Wednesday, November 23, 2011

Jukwaa la Katiba kuandamana nchi nzima

JUKWAA la Katiba nchini limesema Jumamosi litafanya maandamano ya amani nchi nzima yenye lengo la kumwomba Rais Jakaya Kikwete, asisaini Muswada wa Sheria wa Mabadiliko ya Katiba 2011.

Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deus Kibamba, alisema hayo jana Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari akitoa msimamo wa Jukwaa kuhusu Muswada huo.

Alisema wanamwomba Rais asiusaini kwa kuwa wananchi wengi watakosa fursa ya kushiriki mchakato kuanzia hatua ya msingi na hivyo kujenga chuki baina ya Serikali na wananchi.

“Maandamano haya yatafanyika nchi nzima katika maeneo mbalimbali na kwa Dar es Salaam yataanzia viwanja vya Mnazi Mmoja kuelekea Jangwani,” alisema Kibamba.

Alisema kwa kutousaini, Rais atakuwa amelinda Katiba ya sasa ambayo inatambua kuwa wananchi ndio wenye mamlaka ya mwisho juu ya jambo lolote linalohusu maslahi yao na Taifa lao.


Kuhusu kibali cha maandamano, Kibamba alisema yameandaliwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi, ambayo inalinda Watanzania katika kutoa maoni, kwani Ibara ya 18 hadi 22 inatamka kuwa kila raia ana haki ya kutoa maoni na ya kukusanyika.

Alisema Jukwaa hilo limepeleka barua kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) likimtaarifu kuhusu maandamano hayo ya amani na kushauri kuwa ili yafanikiwe ni vema askari watakaokuwapo wavae kiraia ili wasitishe wananchi na kusababisha vurugu.

Alipoulizwa kama ana taarifa na barua ya Jukwaa la Katiba, Kamishna wa Polisi wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, alisema Jeshi hilo halijapata barua yoyote kutoka kwa Jukwaa hilo inayoelezea maandamano hayo na kwamba litasimamia utekelezaji wa kanuni na taratibu zilizopo.

Kibamba alisema maandamano hayo ni ya wananchi na kwamba silaha yao ni hoja watakazozitoa na watazisimamia kwa sala.

Kuhusu Muswada huo, Kibamba alisema Jukwaa linalaani maelezo yasiyokuwa na ukweli yaliyotolewa na baadhi ya wabunge na viongozi wa Serikali dhidi yao kwamba kauli zilizotolewa kwa nyakati tofauti na Jukwaa zimeupotosha umma kwa kutaka Muswada huo usomwe mara ya kwanza na si mara ya pili.

“Kauli hizo za kupinga Jukwaa haziwaelezi wananchi ukweli, bali zimetolewa kiitikadi, kwa maslahi binafsi ya kisiasa na si kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa jumla,” alisema Kibamba.

Hata hivyo alisema Jukwaa litaendelea kusema ukweli kwamba Muswada haukupaswa kusomwa kwa mara ya pili bungeni kabla ya kufikishwa kwa wananchi vijijini na mijini, kwa sababu ulikuwa umeandikwa kwa Kiswahili kwa mara ya kwanza na hivyo ushiriki wa wananchi ungetoa fursa kwa wote kutengeneza msingi imara wa kuandika Katiba mpya.

Wiki iliyopita, Rais Kikwete akizungumza na wazee wa Dar es Salaam, alisema Muswada huo haukuondolewa bungeni, hivyo kutokana na hilo, hapakuwa na sababu ya kurudia kusomwa mara ya kwanza kwa mujibu wa taratibu za Bunge.

Alisema baada ya Muswada kupitishwa na Bunge, utawasilishwa kwake ili kusainiwa uwe sheria na baada ya hapo itabaki kazi yake na Rais wa Zanzibar kuunda Tume, ili mapema mwakani kazi ya kukusanya maoni ya wananchi ianze.

Alisema lengo ni kuwa ifikapo mwaka 2014 kazi iwe imekamilika ili mwaka 2015 Uchaguzi Mkuu ufanyike chini ya Katiba mpya na kuwasihi Watanzania kujiandaa kutoa maoni kwenye Tume ya Katiba mara itakapoanza kazi.

Rais alisema njia ya maandamano na vurugu si ya busara kwani haijengi bali inabomoa, haina faida bali hasara nyingi, haina faraja bali machungu kwa pande zote, na kutaka busara iwaongoze kuchagua njia inayojenga, yenye faida, furaha na faraja kwa wote.

No comments: