IDADI ndogo ya wanawake wanaomaliza mafunzo ya udaktari katika vyuo vikuu inatokana na msingi mbovu uliojengwa kwenye shule za msingi, sekondari na hofu waliyonayo katika masomo ya Sayansi.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Katoliki cha Sayansi za Afya (CUHAS)-Bugando, Profesa Jacob Mtabaji alisema hayo wakati akizungumzia mahafali ya nne ya chuo hicho ambayo
yatafanyika chini ya Chuo Kikuu cha Saint August (SAUT).
Alisema wanawake wamekuwa wakipewa upendeleo kwenye usajili na tegemeo la chuo ni
kupata angalau asilimia 30 ya wanawake kila mwaka.
“Wanaofanya vizuri zaidi kwenye masomo ya udaktari ni wanawake lakini uchache wao unatokana na msingi wa chini pamoja na hofu ya masomo ya sayansi…sio tatizo la sasa ni la zamani licha ya kutoa upendeleo,” alisema Makamu Mkuu wa Chuo.
Alisema kwa mara ya kwanza katika mahafali hayo kutakuwa na mwanafunzi mmoja anayefuzu shahada ya uzamivu yaani PhD ambaye ni Dk. Stephen Mshana.
Alisema wanaohitimu kwa mwaka huu ni wanafunzi 149 wakiwemo wanawake 50 na wanaume 99 wa fani mbalimbali ikiwemo Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Afya ya Jamii waliyoiandaa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Calgary huko Canada.
Profesa Mtabaji alisema idadi hiyo ya wahitimu, inafanya chuo hicho kifikishe wahitimu 555 tangu kilipoanzishwa wakiwemo wanawake 216 na wanaume 340.
Mahafali hayo yatatanguliwa na kongamano la kitaaluma litakalozungumzia changamoto za mafunzo ya udaktari ikiwemo mchango na mtazamo wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika kufundisha madaktari.
No comments:
Post a Comment