Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Bi. Ananilea Nkya leo Dar es Salaam. Amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikiongezeka kwa kasi Zanzibar ambapo vinaleta athari kubwa za kimwili na kisaikolojia kwa waathirika na ni kesi chache ndizo zinazoripotiwa na kutolewa hukumu inayostahiki.
Akifafanua juu ya mafunzo hayo amesema waandishi wa habari wataelimishwa sheria zinazohusiana na ukatili wa kijinsia pamoja na mapungufu yake zikiwemo sheria za makosa ya jinai ya 2004, sheria ya taratibu za uhalifu, sheria ya Mahakama ya Kadhi ya 1985, sheria ya wari na uhifadhi wa watoto wa mzazi mmoja ya 2005.
Sheria hizo zimeundwa katika muda tofauti ili kupambana na vitendo vya ukatili ambapo bado hazifahamiki vyema kwa wadau mbalimbali wakimemo wanahabari. Wanahabari pia wataelewa hali halisi ya vitendo vya ukatili na kujifunza mbinu bora za kuripoti vitendo hivyo ili mabadiliko yaweze kupatikana.
“Vitendo vya ukatili wa kijinsia vilivyoshamiri Zanzibar ni pamoja na ubakaji, ndoa za kulazimisha, mimba za utotoni, vipigo kwa wanawake, utelekezaji wa wanawake na watoto, upigaji na wanawake kunyimwa fursa za kushiriki katika shughuli za kimaendeleo,” alisema Nkya.
Aidha ameongeza kuwa wanaharakati wanaeleza kuwa vitendo hivyo vinaongezeka kwa kasi kutokana na usiri wa jamii kuripoti kesi hizo pamoja na taasisi zinazohusika kutokuchukua hatua zinazostahili kwa wakati muafaka.
Kwa mujibu ya utafiti wa ukatili dhidi ya watoto (VAC), 2011 asilimia 66.5 ya wanawake na wanaume walifanyiwa ukatili wa kimwili kabla ya kufikisha miaka 18 na kwamba asilimia 50.6 ya wanawake waliofanyiwa ukatili wa kijinsia wakiwa wadogo walipata mfadhaiko baada ya siku 30.
TAMWA imeandaa mafunzo hayo kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya idadi ya watu (UNFPA) kama sehemu ya shughuli za pamoja za Umoja wa Mataifa.
No comments:
Post a Comment