ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) David Mattaka na vigogo wenzake wawili wa zamani wa shirika hilo, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakidaiwa kununua magari chakavu 26 kinyume cha sheria ya ununuzi.
Washitakiwa wengine ni aliyekuwa Kaimu Mhasibu Mkuu, Eliasaph Ikomba na aliyekuwa Mkurugenzi wa Mahesabu, William Haji.
Washitakiwa hao jana walisomewa mashitaka na waendesha mashitaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ben Lincon na Osward Tibabyekomya, na baadaye kuachiwa kwa dhamana walipotimiza masharti.
Katika mashitaka ya kwanza, washitakiwa wote walidaiwa kati ya Juni 2007 na Julai 2007 katika Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, kwa nyadhifa walizokuwa nazo, walishindwa kutunza kumbukumbu ya taarifa za kukubali zabuni ya ununuzi wa magari chakavu 26 yenye thamani ya dola 809,300 za Marekani, sawa na zaidi ya Sh bilioni 1.4.
Katika mashitaka ya pili, wote walidaiwa kwamba kati ya Julai 2 na Agosti 23, 2007 Ilala, kwa nyadhifa zao katika ATCL, walishindwa kufuata sheria ya ununuzi waliponunua magari hayo 26.
Pia katika mashitaka ya tatu yaliyomhusu Mattaka peke yake, ilidaiwa kuwa kati ya Julai 2 na Agosti 23, 2007 akiwa Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, kwa kukusudia alitumia madaraka yake vibaya na kuruhusu ununuzi wa magari hayo kutoka kwa Kampuni ya Bin Dalmouk Motors ya Dubai, Falme za Kiarabu, bila ridhaa ya wajumbe wa Bodi ya Zabuni.
Magari hayo ni Toyota Coster za mwaka 1993, 1996 na 1997; Toyota Hiace za mwaka 1998 na 1994; Toyota Corolla mbili za mwaka 1999; Mercedes-Benz ya mwaka 2001; Volvo ya mwaka 2003 na Toyota Land Cruiser 14 za mwaka 1998 na mwaka 1999.
Baada ya kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Rita Tarimo, mawakili wa utetezi, Peter Swai na Alex Mgongolwa, waliomba dhamana kwa washitakiwa hao, huku mshitakiwa Ikomba akijiwakilisha mwenyewe kwa kuwa hakuwa na wakili.
Ingawa upande wa mashitaka haukuwa na pingamizi katika maombi ya dhamana, lakini waliiomba Mahakama katika masharti ya dhamana izingatie sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, inayotaka kwanza kutoa nusu ya fedha inayodaiwa katika hati ya mashitaka.
Ombi hilo lilipingwa na mawakili wa utetezi wakidai kwamba mashitaka yote matatu yaliyoko kwenye hati hiyo, hayazungumzii hasara iliyopatikana kifedha, haizungumzii wizi wa fedha na uharibifu wa mali yenye gharama kadhaa, hivyo si fedha wanazodaiwa washitakiwa na hivyo sheria hiyo haiwezi kutumika.
Hakimu Tarimo alikubaliana na upande wa mawakili wa utetezi, akisema hati ya mashitaka haioneshi mwajiriwa alipata hasara kiasi gani na hivyo kutupilia mbali ombi la upande wa mashitaka.
Masharti ya dhamana waliyopewa ni kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika na mmoja awe mwajiriwa katika taasisi inayotambulika, sambamba na kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni 10, masharti ambayo waliyatimiza na kuachiwa kwa dhamana.
Baada ya kutoka mahakamani, Mattaka alitoka akikimbia kamera za wanahabari zisimnase huku akifichwa na jamaa zake. Kesi hiyo itatajwa Desemba 5 mwaka huu.
Mattaka kabla ya kupata wadhifa wa ukurugenzi mkuu wa ATCL alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Pensheni la PPF.
No comments:
Post a Comment