Uchunguzi wetu unaonyesha kuwa Bunge halijawahi kutunga sheria. Serikali ndiyo imekuwa ikitengeneza miswada yote. Kinachofanyika ni wabunge kuhojiwa kwa kusema ndiyo au hapana, mwishowe hupitishwa kwa kauli waliosema ndiyo wameshinda kwa hivyo, umepita,” alisema Dk Shemsanga.

Akielezea juu ya malengo ya mjadala huo, Katibu wa TEC, Padre Antony Makunde alisema ni moja ya mkakati wa kuwaunganisha viongozi wa dini katika kufanikisha mpango wa kuundwa kwa Katiba Mpya nchini.

No comments: