Thursday, November 10, 2011

CCM yahoji msimamo wa Chadema kuhusu Ushoga

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutoa msimamo wao kuhusu ushoga hasa kutokana na urafiki uliopo baina ya chama hicho na Chama cha Conservative cha Uingereza kinachoongozwa na Waziri Mkuu, David Cameron.

Kauli hiyo ya CCM imetokana na kauli ya Cameron aliyoitoa hivi karibuni katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Madola uliofanyika Perth nchini Australia, akieleza kuwa Uingereza itasitisha misaada kwa nchi zisizotekeleza haki za binadamu ikiwemo yaki za ndoa ya jinsi moja.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Mnauye akizungumza na gazeti hili jana alisema kwa muda mrefu, Chadema imekuwa rafiki wa karibu wa chama cha Conservative, hivyo ni vyema ikafahamika msimamo wao ili wananchi na jamii ijue.

“Msimamo wa CCM haupingani na wa Serikali kwamba hatukubaliani na suala hilo kamwe, ila ndugu zetu hawa wa Chadema ni maswahiba zaidi wa Conservative, mwito wa CCM ni kuitaka Chadema itoe kauli yao waseme wanasimamia wapi katika hili, kama ujuavyo tabia za marafiki hufanana, ili Watanzania wajue wakiwapa dhamana itakuwaje katika hili,” alisema Nape.

Lakini Chadema kwa upande wao, wameeleza kwamba msimamo wao ulishawekwa wazi na viongozi wa ngazi za juu akiwemo Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, John Mnyika kuwa hawakubaliani nalo na kamwe utamaduni wa kinyume cha maadili hawaukubali.

Mkurugenzi wa Sera na Utafiti, Waitara Mwikwabe, alikiri jana kwamba Chadema ina urafiki na Conservative na kueleza kuwa urafiki ni baina ya chama na chama na si Serikali na kwamba Cameron alizungumza kwa niaba ya Serikali ya Malkia Elizabeth II na si kwa niaba ya chama.

“CCM watofautishe mambo mawili, kuna kauli ya Serikali na chama, lakini pia waache unafiki, mbona mtoto wa Malkia (Prince Charles) alikuwa hapa nchini, amekuwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, amekunywa chai na Rais Jakaya Kikwete na misaada wamepokea, wala hajaja kusalimia Chadema? Hiyo ni Serikali na si chama,” alisema Mwikwabe.

Miongoni mwa vyama vyenye nguvu nchini Uingereza ni Conservative, Liberal Democrats Party na Labour Party ambapo chama cha Labour ni rafiki zaidi wa CCM.

No comments: