Monday, November 28, 2011

Msichana ajinyonga akibisha kupika chakula

MWANAFUNZI wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Mbezi Juu, Kinondoni mkoani Dar es Salaam, amejinyonga kwa kutumia kitenge baada ya kubishana na kaka yake kuhusu nani apike chakula cha mchana.

Mwanafunzi huyo wa kike mwenye amri wa miaka 11 (jina limehifadhiwa), alikutwa amejinyonga chumbani kwake juzi akiwa amejitundika kwa kutumia kitenge kilichofungwa katika nondo ya dirisha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema jana kuwa msichana huyo kabla ya kuchukua uamuzi huo, alibishana na kaka yake mwenye umri wa miaka 12 (jina limehifadhiwa) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo.

Alisema inavyoonekana, msichana huyo alichukua uamuzi huo baada ya kugombana kuhusu nani apike chakula cha mchana kwa kuwa baada ya ugomvi, aliingia ndani ya chumba chake
na ndipo baadaye mwili wake ukakutwa ukining’inia.

Katika tukio lingine, mfanyabiashara Ahmed Mguni (27), mkazi wa Mbagala Charambe amekutwa juzi amekufa na mwili wake umelala kitandani bila jeraha lolote.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime alisema sababu ya kifo chake haijafahamika na kwamba Polisi wanaendelea na uchunguzi huku mwili wake ukiwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Temeke.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile alisema Polisi inamtafuta dereva
na gari lililomgonga fundi ujenzi aliyetambuliwa kwa jina moja la James (35) na kufa papo hapo.

Shilogile alisema fundi huyo aliyekuwa akitembea kwa miguu aligongwa na gari juzi asubuhi
katika eneo la Mvuti kwenye barabara ya kwenda Msongola.

No comments: