RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete hatimaye leo, Novemba 29, 2011, ametia saini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011, muswada ambao Chama cha Demokrasia na Maendeleo kiliugomea bungeni.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo zimetolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, imesema hatua hiyo ya kutia saini Muswada huo inakamilisha safari ya kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 baada ya Bunge kuwa limepitisha Muswada huo uliowasilishwa na Serikali katika kikao kilichopita cha Bunge.
Aidha, kutiwa saini kwa Muswada huo ili uwe Sheria ni hatua kubwa na muhimu katika safari ya kutungwa kwa Katiba mpya ya Tanzania kama ilivyoahidiwa na Rais Kikwete katika salamu zake za Mwaka Mpya kwa wananchi Desemba 31, mwaka jana, 2010.
Hata hivyo Rais Kikwete amesema pamoja na kutiwa saini hiyo bado Serikali itaendelea kusikiliza maoni na mawazo ya wadau na wananchi mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha sheria hiyo.
Pia Rais Kikwete ametoa wito kwa mwananchi yoyote mwenye maoni ama mawazo ya namna ya kuboresha Sheria hiyo, ajisikie yuko huru kutoa maoni yake na Serikali itasilikiza na kuchukua hatua zipasazo.
Hata hivyo tayari Rais Kikwete alifanya mazungumzoa na viongozi waandamizi wa CHADEMA, ambapo waliwasilisha mapendekezo yao kuhusu muswada huo na Rais kukubali kuendelea kuboresha zaidi sheria hiyo.
Pamoja na makubaliano hayo ya CHADEMA na Serikali kupita haijajulikana kama yataingizwa sasa katika kipindi hiki cha kuelekea kuundwa kwa tume au hapo baadaye.
No comments:
Post a Comment