Friday, November 18, 2011

Mbunge- Ujerumani inafadhili wapinzani

UJERUMANI imetajwa bungeni kukitumia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupinga kusomwa kwa mara ya pili Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011.

Tuhuma hizo zilitolewa na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), wakati akichangia muswada huo uliojadiliwa kwa siku ya tatu sasa na unaotarajiwa kuhitimishwa leo.

Wakati Lusinde akitoa tuhuma hizo, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amewataka Watanzania kutatua matatizo yao bila ya kukimbilia kwa mabalozi na kuonya kuwa vinginevyo watakuwa wakiendekeza ukoloni mamboleo.

Lusinde katika madai hayo, aliweka bayana kuwa Ujerumani imewachochea wapinzani na wanaharakati kufanya vurugu na imewaahidi fedha ikiwa watafanikisha muswada huo usomwe mara ya kwanza bungeni.

“Ujerumani wanawasaidia hawa wanaopinga muswada huu, wamewaahidi fedha kama muswada utasomwa kwa mara ya kwanza…kuna watu wanafanya udalali wa kisiasa hapa,” alisema mwanasiasa huyo kijana.

Katika mjadala wa muswada, Chadema na NCCR Mageuzi wamesusia majadiliano ya muswada huo baada ya kuwasilisha maoni ya Kamati yao ya Upinzani iliyowasilishwa na Mbunge wa Iramba Mashariki, Tundu Lissu.

Akijibu tuhuma hizo, Katibu wa Wabunge wa Chadema, John Mnyika alisema; “hizo ni taarifa za uzushi, propaganda zenye lengo la kuwapotosha Watanzania, sisi tunapinga kusomwa mara ya pili kwa sababu wananchi wanapinga hivyo.”

Gazeti hili lilipomuuliza Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) kuhusu tuhuma hizo zilizotolewa na Lusinde, alisema taarifa hizo za kuahidiwa fedha si za kweli.

“Mataifa ya Ulaya ndiyo yanafaidika na sera za CCM kuliko upinzani, haiwezekani leo watufadhili sisi kuiondoa Serikali ya CCM inayowasaidia wao kama kwenye madini,” alidai Kafulila na kuungwa mkono na mwenzake wa Kasulu Mjini, Moses Machali aliyesema; “Lusinde ni mpigadebe wa CCM, hatunyimi usingizi.”

Lusinde pia alisema kutokana na kauli za Chadema, inaonesha Wazanzibari walioko kwenye chama hicho wanajipendekeza na wanadharauliwa na hawatakiwi.

Kuhusu kauli ya Chadema kuwa Rais wa sasa ni wa kifalme, Lusinde alisema: “Chadema ni chama cha wabinafsi na wanaweka viongozi kwa unasaba.

“Angalieni humu bungeni kuna mtu na mkwewe na mwanawe, yupo mwingine na dada yake na yupo aliyemuweka mzazi mwenzake, sasa nani anayefuata uongozi wa kifalme, sisi au wao?” alihoji.

Kwa upande wa Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jason Rweikiza (CCM), alishauri muswada huo uondoe kipengele cha kuundwa kwa Bunge la Katiba na ibaki Tume ya kukusanya maoni pekee ili kupunguza gharama kubwa pamoja na kuepusha usumbufu wa kisiasa.

“Katika demokrasia kuna uwakilishi wa moja kwa moja na kupitia uwakilishi sasa tume ingechukua maoni na kuandaa rasimu na kuirudisha kwa wananchi. Kuondolewe Bunge la Katiba ambalo linakuwa la uwakilishi, duniani kote wanachagua njia moja, lakini sisi tunataka kuchukua njia zote mbili hii haina maana,” alisema.

Mbunge huyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alipendekeza jina la muswada libadilishwe kutoka Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kuwa Muswada wa Kutunga Katiba mpya, kutokana na kwamba Katiba inaandikwa upya na haifanyiwi mabadiliko ya vipengele vya sasa.

Mbunge wa Tumbe, Rashid Ali Abdalla (CUF), alitaka Watanzania waliopo nje waangaliwe namna ya kuwasilisha maoni yao kwa Tume itakayoundwa kukusanya maoni.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Clara Mwatuka (CUF), aliwataka wabunge wenzake kuachana na kujadili kauli ya Chadema na badala yake kuujadili muswada huo.

“Tusiwapuuze (Chadema) katika waliyosema yapo mengine machache mazuri tuyachukue kuyafanyia kazi,” alisema Mwatuka.

Waziri Mkuu mstafu, Warioba, alisema Watanzania lazima wajitathimini wenyewe kujiletea maendeleo yao na kutatua matatizo bila ya kukimbilia kwa mabalozi na kuonya kuwa vinginevyo watakuwa wakiendekeza ukoloni mamboleo.

Alisema hayo jana katika warsha ya kumuenzi Baba wa Taifa, Malimu Julius Nyerere, iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro inayojulikana kama ‘Mzumbe Nyerere Day’.

“Inasikitisha kuona tumepoteza maadili na nidhamu yetu ambayo Baba wa Taifa alituachia kama tunu na sasa mtu anatafuta uongozi ili kujipatia mali,” alisema Jaji Warioba.

Alisema wanasiasa wana wajibu wa kukaa pamoja na kuondoa tofauti zinazoendelea hivi sasa nchini, ili kutoa fursa kwa Taifa kufanya shughuli zake.

Warioba alisema siku hizi hajui nchi inakwenda wapi kwa sababu watu wamepoteza imani ya nchi na kila mtu analalamika, kiongozi analalamika na wananchi wanalalamika.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Joseph Kuzilwa alisema chuo chake kinaandaa kila mwaka kumbukumbu ya kumuenzi Baba wa Taifa kwa yale aliyoyafanya ili yaweze kukumbukwa na vizazi vya sasa na vya badaye na kuwa chachu ya maendeleo.

“Leo hii ni siku ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambaye alitumikia Taifa kwa uadilifu na alipenda Taifa lake liwe na wasomi wa ngazi mbalimbali ikiwemo ya elimu ya juu ili kuwa nguzo ya maendeleo ya nchi,” alisema Profesa Kuzilwa.

No comments: