Monday, November 7, 2011

Muswada wa Marekebisho ya Katiba ujenge Mwafaka wa Kitaifa

Na Zitto Kabwe, Mb

Kama kuna jambo moja ambalo huunganisha Taifa ni Katiba ya Taifa hilo. Katiba huweka misingi mikuu ya nchi na namna ya kujenga na kuendesha Taifa. Hivyo Katiba inapaswa kuwa ni matokeo ya mwafaka wa kitaifa kwenye masuala yote ya msingi ya nchi husika. Tanzania imekuwa ikiongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara. Kabla ya hapo kulikuwa na Katiba ya Uhuru ambayo ilitokana na Mwafaka wa wapigania Uhuru wa nchi yetu, baadaye Katiba ya Jamhuri ya Tangayika na kisha Katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kabla ya kubadili jina na kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ukiachana na Katiba ya Uhuru, Katiba nyingine zote hazikutokana na mwafaka wa kitaifa bali matakwa ya tabaka la watawala. Katiba ya kudumu ya mwaka 1977 ni zao dhahiri kabisa la utawala wa chama kimoja ambacho kilikuwa na dhamira ya kushika hatamu za uongozi. Kutokana na hali hii haikuchukua muda kwa wasomi mnamo mwaka 1983 kuanza harakati za kuifanyia mabadiliko makubwa. Mabadiliko hayo yalizaa kuwemo kwa Haki za Msingi za Binaadamu katika Katiba katika mabadiliko ya mwaka 1984, miaka saba tu toka kuandikwa kwa Katiba ya kudumu.

Takribani mwaka mzima huu kumekuwa na madai ya kuandikwa kwa Katiba mpya. Madai haya sio mapya kwani huibuka na kusinyaa kila baada ya uchaguzi Mkuu. Itakumbukwa kwamba miaka ya Tisini mwishoni kundi la vyama vya siasa liliunda Kamati ya Mabadiliko ya Katiba (KAMAKA) ili kudai kuandikwa kwa Katiba mpya. Hata hivyo safari hii sauti ya mabadiliko imekuwa ni kubwa sana kiasi cha Serikali kusikia na hivyo kupeleka Bungeni muswada wa Marejeo ya Katiba kwa lengo la kuandika Katiba mpya ya nchi yetu. Muswada huu umeleta kelele nyingi na manung’uniko mengi sana kutoka kwa makundi mbalimbali ya jamii kuanzia vyama vya siasa, viongozi wa dini na Asasi za Kijamii. Baadhi ya Asasi za Kijamii zimeunda Jukwaa la Katiba ili kuweza kuratibu vizuri juhudi za kuandikwa kwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sababu kubwa ya kupingwa kwa muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ni kwamba mchakato umewekwa kwenye Dola mno na hasa kwenye Urais. Rais anateua Tume ya kukusanya maoni, Rais anateua Bunge la Katiba nk. Watu wengi tungependa kuona mchakato unakuwa kwa wananchi zaidi. Serikali imefanya marekebisho kadhaa na kupanua wigo wa mjadala wa Katiba na pia kumhusisha kikamilifu Rais wa Zanzibar katika mchakato.

Baadhi yetu tunaona kama nafasi ya Zanzibar katika mchakato imepewa nguvu kubwa kupita kiasi. Ninadhani Zanzibar inastahili kupata nafasi hii katika mchakato wa Katiba. Jambo ambalo ni vizuri tulitilie maanani ni kwamba Muungano wa Mwaka 1964 ulihusisha nchi mbili huru zenye hadhi sawa mbele ya sheria za kimataifa. Linapokuja suala la kuandika Katiba ya Muungano, pande mbili za Muungano zinakuwa na hadhi sawasawa. Kwamba Zanzibar ishiriki kwenye masuala ya Muungano tu ni hoja inayojadilika iwapo tu Katiba ya Muungano ingetofautisha kinagaubaga taasisi za kimuungano na zisizo. Kwa mfano Sura ya Bunge katika Katiba ni lazima ijadiliwe na pande zote mbili ingawa Bunge wakati mwingine hupitisha miswaada ambayo sio ya masuala ya Muungano. Aina ya Muungano wetu inatulazimisha kufanya hivi tunavyofanya sasa. Mkataba wa Muungano ni lazima uheshimiwe kama ulivyo sasa.

Katiba mpya yaweza kuweka makubaliano mapya lakini muswada wa sasa ni lazima utambue nafasi halali ya Zanzibar kwa mujibu wa Katiba ya sasa na Hati za Muugano. Suala hili ni suala la kisheria na sio suala la idadi ya watu au ukubwa wa eneo la nchi husika. Nchi ya Ushelisheli yenye watu 80,000 ina nafasi sawa na Tanzania yenye watu 42 milioni katika SADC, AU na UNO. Zote zina kura moja tu. Huu ndio ukweli na hatuna budi kukubaliana nao.

Muswada unampa mamlaka Rais wa Tanzania na Rais wa Zanzibar kuteua Tume ya Katiba. Tume hii maRais hawatapata ushauri wa mtu mwingine yeyote kwa mujibu wa kifungu cha (6) na vifungu vidogo (1), (2) na (3). Wanasiasa wakiwemo Wabunge, Wawakilishi, viongozi wa vyama wa Ngazi za Taifa, Mkoa au Wilaya hawatakuwa na sifa za kuteuliwa.

Inawezekana kabisa waandishi wa muswada walikuwa na mantiki ya kuuondoa mchakato kwenye mikono ya wanasiasa. Nia hii njema haikufikiriwa vizuri hata kidogo. Njia hii haijengi mwafaka. Tume hii sio ya Wataalamu, ni Tume inayopaswa kuwa na sura ya kitaifa. Nafasi ya wanasiasa katika mchakato wa kukusanya maoni ni muhimu sana katika kuhalalisha mchakato wenyewe. Tume lazima ionekane ni Tume ya Taifa na sio Tume ya maRais. Hivyo kipengele hiki cha kuwanyima sifa wanasiasa kinapaswa kufutwa katika muswada. Wabunge na Wawakilishi kwa kuwa ni sehemu ya Bunge la Katiba wasiwemo katika Tume, lakini viongozi wengine wa kisiasa wawe na haki ya kuteuliwa kuwa wajumbe.

Lakini pia Rais ateue Tume kutokana na maoni kutoka katika makundi yenye maslahi ya karibu na Katiba ya nchi na hivi ni vyama vya siasa. Ninapendekeza kwamba katika Wajumbe 30 wa Tume ya kukusanya maoni ya Katiba, 10 watokane na vyama vya siasa vyenye Wabunge kwa uwiano wa CCM 2, CHADEMA 2, CUF 2, NCCR 2, TLP 1 na UDP 1. Kila chama cha siasa chenye Wabunge kupitia kiongozi wake Bungeni kipeleke majina ya watu wanaowapendekeza kuwa katika Tume ya Katiba na kutokana na Mapendekezo hayo Rais atawateua kuwa wajumbe. Masharti mengine ya nusu kutoka kila upande wa Muungano yazingatiwe.

Muswada unapendekeza kuwepo kwa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume. Kifungu cha cha 7 kifungu kidogo (1), (2) na (3) kinaweka utaratibu wa kupatikana kwa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume. Muswada unasema UTEUZI wa Mwenyekiti na Makamu utazingatia kwamba mmoja atoke uapnde mmoja wa Muungano na mwingine upande wa Pili wa Muungano. Ingawa Muswada hausemi waziwazi lakini ni dhahiri kwamba Mwenyekiti wa Tume atateuliwa na Rais baada ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar. Sitaki kujenga hoja kwamba Mwenyekiti na Makamu wachaguliwe na wajumbe wa Tume kutoka miongoni mwao lakini ni dhahiri Mwenyekiti wa Tume anapaswa kuwa mtu mwenye heshima kubwa hapa nchini. Ningependekeza kwamba maRais wateue Wenyeviti wenza badala ya Mwenyekiti na Makamu wake ili kuweka nafasi sawa kwa pande mbili za Muungano. Hapa nchini tunao Watanzania ambao wamefanya kazi iliyotukuka katika nyadhifa mbalimbali na sasa ni wastaafu wasio na nia yeyote ya madaraka ya kisiasa wanaoweza kuongoza vizuri kabisa Tume hii. Ni pendekezo langu kwamba Dkt. Salim Ahmed Salim na Jaji Joseph Sinde Warioba wawe wenyeviti wenza wa Tume ya Katiba. Uzoefu wao katika uongozi na kuijua kwao nchi kutasaidia sana kuhakikisha kwamba mchakato wa kukusanya maoni na kisha kuandika Katiba unakuwa na mafanikio kwa kuzingatia misingi ya Taifa letu.

Muswada unapendekeza kwamba Hadidu rejea za Tume zitolewe na maRais. Kifungu cha nane na muswada kuhusu hadidu rejea nadhani hakina mantiki sana. Madhumuni ya muswada yanasema pamoja na mambo mengine muswada unaweka masharti kuhusu Hadidu rejea za Tume. Wakati huo huo muswada unasema Hadidu rejea zitakuwa ni hati ya kisheria itakayozingatiwa na Tume katika kazi zake.

Mantiki ni kwamba Hadidu rejea zinapaswa kuwa sehemu ya Muswada kama ‘schedule’ ili kuzipa nguvu ya kisheria badala ya tangazo katika gazeti la Serikali. Hadidu rejea zikiwa ni sehemu ya Muswada zitajadiliwa na Bunge na kupitishwa hivyo kuwa ni jambo ambalo limefikiwa kwa mwafaka wa wawakilishi wa wananchi.

Muswada unataka uamuzi wa kura ya maoni kuhusu Katiba uwe ni kukubaliwa na nusu ya Watanzania katika kila upande wa Muungano. Nadhani hapa tunacheza na Katiba ya nchi. Katiba ya nchi inapaswa kukubaliwa na theluthi mbili ya wapiga kura wa pande zote za Muungano yaani kila upande theluthi mbili. Hii itaipa Katiba ‘legitimacy’ na hivyo kuheshimiwa na wananchi na watawala. Kuna woga gani uliopo kutaka katika ikubalike na nusu ya wapiga kura? Mifano ya nchi nyingi duniani Katiba inapaswa kukubaliwa na theluthi mbili ya wapiga kura. Hata jirani zetu wa Kenya ilikuwa hivyo na hata kura ya maoni kuhusu mwafaka huko Zanzibar ilikuwa hivyo. Kwa kuwa Katiba ni chombo cha mwafaka wa kitaifa, muswada utamke kwamba Katiba mpya itakuwa imepita iwapo theluthi mbili ya wapiga kura watapiga kura ya ndio.

Mwisho

Zitto Kabwe ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu CHADEMA. Maoni haya ni maoni binafsi ya Zitto na kwa vyovyote vile hayawakilishi msimamo rasmi wa CHADEMA au Kambi ya Upinzani Bungeni.

No comments: