Monday, November 21, 2011

Wafungwa wanawake wapewa msaada

KIKUNDI cha Kinamama cha WINA cha Mwanza, kimetoa msaada wa vitu mbalimbali vikiwemo vyakula kwa wafungwa wanawake wa Gereza la Butimba pamoja na vituo vya watoto
wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Msaada huo wenye thamani ya Sh milioni mbili, waliutoa jana baada ya kutembelea Gereza la Butimba lililopo jijini hapa na kuzungumza na wanawake waliofungwa kwa makosa mbalimbali.

Misaada hiyo pia iliwanufaisha kituo cha watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu cha Tanzania Children Rescue Centre (TCRC) kilichopo Nyasaka na Kituo cha Maisha ya Kristo na huduma zake kilichopo Kiloleli.

Akizungumza baada ya kusambaza misaada hiyo, Mwenyekiti wa Kikundi cha WINA, Anna Mukasa alisema kwa kuwa wao ni watumishi wameona ni vyema kurudisha kile kidogo wanachopata kwa jamii hasa watoto ambao wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu.

Msaada uliotolewa katika gereza la Butimba pamoja na vituo hivyo ni mchele, sembe, sukari, chumvi, mboga, matunda, biskuti, juisi, sabuni, mafuta ya kupaka na kupikia, viatu, ngano pamoja na mashuka.

Naye Mchungaji Mika Ngusa wa Kituo cha kulelea watoto cha TCRC aliwashukuru kinamama hao na kusema kuwa Watanzania sasa wameanza kuwa na mwamko wa kusaidia watoto wao.

Alisema kituo hicho chenye watoto 86, kilianzishwa mwaka 1997 kikiwa na lengo la kuwasaidia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na kwamba tayari watoto wawili
wamejiunga na vyuo vikuu huku wengine wakisoma sekondari na shule za msingi.

No comments: