POLISI wilayani Mpanda, Rukwa, inamshikilia Seif Aldi (41) raia wa Oman ambaye ni mwekezaji wa kampuni ya madini ya Kapufi Katavi Gold Mine, kwa tuhuma za kufunga ndoa na mwanafunzi wa kidato cha pili.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Isuto Mantage, alisema jana kuwa, Seif alikamatwa Jumapili saa 2.30 usiku katika sherehe ya harusi yake kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu Huria mjini humo.
Mtuhumiwa anadaiwa kufunga ndoa ya Kiislamu na mwanafunzi huyo Jumapili saa 1.30 usiku katika Msikiti wa Madukani, ndoa ambayo ilifungishwa na Shehe wa Msikiti huo aliyemtaja kwa jina moja la Shehe Idd.
Alisema Jeshi hilo lilipata taarifa ya mpango wa maandalizi ya kumwoza mwanafunzi huyo wa kidato cha pili katika Sekondari ya Rugwa huku wazazi wa mtoto wakijua kuwa bado ni mwanafunzi.
Kamanda Mantage alisema Polisi iliandaa mtego wa kumkamata Jumamosi kwenye sherehe ya kumfunda mwanafunzi huyo maarufu kama ‘kitchen party’.
“Lakini askari Polisi siku hiyo hawakumkamata mtuhumiwa kutokana na washiriki wa sherehe hiyo kuwa wa jinsia moja ya kike,” alisema Kamanda Mantage.
Siku iliyofuata kwa mujibu wa Kamanda Mantage, polisi walimkamata baada ya ndoa kufungwa.
Alisema polisi wakiongozwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mpanda (OCD), Joseph Myovela, walifuatilia msafara wa harusi mpaka kwenye ukumbi ilimokuwa sherehe ya wana ndoa hao.
Baada ya maharusi kuingia ukumbini na ratiba kufuatwa kwa muda, timu hiyo ya askari iliwaweka chini ya ulinzi Seif na bibi harusi (mwanafunzi) na kuwachukua hadi Kituo cha Polisi mjini Mpanda kwa mahojiano.
Wakati wa kuwaweka chini ya ulinzi, Kamanda Mantage alisema ratiba ilishafikia waalikwa kutoa zawadi, ikabidi shughuli hiyo isimamishwe na waalikwa kusambaa na zawadi zao na kurejea makwao.
No comments:
Post a Comment