CHAMA cha Wanasheria wa Tanzania Bara (TLS) kimetaka uwasilishaji wa muswada wa katiba mpya usitishwe, kwa sababu mbalimbali.
TLS pia imependekeza Rais Jakaya Kikwete asiridhie sheria itakayopitishwa, endapo Bunge litaruhusu kusomwa kwa muswada huo kwa mara hiyo ya pili na ya tatu, ili kuhifadhi utawala wa sheria.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa TLS, Francis Stolla alisema pamoja na kuufanyia marekebisho kadhaa, kwa kuzingatia matakwa ya wananchi na wadau mbalimbali, kuuwasilisha bungeni bila kuwarejeshea ili wajiridhishe na marekebisho yaliyofanywa ni sawa na kazi bure.
“Tunakubaliana na marekebisho mengi yaliyofanywa katika muswada huo, kama kuandikwa kwa rasimu ya Kiswahili, lakini tumeona kuwa shauku ya Watanzania ya kutaka kuiona rasimu hiyo na kuchangia kwa upana zaidi imekatwa kutokana na utaratibu wa kuipeleka bungeni ili isomwe kwa mara ya pili na ya tatu.
“TLS inaamini kuwa rasimu hiyo ya Kiswahili ingetoa nafasi nzuri kwa wengi kuielewa vizuri na kutoa michango yao itakayoifanya isihitaji marekebisho baada ya muda mfupi wa matumizi, kwa kuwa watakuwa wameainisha wayatakayo wenyewe wakiwa na uelewa wa kila jambo kwa lugha yao ya Taifa,” alisema Stolla.
Kwa maelezo yake, kutokana na utaratibu huo wa kuusoma bungeni kwa mara ya pili, nafasi ya wananchi katika kuujadili ndio haipo tena, labda kama Rais ataafikiana na wao kwa kutoridhia sheria itakayopitishwa.
Stolla pia alionya kuwa endapo Katiba inayotumika sasa haitarekebishwa kwanza kuruhusu au kuelekeza namna Katiba mpya itakavyopatikana, haitakuwa halali.
“Huo ndio ukweli na itakuwa ni ukiukwaji wa sheria endapo itaandikwa mpya kabla ya iliyopo kurekebishwa. Hadi sasa hakuna marekebisho yaliyopitishwa tayari, na muswada haupendekezi marekebisho hayo,” aliongeza.
No comments:
Post a Comment