Friday, November 25, 2011

TAMWA Yawakutanisha Wahariri Kujadili Ukatili Wa Kijinsia

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Bi. Ananilea Nkya (kulia) akizungumza katika warsha ya wahariri wa habari kutoka vyombo mbalimbali walipokutana kujadili vitendo vya Unyanyasaji wa Kijinsia jijini Dar es Salaam Novemba 23, 2011.


Baadhi ya wahariri wa habari kutoka vyombo anuai nchini Tanzania walipokutana Novema 23, 2011 kwenye semina kujadili masuala ya Ukatili wa Kijinsia, semina hiyo iliandaliwa na TAMWA kwa kushirikiana na UNFPA.

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) jana kimewakutanisha wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini kujadili ukatili wa kijinsia kwa jamii. Hatua hii ni moja ya programu ya Kihistoria ya Siku 16 za wanaharakati kupinga ukatili wa kijinsia kwa jamii ambayo ilianzishwa tangu mwaka 1991 na Kituo cha Kimataifa cha Wanawake katika Uongozi (Centre for Women’s Global Leadership). Akizungumza katika semina hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya amesema lengo la semina kwa wahariri hao ni kuhakikisha wanafahamu mchango wa wanaume katika kupambana na ukatili wa kijinsia nchini Tanzania. Akifafanua zaidi Mkurugenzi huyo alisema lengo lingine ni kuhakikisha wahariri wanakuwa mstari wa mbele kuanzia Novemba 23 hadi Desemba 10 kuwaamsha kiutendaji pande husika kuchukua hatua juu ya vitendo hivyo vya kikatili. Aidha mada anuai zimetolewa kwa washiriki ili kujenga uelewa juu ya namna ya kutumia nafasi zao kwa vyombo vya habari na kuleta mabadiliko katika suala zima la ukatili wa kijinsia ambalo limekuwa likiwaathiri zaidi wanawake na wanafunzi hasa wa kike.Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia ni “Miaka 50 ya Uhuru: Pinga Ukatili Kuimarisha Tanzania Huru”.

No comments: