Monday, November 21, 2011

Dokumentari ya uzazi salama kuzinduliwa

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Utepe Mweupe (White Ribbon Alliance (WRATZ), linatarajia kuzindua dokumentari itakayosaidia kuelimisha wananchi kuhusu masuala mbalimbali juu ya uzazi salama.

Dokumentari hiyo iliyopewa jina la ‘Play Your Part’ ikimaanisha Timiza Wajibu wako, iliandaliwa nchini na wataalamu mbalimbali wa sekta ya afya kutoka Hospitali ya Temeke, Hospitali ya Babati na Hospitali ya Rombo na tayari imenyakua tuzo ya kimataifa maarufu kama BOLD inayothamini mchango wa mashirika mbalimbali kwenye kuelimisha jamii zinazowazunguka juu ya uzazi salama.

Pia dokumentari hiyo iliwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali na kata walitoa maoni yao juu ya kuimarisha uzazi salama.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mratibu wa Shughuli wa WRATZ, Rose Mlay, alisema shirika hilo linatarajia kusambaza dokumentari hiyo nchi nzima ili kuelimisha kinamama juu ya kuepuka vifo wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua.

“Vifo vingi vinatokea huko vijijini ambako kinamama wengi bado hawajapata taarifa juu ya kuepuka vifo hivyo. Jitihada zetu zitasaidia sana kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia
(MDG) 4 na 5 yanayolenga kupunguza vifo vya akinamama na watoto ifikapo 2015,” alisema Mlay.

Mlay alisema vifo 168 vinatokea nchini kila siku kutokana na uzazi usio salama, 28 ya vifo hivyo wakiwa kinamama na vifo 144 wakiwa watoto wachanga.

“Filamu hii itasaidia kuelimisha wananchi juu ya kujifungulia hospitalini badala ya majumbani ambapo watu wasiyo na ujuzi wanatumika kufanya kazi hiyo. Hii ni hatari kwa kinamama,”
alieleza Mlay.

Taarifa zinaonesha kuwa ingawa nchi nyingi barani Afrika na duniani kwa ujumla zimejikita katika kupunguza vifo vya kinamama na watoto, nchi nyingi hazitoweza kupunguza vifo hivyo kwa asilimia 75 pamoja na kuhakikisha kuwa wanawake wengi wanajifungulia hospitalini ifikapo 2015.

No comments: