MBUNGE wa Viti Maalum, Diana Chilolo (CCM) ameitaka serikali kuorodhesha ahadi zote alizowahi kutoa Rais Jakaya Kikwete na kutoa tarehe ya kuzitekeleza.
Chilolo alitoa maelezo hayo katika swali la nyongeza alipohoji kama serikali haioni umefika wakati kutekeleza hilo ili kuondoa kero wanazopata wabunge kushindwa kujibu utekelezaji wa ahadi hizo wanapoulizwa na wananchi.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisema: “Hatuwezi kuweka tarehe ya kila ahadi ila ratiba ni kwamba ahadi zote zitatekelezwa ndani ya miaka mitano”.
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa (CCM) aliyetaka kufahamu wizara zinazoratibu utekelezaji wa ahadi za Rais, Lukuvi alisema ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo yenye jukumu la kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa ahadi hizo zinapotolewa kwa wananchi kila anapofanya ziara ya kikazi mikoani.
Alisema baadhi ya ahadi ni pamoja na zinashughulikiwa na kuratibiwa na Ofisi ya Rais yenyewe na zile zinazohitaji bajeti kuwekwa kwenye mipango ya Wizara au mikoa husika kutegemea na aina ya ahadi.
Alisema Ofisi ya Waziri Mkuu inafuatilia ahadi hizo ambazo hutolewa katika wizara na mikoa na huchapisha kamusi maalumu ili iwe rahisi kwa ufuatiliaji.
“Wizara na mikoa huwasilisha ofisi ya Waziri Mkuu taarifa ya utekelezaji wa ahadi hizo…ahadi zote za rais zimerekodiwa na nyingi zilitolewa mwaka jana hivyo zitatekelezwa ndani ya miaka mitano ya kipindi chake cha uongozi,” alisema.
No comments:
Post a Comment