Wednesday, November 23, 2011

Kikwete awakaribisha Chadema Ikulu

RAIS Jakaya Kikwete amekubali kukutana na kuzungumza na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) juu ya Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011, Ikulu imetangaza.

Katika taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu kutoka Dodoma jana jioni,ilieleza, kwamba “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea barua ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kuomba viongozi wa chama hicho kukutana na Mheshimiwa Rais kuzungumzia Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011.

“Mheshimiwa Rais Kikwete amelipokea ombi hilo kwa furaha kwa sababu ni jambo jema.”

Kutokana na kukubaliwa kwa ombi hilo, Ikulu ilieleza kwamba “Rais ameagiza mawasiliano yafanyike ili kupanga tarehe mwafaka ya kukutana na viongozi hao wa CHADEMA na
kuzungumzia suala hilo.”

Majibu hayo ya Rais Kikwete yamekuja siku moja baada ya Chadema kupitia kwa Mwenyekiti wake wa Taifa, Freeman Mbowe, kutangaza kuundwa kwa Kamati ndogo ya chama hicho kwenda kumuona Rais kumuelezea msimamo wao kuhusu mchakato wa Katiba mpya.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa alililiambia gazeti hili jana alasiri kwamba tayari walipeleka barua hiyo Ikulu, Dar es Salaam jana mchana, kuomba kukutana na Rais
Kikwete na wanasubiri jibu kulingana na nafasi ya karibu ya Rais kama walivyoeleza katika barua yao.

“Barua imepelekwa Ikulu leo (jana) na kwa nafasi ya Rais atakayoona ya mapema kwa suala hilo tutakutana naye, tutazungumzia mambo mbalimbali, lakini la msingi kabisa ni mchakato
wa Katiba mpya kama tulivyoeleza tulipozungumza na vyombo vya habari juzi (Jumatatu),” alisema Dk. Slaa.

Katika mkutano huo na waandishi Jumatatu wiki hii, Mbowe akitoa maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutana Jumapili Dar es Salaam,alisema waliunda Kamati ndogo ya
kwenda kumwona Rais Kikwete kumweleza msimamo wao kuhusu mchakato wa Katiba mpya.

Mbowe alisema hatua hiyo imetokana na kutoridhika na Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 uliopitishwa Ijumaa iliyopita na Bunge, Dodoma, bila ushiriki
wa wabunge wa Chadema na NCCRMageuzi, waliosusa na kutoka nje.

Miongoni mwa madai yaliyosababisha wasusie mjadala huo ni kuwa Muswada ulikuwa na upungufu na marekebisho mengi yaliyosababisha wao kuona ni bora usomwe mara ya
kwanza na kurudi kwa wadau wakiwamo wananchi ili watoe maoni kabla ya kusomwa mara ya pili.

Muswada huo uliotolewa kwa Hati ya Dharura, ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni Aprili na kupelekwa kwa wadau na kufanyiwa marekebisho kadhaa, ikiwemo kuuweka katika
lugha ya Kiswahili na kisha kusomwa kwa mara ya pili katika Bunge lililomalizika Ijumaa ulipitishwa na kusubiri kusainiwa na Rais ili kuwa sheria.

Wajumbe wa Kamati hiyo ya watu saba ni viongozi wa juu wa Chadema na baadhi ya wabunge wa chama hicho wakiongozwa na Mwenyekiti Mbowe (Mbunge wa Hai na Kiongozi
wa Kambi ya Upinzani Bungeni), Makamu Mwenyekiti Bara na Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa Mohammed.

Wamo pia Katibu Mkuu, Dk. Slaa, Mwanasheria wa Chama na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, wajumbe wawili wa Kamati Kuu ya Chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu
na Profesa Abdallah Safari.

Naye Lucy Lyatuu anaripoti kwamba Jukwaa la Katiba nchini limesema Jumamosi litafanya maandamano ya amani nchi nzima yenye lengo la kumwomba Rais Jakaya Kikwete,
asisaini Muswada wa Sheria wa Mabadiliko ya Katiba 2011.

Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deus Kibamba, alisema hayo jana Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari, akitoa msimamo wa Jukwaa kuhusu Muswada huo.

Alisema wanamwomba Rais asiusaini kwa kuwa wananchi wengi watakosa fursa ya kushiriki mchakato kuanzia hatua ya msingi na hivyo kujenga chuki baina ya Serikali na wananchi.

“Maandamano haya yatafanyika nchi nzima katika maeneo mbalimbali na kwa Dar es Salaam yataanzia viwanja vya Mnazi Mmoja kuelekea Jangwani,” alisema Kibamba.

Alisema kwa kutousaini, Rais atakuwa amelinda Katiba ya sasa ambayo inatambua kuwa wananchi ndiyo wenye mamlaka ya mwisho juu ya jambo lolote linalohusu maslahi yao na
Taifa lao.

Kuhusu kibali cha maandamano, Kibamba alisema yameandaliwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi, ambayo inalinda Watanzania katika kutoa maoni, kwani Ibara ya 18 hadi 22 inatamka
kuwa kila raia ana haki ya kutoa maoni na ya kukusanyika.

Alisema Jukwaa hilo limepeleka barua kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) likimtaarifu kuhusu maandamano hayo ya amani na kushauri kuwa ili yafanikiwe ni vema askari watakaokuwapo wavae kiraia ili wasitishe wananchi na kusababisha vurugu.

Alipoulizwa kama ana taarifa na barua ya Jukwaa la Katiba, Kamishna wa Polisi wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, alisema Jeshi hilo halijapata barua yoyote kutoka kwa Jukwaa hilo inayoelezea maandamano hayo na kwamba litasimamia utekelezaji wa kanuni na taratibu zilizopo.

Kuhusu Muswada huo, Kibamba alisema Jukwaa linalaani maelezo yasiyokuwa na ukweli yaliyotolewa na baadhi ya wabunge na viongozi wa Serikali dhidi yao kwamba kauli zilizotolewa kwa nyakati tofauti na Jukwaa zimeupotosha umma kwa kutaka Muswada huo usomwe mara ya kwanza na si mara ya pili.

Hata hivyo alisema Jukwaa litaendelea kusema ukweli kwamba Muswada haukupaswa kusomwa kwa mara ya pili bungeni kabla ya kufikishwa kwa wananchi vijijini na mijini.

Wiki iliyopita, Rais Kikwete akizungumza na wazee wa Dar es Salaam, alisema Muswada huo
haukuondolewa bungeni, hivyo kutokana na hilo, hapakuwa na sababu ya kurudia kusomwa mara ya kwanza kwa mujibu wa taratibu za Bunge.

Alisema baada ya Muswada kupitishwa na Bunge, utawasilishwa kwake ili kusainiwa uwe sheria na baada ya hapo itabaki kazi yake na Rais wa Zanzibar kuunda Tume, ili mapema
mwakani kazi ya kukusanya maoni ya wananchi ianze.

Alisema lengo ni kuwa ifikapo mwaka 2014 kazi iwe imekamilika ili mwaka 2015 Uchaguzi Mkuu ufanyike chini ya Katiba mpya na kuwasihi Watanzania kujiandaa kutoa maoni
kwenye Tume ya Katiba mara itakapoanza kazi.

Rais alisema njia ya maandamano na vurugu si ya busara kwani haijengi bali inabomoa, haina faida bali hasara nyingi, haina faraja bali machungu kwa pande zote, na kutaka busara
iwaongoze kuchagua njia inayojenga, yenye faida, furaha na faraja kwa wote.

No comments: