Monday, November 21, 2011

Wanawake wahamasika kiuchumi

WANAWAKE 750 kisiwani Pemba wameanzisha vikundi vyao vya kujikwamua kijamii na kiuchumi baada ya kuhamasika kutokana na jinsi wanawake wenzao walionufaika na mradi wa Kuwezesha Wanawake Zanzibar (WEZA).

Ofisa Mwezeshaji wa Mambo ya Kijamii Pemba, Zuwena Khamis Omar alisema wanawake hao wamelazimika kuunda vikundi vyao wenyewe kwa vile WEZA ilishafikisha lengo lake la kuwa na wanachama 7,842.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania
(TAMWA), wanawake hao 750 wameanzisha vikundi hivyo mwaka jana baada ya kuona mabadiliko makubwa kiuchumi na kijamii waliyopata wanawake walinufaika na mradi
wa WEZA ambao umeendeshwa kwa miaka minne na unamalizika mwezi ujao.

Maeneo hayo na idadi ya vikundi kwenye mabano ni Shumba mjini (4), Kiuyu mbuyuni (2), Kisiwani (2), Mtambwe Kaskazini (3), Shumba viamboni (1), Mjini Ole (3), Kiungoni (3),
Mgogoni (2), Shengejuu (3) na Piki (2).

Mratibu wa Shehia ya Mtambwe Kaskazini, Khadija Omar Kibano alisema wanawake wengi wamekuwa na hamu ya kujiunga na vikundi vya uzalishaji baada ya kuona wanawake
wenzao waliopata mafunzo kutoka WEZA wamemudu kufanya biashara kwa mafanikio na kushiriki harakati za maendeleo.

Mradi wa WEZA unaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Care Tanzania na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) na kufadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Austria pamoja na Care Austria.

No comments: